Maombolezo 4

Maombolezo 4

Maangamizo mabaya ya Yerusalemu na ya Yuda.

1Imekuwaje, dhahabu ikichujuka,

dhahabu iliyo nzuri yenyewe ikigeuka kuwa mbaya?

Imekuwaje, vijiwe vya pambo vya Patakatifu

vikitupwa pembeni penye barabara zote?

2Vijana wa Sioni waliohesabiwa kuwa mali,

waliolinganishwa na dhahabu tupu,

imekuwaje, wakiwaziwa kuwa vyombo vya udongo

vinavyofanywa kwa mikono ya mfinyanzi?

3Mbwa wa mwitu nao hutoa maziwa

ya kuwanyonyesha watoto wao,

lakini wanawake wao walio ukoo wangu wamegeuka,

wasione uchungu kama mbuni wa nyikani.

4Ndimi za vitoto vinyonyavyo zinagandamana

na fizi zao kwa kiu;

wana wachanga wanaomba mkate,

lakini hakuna anayewamegea.

5Waliokula vya urembo wanazimia

barabarani kwa njaa,

waliokuzwa na kuvikwa mavazi mororo ya kifalme

sasa wanalala jaani.

6Manza, walizozikora wazaliwa wa ukoo wangu,

ni kubwa kuliko makosa ya Sodomu

uliogeuzwa kwa kitambo kimoja kuwa si mji tena,

lakini haikuwako mikono ya watu iliyougusa tu.

7Wakuu wao waling'aa kuliko theluji,

wakawa weupe kuliko maziwa;

miili yao ilikuwa miekundu kuliko marijani,

sura zao zilikuwa kama za jiwe la safiro;

8lakini sasa ukiwatazama, ni weusi kuliko masizi,

hawajulikani barabarani,

ngozi zao zimekunjana na kugandamana na mifupa yao,

zimekauka, zikawa kama maganda ya mti.

9Waliouawa kwa panga ndio waliopata mema,

kuliko wao waliouawa kwa njaa;

hao ndio waliozimia

wakichomwa na ukosefu wa mazao ya mashamba.

10Ikawa, wanawake wenye uchungu

wakawatokosa wana wao wenyewe kwa mikono yao,

wawe chakula chao hapo,

wazaliwa wa ukoo wangu walipovunjwa.

11Bwana ameyatimiza machafuko yake,

akayamwaga makali yake yenye moto;

hivyo ndivyo, alivyowasha moto Sioni

ulioila nayo misingi yake.

12Wafalme wa nchi nao wote wakaao humu ulimwenguni

kwao hakuwako aliyeitikia kwamba:

Malangoni mwa Yerusalemu ataingia

ausongaye au adui ye yote.

13Hayo yamefanyika kwa ajili ya makosa ya wafumbuaji

wake

na kwa ajili ya maovu, watambikaji waliyoyafanya

walipomwaga mwake katikati

damu zao waliokuwa waongofu.

14Wakatangatanga barabarani kama vipofu,

kwa kuwa walijichafua kwa damu,

watu wasiweze kabisa kuzigusa nguo zao.

15Mwondokeeni mchafu! Ndivyo, watu walivyotangaza mbele

yao.

Ondokeni! Ondokeni! Msiwaguse!

Walipopiga mbio na kutangatanga hivyo,

watu wakasema nako kwa wamizimu: Wasikae tena kuwa wageni

wetu!

16Macho ya Bwana yenye ukali yakawatenga,

naye hatawatazama tena;

kwani hawakuwaheshimu watambikaji,

wala wazee hawakuwahurumia.

17Nasi macho yetu yakafifia yasipokoma kuutazamia msaada wetu,

lakini haukupatikana;

katika kilindo chetu tukaendelea kuchungulia taifa,

lakini halikuwako lililoweza kutuokoa.

18Wakazinyatia nyayo zetu,

tusiweze kwenda katika barabara zetu;

mwisho wetu uko karibu, siku zetu zimetimia,

kwani mwisho wetu umefika.

19Watukimbizao ni wepesi

kuliko tai wa mbinguni,

wakatufukuza nako milimani juu

na kutuvizia nyikani.

20Aliyekuwa kama pumzi puani mwetu yeye aliyepakwa

mafuta na Bwana

akanaswa katika mashimo yao;

ni yeye, tuliyemsema:

Kivulini kwake tutakaa kwenye makabila ya watu

21Furahi na kujichekelea, binti Edomu,

ukaaye katika nchi ya Usi!

Wewe nawe kitakufikia hiki kinyweo,

ulewe, mpaka ujikalishe mwenye uchi.

22Manza, ulizozikora, binti Sioni, zimemalizika:

Bwana hatakutoa tena, uhamishwe.

Manza, ulizozikora, binti Edomu, atakupatilizia

atakapoyavumbua makosa yako.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania