The chat will start when you send the first message.
1Wafalme wote wa Waamori waliokaa ng'ambo ya huku ya Yordani upande wa baharini nao wafalme wote wa Wakanaani waliokaa pwani waliposikia, jinsi Bwana alivyoyapwesha maji ya Yordani mbele ya wana wa Isiraeli, mpaka waishe kuvuka, mioyo yao ikayeyuka, hakuwako mtu wa kwao asiyezimia roho kwa ajili ya wana wa Isiraeli.[#Yos. 2:24; 3:16.]
2Wakati huo Bwana akamwambia Yosua: Jitengenezee visu vya mawe makali, uwarudie wana wa Isiraeli kuwatahiri mara ya pili!
3Ndipo, Yosua alipojitengenezea visu vya mawe makali, akawatahiri wana wa Isiraeli katika Kilima cha Araloti (Tohara).
4Tena sababu yake Yosua ya kuwatahiri ilikuwa hii: watu wote waliotoka Misri waume wao wote walikuwa watu wa vita, nao walikufa nyikani njiani, walipokwisha kutoka Misri.
5Wale watu wote waliotoka walikuwa wametahiriwa, lakini wale watu wote waliozaliwa nyikani njiani, walipokwisha kutoka Misri, hawakutahiriwa.
6Kwani wana wa Isiraeli walizunguka nyikani miaka 40, mpaka wale watu wa vita wote pia waliotoka Misri walipokwisha kufa, kwa kuwa hawakuisikia sauti ya Bwana; kwa hiyo Bwana aliwaapia, wasiione ile nchi, yeye Bwana aliyowaapia baba zao, ya kama atatupa sisi, ni nchi hiyo inayochuruzika maziwa na asali.[#4 Mose 14:22-23.]
7Kisha akawainua wana wao mahali pao; wao ndio, Yosua aliowatahiri, kwani walikuwa hawajatahiriwa bado, kwa kuwa njiani hawakuwatahiri.
8Nao hao wote walipokwisha kutahiriwa, wakakaa papo hapo makambini, mpaka waishe kupona.
9Kisha Bwana akamwambia Yosua: Zile soni, Wamisri walizowapatia, nimezifingirisha, ziwaondokee ninyi. Kwa hiyo walipaita mahali pale Gilgali (Mfingirisho) mpaka siku hii ya leo.
10Wana wa Isiraeli walipokaa makambini kule Gilgali wakala sikukuu ya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi jioni kulekule katika nyika za Yeriko.[#2 Mose 12:6; 3 Mose 23:5.]
11Siku ya pili ya Pasaka wakala mazao ya nchi, mikate isiyochachwa na bisi; ndiyo, waliyoila siku hiyohiyo.
12Ndipo, Mana zilipokoma kesho yake hiyo siku, walipokula mazao ya nchi, wana wa Isiraeli wasizipate Mana tena; kwa sababu hii wakala mwaka huo mapato ya nchi ya Kanaani.[#2 Mose 16:35.]
13Ikawa, Yosua alipokuwa huko karibu ya Yeriko, akayainua macho yake na kuchungulia, mara akaona mtu aliyesimama hapo na kumtazama, namo mkononi mwake alishika upanga uliokwisha kuchomolewa. Yosua alipomwendea na kumwuliza: Wewe u mtu wa kwetu au wa adui zetu?[#4 Mose 22:23,31.]
14akasema: Sivyo, kwani mimi ni mkuu wa vikosi vya Bwana; nimefika sasa hivi. Ndipo, Yosua alipojiangusha chini kifudifudi, amwangukie, akamwuliza: Bwana wangu yuko na maneno gani ya kumwambia mtumishi wake?[#2 Mose 14:19.]
15Naye mkuu wa vikosi vya Bwana akamwambia Yosua: Vivue viatu miguuni pako! Kwani mahali hapa, wewe unaposimama, ndipo patakatifu. Yosua akafanya hivyo.[#2 Mose 3:5.]