Yosua 4

Yosua 4

Yosua anajenga vikumbusho viwili vya mawe.

1Watu wote walipokwisha kuuvuka Yordani, Bwana akamwambia Yosua kwamba:

2Jichagulieni katika watu wa ukoo huu watu kumi na wawili, katika kila shina moja mtu mmoja!

3Kisha waagizeni kwamba: Chukueni katikati ya Yordani hapo, watambikaji waliposimama na kuishikiza miguu, mawe kumi na mawili, myapitishe mtoni kwenda nayo, myapeleke kambini, mtakakolala usiku huu.

4Ndipo, Yosua alipowaita wale watu kumi na wawili, aliowachagua katika wana wa Isiraeli, mtu mmoja katika kila shina moja,

5kisha Yosua akawaambia: Nendeni mbele penye Sanduku la Bwana Mungu wenu lililoko katikati ya Yordani, mjitwike kila mtu jiwe moja begani pake kwa hesabu ya mashina ya wana wa Isiraeli,

6hapo pawe kielekezo kwenu, kwani kesho wana wenu watawauliza kwamba: Haya mawe yenu maana yao nini?[#2 Mose 12:26.]

7Ndipo, mtakapowaambia: Ni kwa kuwa maji ya Yordani yalikupwa mbele ya Sanduku la Agano la Bwana, lilipouvuka Yordani; hapo maji ya Yordani yalikupwa kabisa. Ndivyo, haya mawe yatakavyokuwa kikumbusho cha wana wa Isiraeli kale na kale.

8Wana wa Isiraeli wakafanya, kama Yosua alivyowaagiza, wakachukua mawe kumi na mawili hapo katikati ya Yordani, kama Bwana alivyomwambia Yosua, kwa hesabu ya mashina ya wana wa Isiraeli, wakayapitisha kwenda nayo kambini; ndiko walikoyaweka.

9Mawe kumi na mawili mengine Yosua akayasimika katikati ya Yordani hapo chini, watambikaji waliolichukua Sanduku la Agano walipoishikiza miguu yao, nayo yako huko mpaka siku hii ya leo.

10Lakini watambikaji waliolichukua hilo Sanduku walikuwa wanasimama katikati ya Yordani, mpaka mambo yote yakamalizika, Bwana aliyomwagiza Yosua kuwaambia watu, nayo yalikuwa sawa na yale, Mose aliyomwagiza Yosua. Nao watu wakavuka mbiombio.

11Ikawa, watu wote walipokwisha kuvuka, Sanduku la Bwana nalo likavuka pamoja na watambikaji machoni pa watu.

12Nao wana wa Rubeni na wana wa Gadi nao wa nusu ya shina la Manase wakavuka wenye mata yao na kuwatangulia wana wa Isiraeli, kama Mose alivyowaambia.[#4 Mose 32:21,29.]

13Kikosi chao cha washika mata ya vita kilikuwa kama watu 40000 waliovuka machoni pa Bwana kwenda kupiga vita katika mbuga za Yeriko.

14Siku hiyo Bwana alimkuza Yosua machoni pa Waisiraeli wote, wakamwogopa, kama walivyomwogopa Mose siku zote, alizokuwapo.[#Yos. 3:7.]

15Kisha Bwana akamwambia Yosua kwamba:

16Waagize watambikaji wanaolichukua Sanduku la Ushahidi, wapande na kutoka Yordani.

17Ndipo, Yosua alipowaagiza watambikaji kwamba: Pandeni na kutoka Yordani!

18Ikawa, watambikaji waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana walipopanda na kutoka katikati ya Yordani, basi, nyayo za miguu ya hao watambikaji zilipoinuliwa kukanyaga pakavu, ndipo, maji ya Yordani yaliporudi mahali pao kuishika njia yao kama siku zote mpaka juu ukingoni pande zote mbili.

19Watu walipopanda kutoka Yordani, ilikuwa siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, wakapiga makambi Gilgali kwenye mpaka wa Yeriko wa maaawioni kwa jua.[#Yos. 5:9.]

20Kisha yale mawe kumi na mawili, waliyoyachukua mle Yordani, Yosua akayasimika Gilgali,

21akawaambia wana wa Isiraeli kwamba: Watoto wenu watakapowauliza kesho baba zao kwamba: Haya mawe maana yao nini?[#Yos. 4:6.]

22mtawajulisha hiyo maana na kuwaambia: Waisiraeli waliuvuka huu mto wa Yordani pakavu,

23kwa kuwa Bwana Mungu wenu aliyapwesha maji ya Yordani mbele yenu, mpaka mwishe kuvuka, kama Bwana Mungu wenu alivyofanya penye Bahari Nyekundu, alipoipwesha mbele yetu, mpaka tuishe kuvuka.[#2 Mose 14:21-22.]

24Ndipo, makabila yote ya nchi watakapoujua mkono wa Bwana kuwa wenye nguvu, kusudi mpate kumwogopa Bwana Mungu wenu siku zote.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania