The chat will start when you send the first message.
1Ndipo, Yosua alipowaita Warubeni na Wagadi nao waliokuwa nusu ya shina la Manase,[#4 Mose 32:20-22; 5 Mose 3:18-20.]
2akawaambia: Mmeyaangalia yote, Mose, mtumishi wa Bwana, aliyowaagiza, mkaisikia sauti yangu na kuyatii yote, niliyowaagiza ninyi.
3Hamkuwaacha ndugu zenu siku hizi nyingi mpaka siku hii ya leo, mkaliangalia agizo la Bwana Mungu wenu lililowapasa kuliangalia.
4Sasa Bwana Mungu wenu amewapatia ndugu zenu kutulia, kama alivyowaambia; kwa hiyo geukeni, mwende zenu mahemani kwenu katika nchi hiyo, mliyoichukua, iwe yenu, Mose, mtumishi wa Bwana, aliyowapa ng'ambo ya huko ya Yordani!
5Mjiangalie tu kabisa, myafanye maagizo na Maonyo, Mose, mtumishi wa Bwana, aliyowaagiza ninyi! Ni yale ya kumpenda Bwana Mungu wenu, mkiendelea katika njia zake zote, mkiyaangalia maagizo yake na kugandamana naye, tena mkimtumikia kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote.
6Kisha Yosua akawabariki, akawapa ruhusa kwenda zao, nao wakashika njia kwenda mahemani kwao.
7Nusu ya shina la Manase Mose aliwapa kukaa huko Basani, nayo nusu ya pili Yosua aliwapa kukaa na ndugu zao ng'ambo ya huku ya Yordani inayoelekea baharini; hawa nao Yosua aliwabariki alipowapa ruhusa kwenda mahemani kwao,
8akiwaambia kwamba: Rudini mahemani kwenu na kuyachukua mapato yenu mengi, mbuzi na kondoo wengi sana na fedha na dhahabu na shaba na vyuma na nguo nyingi mno. Hayo mliyoyateka kwa adui zenu yagawanyeni na ndugu zenu![#4 Mose 31:27.]
9Kisha Warubeni na Wagadi nao wale wa nusu ya shina la Manase wakarudi na kutoka kwao wana wa Isiraeli kule Silo ulioko katika nchi ya Kanaani, wakashika njia ya kwenda katika nchi ya Gileadi, ndiyo nchi, waliyoichukua, iwe yao, watue huko kwa kuagizwa na Bwana kinywani mwa Mose.
10Walipofika katika majimbo ya Yordani yaliyoko katika nchi ya Kanaani, wana wa Rubeni na wana wa Gadi nao wale wa nusu ya shina la Manase wakajenga huko Yordani pakubwa pa kutambikia palipoonekana hata mbali.
11Wana wa Isiraeli waliposikia kwamba: Tazameni, wana wa Rubeni na wana wa Gadi nao wale wa nusu ya shina la Manese wamejenga pa kutambikia upande wa kwao wa kuielekea nchi ya Kanaani katika majimbo ya Yordani ng'ambo ya huko, wana wa Isiraeli wapaone,
12basi, wana wa Isiraeli walipoyasikia wakakusanyika mkutano wote wa wana wa Isiraeli huko Silo, wawapandie kupiga vita.[#4 Mose 25:7.]
13Lakini kwanza wana wa Isiraeli wakatuma wajumbe kwa wana wa Rubeni na kwa wana wa Gadi na kwa wale wa nusu ya shina la Manese katika nchi ya Gileadi; waliotumwa ni Pinehasi, mwana wa mtambikaji Elazari,
14na wakuu kumi wa kwenda naye, mkuu mmoja mmoja wa milango yenye baba ya mashina yote ya Waisiraeli; nao hao wakuu kila mmoja wao alikuwa kichwa cha mlango wa baba zao miongoni mwa maelfu ya Waisiraeli.
15Walipofika kwa wana wa Rubeni na kwa wana wa Gadi nako kwao wa nusu ya shina la Manase katika nchi ya Gileadi wakasema nao kwamba:
16Hivi ndivyo, wao wa mkutano wote wa Bwana wanavyosema: Huku kuyavunja maagano, mnayomvunjia Mungu wa Isiraeli, maana yake nini? Mbona sasa mmerudi nyuma na kumwacha Bwana kwa kujijengea pa kutambikia? Basi, hivyo hamkumkataa sasa Mungu mkiacha kumtii?[#3 Mose 17:8-9; 5 Mose 12:13-14.]
17Manza, tulizozikora kwa ajili ya Peori, hazikututoshea? Nasi hata siku hii ya leo hatujajieua kwa ajili yao, ingawa mkutano wa Bwana ulipigwa naye.[#4 Mose 25.]
18Nanyi leo hivi mnarudi nyuma na kumwacha Bwana. Kweli ninyi leo hivi mnamkataa Bwana, msimtii, naye kesho ataukasirikia mkutano wote wa Waisiraeli.
19Nchi hii, mliyoichukua, iwe yenu, kama mnaiona kuwa chafu, haya! Itokeni kwenda katika nchi iliyo yake Bwana, Kao lake Bwana linakokaa, mjipatie katikati yetu nchi ya kuwa yenu! Lakini msimkatae Bwana mkiacha kumtii, wala sisi msitukatae mkiacha kututii mkijijengea pa kutambikia pasipokuwa pake Bwana Mungu wetu pa kutambikia.
20Akani, mwana wa Zera, alipouvunja ule mwiko wa kuchukua nyara, makali hayakuutokea mkutano wote wa Waisiraeli? Naye yeye hakuangamia peke yake tu kwa ajili ya hizo manza, alizozikora.[#Yos. 7.]
21Ndipo, wana wa Rubeni nao wana wa Gadi nao wale wa nusu ya shina la Manase walipowajibu na kuwaambia wale wakuu wa maelfu ya Waisiraeli:[#4 Mose 1:16; 10:4.]
22Mungu Mwenyezi ni Bwana, kweli Mungu Mwenyezi ni Bwana. Yeye anavijua, lakini Waisiraeli nao na wavijue! Kama tumemkataa Bwana kwa kuacha kumtii au kama tumemvunjia maagano, basi, Bwana, usitupatie wokovu siku hii ya leo!
23Kama tumejijengea pale pa kutambikia, tupate kurudi nyuma na kumwacha Bwana, au kwa kwamba tupate pa kutolea ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima pamoja na vipaji vya tambiko au pa kuchinjia ng'ombe za shukrani, basi, Bwana mwenyewe na atupatilize!
24Lakini hivi sivyo, ila tumevifanya hivi kwa kulihangaikia jambo hili la kwamba: Kesho wana wenu watawaambia wana wetu kwamba: Ninyi mko na bia gani na Bwana Mungu wa Isiraeli?
25Bwana aliuweka Yordani kuwa mpaka wa kututenga sisi nanyi, wana wa Rubeni na wana wa Gadi, hakuna fungu lenu lililoko kwa Bwana! Hivyo wana wenu wangewakomesha wana wetu, wasimwogope Bwana.
26Kwa hiyo twalisema: Na tujikaze kujijengea pa kutambikia! Lakini pasiwe pa kuteketezea ng'ombe nzima za tambiko wala pa kuchinjia ng'ombe zo zote za tambiko;
27ila pawe pa kutushuhudia sisi nanyi na vizazi vyetu vitakavyokuwa nyuma yetu, ya kama nasi tunamtumikia Bwana machoni pake na kumtolea ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na nyingine zinazoteketezwa vipande vipande tu, hata za shukrani, wana wenu wasiwaambie wana wetu kesho: Hakuna fungu lenu lililoko kwa Bwana.[#Yos. 24:27.]
28Kwa hiyo twalisema: Kama itakuwa, kesho watuambie sisi au vizazi vyetu maneno kama hayo, tutawaambia: Litazameni hilo jengo la mfano wa mahali pale pa kumtambikia Bwana, baba zetu walilolitengeneza, lakini hawakulitaka kuwa pa kuteketezea ng'ombe nzima za tambiko wala pa kuchinjia ng'ombe zo zote za tambiko, ila walilitaka kuwa pa kutushuhudia sisi nanyi.
29Na litukalie mbali shauri kama hilo la kumkataa Bwana, tusimtii, nalo la kurudi nyuma sasa na kumwacha Bwana, tukijijengea pa kutambikia, pawe pa kuteketezea ng'ombe nzima za tambiko na pa kutolea vipaji vya tambiko na pa kuchinjia ng'ombe nyingine za tambiko, pasipokuwa pale pa kumtambikia Bwana Mungu wetu palipo mbele ya Kao lake.
30Mtambikaji Pinehasi na wakuu wa mkutano waliokuwa vichwa vyao maelfu ya Waisiraeli waliokuwa naye walipoyasikia haya maneno, wana wa Rubeni na wana wa Gadi na wana wa Manase waliyoyasema, wakayaona kuwa mema.
31Ndipo, Pinehasi, mwana wa mtambikaji Elazari, alipowaambia wana wa Rubeni na wana wa Gadi na wana wa Manase: Leo hivi tunajua, ya kuwa Bwana yuko katikati yetu, kwa kuwa hamkumvunjia Bwana maagano kwa njia hiyo. Hivi ndivyo, mlivyowaokoa wana wa Isiraeli, mkono wa Bwana usiwapige.
32Kisha Pinehasi, mwana wa mtambikaji Elazari, akarudi pamoja na wale wakuu, wakitoka katika nchi ya Gileadi kwa wana wa Rubeni na kwa wana wa Gadi, waende katika nchi ya Kanaani kwao wana wa Isiraeli, wakawarudisha hayo majibu.
33Neno hili likawa jema machoni pao wana wa Isiraeli, kwa hiyo wana wa Isiraeli wakamtukuza Mungu, wasiseme tena: Na tuwapandie kupiga vita na kuiharibu hiyo nchi, wana wa Rubeni na wana wa Gadi wanakokaa.
34Nao wana wa Rubeni na wana wa Gadi wakapaita pale pa kutambikia Shahidi wakisema: Ndipo, panapotushuhudia, ya kuwa Bwana ni Mungu.