3 Mose 10

3 Mose 10

Wana wawili wa Haroni wanauawa na moto wa Bwana.

1Wana wa Haroni, Nadabu na Abihu, wakachukua kila mtu chetezo chake, wakavitia moto, wakaweka mavukizo juu yake, wakamtolea Bwana moto huu mgeni, Bwana asiowaagiza.

2Ndipo, moto ulipotoka mbele ya Bwana, ukawala; ndivyo, walivyokufa mbele ya Bwana.[#4 Mose 16:35; 2 Mambo 26:16-20.]

3Ndipo, Mose alipomwambia Haroni: Haya ndiyo, Bwana aliyoyasema kwamba: Nitajikatasa kwao, nitukuke mbele ya watu wote wa ukoo huu. Naye Haroni akanyamaza kimya.[#1 Petr. 4:17.]

4Kisha Mose akamwita Misaeli na Elsafani, wanawe Uzieli aliyekuwa baba mdogo wa Haroni, akawaambia: Njoni, mwachukue ndugu zenu na kuwaondoa hapa Patakatifu, mwapeleke nje ya malago.[#2 Mose 6:22; Tume. 5:6-10.]

5Wakaja, wakawachukua kwa shati zao na kuwapeleka nje ya malago, kama Mose alivyosema.

6Kisha Mose akamwambia Haroni na wanawe Elazari na Itamari: Nywele zenu za vichwani msiziache wazi, wala mavazi yenu msiyararue, msife, Bwana asiukasirikie mkutano wote. Ndugu zenu, wao wote walio wa mlango wa Isiraeli, na waomboleze kwa hivyo, walivyoteketezwa, Bwana mwenyewe akiwateketeza.

7Lakini ninyi msitoke hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, msife! Kwani mmekwisha kupakwa mafuta ya Bwana. Nao wakafanya, kama Mose alivyowaagiza.

Mambo yawapasayo watambikaji.

8Bwana akamwambia Haroni kwamba:

9Mvinyo au kileo kingine usinywe wewe wala wanao, ulio nao, mkiingia Hemani mwa Mkutano, msife! Huu ndio mwiko wa kale na kale wa vizazi vyenu,[#Ez. 44:21; 1 Tim. 3:3; Tit. 1:7.]

10mpate kuyapambanua yaliyo matakatifu nayo yaliyo ya watu wote, tena yaliyo machafu nayo yatakayo,

11mpate kuwafundisha hata wana wote wa Isiraeli maongozi yote, Bwana aliyowaambia kinywani mwa Mose.

12Mose akamwambia Haroni na wanawe Elazari na Itamari, ndio waliosalia: Twaeni vilaji vya tambiko vitakavyosalia penye moto wa Bwana, mvile hivyo visivyochachwa kando ya meza ya kutambikia! Kwani ndivyo vitakatifu vyenyewe.

13Mtavila mahali patakafifu, kwani ni haki yako na haki ya wanao kuvipata penye mioto ya Bwana, kwani nimeagizwa hivyo.[#3 Mose 2:3.]

14Navyo vidari vilivyopitishwa motoni na mapaja yaliyonyanyuliwa hayo mtayala mahali panapotakata, wewe na wanao wa kiume na wa kike, kwani hii ni haki yako na ya wanao, yatolewe katika ng'ombe za tambiko za shukrani za wana wa Isiraeli, myapate.[#3 Mose 7:34.]

15Mapaja ya kunyanyuliwa na vidari vya kupitishwa motoni kwanza wayapeleke hapo, mafuta yanapochomwa moto, wavipitishe motoni mbele ya Bwana hivyo vipaji vya tambiko vya kupitishwa motoni. Kuvipata hivi itakuwa haki yako na ya wanao ya kale na kale, kama Bwana alivyoagiza.

16Mose alipomtafuta sana dume la mbuzi aliyetolewa kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo aliona, ya kuwa amekwisha kuteketea; ndipo, alipowakasirikia wale wana wa Haroni waliosalia, Elazari na Itamari, akawaambia:

17Mbona hamkuila ng'ombe ya tambiko ya weuo mahali patakatifu? Kwani ndio takatifu yenyewe, nayo ndiyo, Bwana aliyowapa ninyi, mziondoe manza za mkutano na kuwapatia upozi mbele ya Bwana.

18Tazameni, damu yake haikupelekwa Patakatifu ndani ninyi iliwapasa kuila mahali patakatifu, kama nilivyoagiza.[#3 Mose 6:26-29.]

19Haroni akamwambia Mose: Tazama, leo walipozitoa ng'ombe zao za tambiko za weuo na za kuteketezwa nzima mbele ya Bwana, yalinipata mambo kama hayo! Kama leo ningalikula ng'ombe ya tambiko ya weuo, sijui, kama ingalifaa machoni pake Bwana.

20Mose alipolisikia neno hili, likawa jema machoni pake.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania