Yosua 23

Yosua 23

Yosua anawakusanya Waisiraeli wote, awaonye.

1Siku zilipopita nyingi tangu hapo, Bwana alipowapatia wana wa Isiraeli kutulia, wasipigane na adui zao wote waliowazunguka, Yosua akawa mzee kwa kuwa mwenye siku nyingi.[#Yos. 21:44.]

2Kwa hiyo Yosua akawaita Waisiraeli wote, wazee wao na wakuu wao na waamuzi wao na wenye amri wa kwao, kisha akawaambia: Mimi sasa ni mzee mwenye siku nyingi.

3Ninyi mmeyaona yote, Bwana Mungu wenu aliyowafanyizia hao wamizimu wote machoni penu, Bwana Mungu wenu akiwapigia vita.

4Tazameni: Nimewagawia nazo nchi zao hao wamizimu waliosalia na kuyapigia mashina yenu kura, wazipate kuwa zao toka mto wa Yordani pamoja nazo za wale wamizimu, niliokwisha kuwatowesha mpaka kwenye Bahari Kubwa, jua linakoingia.

5Bwana Mungu mwenyewe atawakumba, waondoke machoni penu, atawafukuza, msiwaone tena, mpate kuzichuua nchi zao, kama Bwana Mungu wenu alivyowaambia.

6Kwa hiyo jishupazeni sana, myaangalie na kuyafanya yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Maonyo ya Mose, msiyaache na kugeuka kuumeni wala kushotoni![#5 Mose 5:32.]

7Msiingie kwao hao wamizimu waliosalia kwenu, wala majina ya miungu yao msiyalilie, wala msiyakumbushe, wala msiyataje mkiapa, wala msiitumikie na kuiangukia![#2 Mose 23:13,24.]

8Ila gandamaneni na Bwana Mungu wenu, kama mlivyofanya mpaka siku hii ya leo!

9Naye Bwana amefukuza machoni penu mataifa makubwa yenye watu wenye nguvu, hata mmoja asiweze kusimama mbele yenu mpaka siku hii ya leo.[#3 Mose 26:7-8; 5 Mose 28:7.]

10Mtu mmoja wa kwenu hufukuza elfu wa kwao, kwani Bwana Mungu wenu ndiye anayewapigia vita, kama alivyowaambia.

11Kwa hiyo jiangalieni sana kwa ajili ya roho zenu, mmpende Bwana Mungu wenu!

12Kwani mtakaporudi nyuma na kuandamana na masao ya hao wamizimu waliosalia kwenu, mwoane nao mkiingia kwao nao wakiingia kwenu,

13ndipo mjue kabisa, ya kuwa Bwana Mungu wenu hataendelea kuwafukuza wamizimu hao, msiwaone tena, ila watakuwa mitego na matanzi ya kuwanasa na viboko vya kuwapiga mbavuni na miiba ya kuyachoma macho yenu, mpaka mwangamie katika nchi hii nzuri, Bwana Mungu wenu aliyowapa.[#4 Mose 26:55; 5 Mose 7:1-7; Amu. 2:3.]

14Tazameni, mimi sasa ninajiendea na kuishika njia yao wote walioko huku nchini. Nanyi tambueni kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote, ya kuwa yale mema yote, Bwana Mungu wenu aliyowaagia, yamewatimilia yote pia, halikuwapotelea hata moja lao![#1 Fal. 2:2; Yos. 21:45.]

15Lakini kama yale mema yote, Bwana Mungu wenu aliyowaagia, yalivyowatimilia, vivyo hivyo Bwana atawatimizia nayo yale mabaya yote, mpaka awatoweshe katika nchi hii nzuri, Bwana Mungu wenu aliyowapa.

16Hayo yatafanyika, msipolishika Agano, Bwana Mungu wenu alilowaagiza, mtakapokwenda kutumikia miungu mingine na kuiangukia, basi, hapo ndipo, makali ya Bwana yatakapowawakia, mwangamie upesi na kutoweka katika nchi hii nzuri, aliyowapa ninyi.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania