3 Mose 11

3 Mose 11

Nyama wenye kutakata na wenye uchafu.

(Taz. 5 Mose 14:2-21.)

1Bwana akasema na Mose na Haroni, akawaambia:[#1 Mose 7:2; Tume. 10:14-15.]

2Waambieni wana wa Israeli kwamba: Katika nyama wote walioko nchini mtakula hawa wenye miguu minne:[#Kol. 2:16; 1 Tim. 4:4.]

3wote wenye kwato zilizopasuka na kutengeka kabisa, kama ni wenye kucheua, mtawala.

4Lakini miongoni mwao wenye kucheua wapasukao kwato msiwale hawa: Ngamia; kweli anacheua, lakini hazipasui kwato zake vema, kwa hiyo ni mwiko kwenu.

5Pelele; naye anacheua, lakini hazipasui kwato, kwa hiyo ni mwiko kwenu.

6Sungura; naye anacheua, lakini hazipasui kwato, kwa hiyo ni mwiko kwenu.

7Nguruwe; kweli anazipasua kwato na kuzitenga kabisa, lakini hacheui, kwa hiyo ni mwiko kwenu.

8Nyama zao hao msizile, nayo mizoga yao msiiguse! kwani wao ni mwiko kwenu.

9Katika nyama wote waliomo majini mtakula hawa: wote wenye mapezi na magamba waliomo majini baharini na mitoni mtawala.

10Lakini wote wasio wenye mapezi na magamba waliomo baharini na mitoni miongoni mwao viumbe vyote vinavyotembea majini namo miongoni mwao nyama wote waliomo majini na wawe tapisho kwenu.

11Kweli na wawe tapisho kwenu! Nyama zao msizile, nayo mizoga yao na mwione kuwa tapisho;

12wote waliomo majini wasio wenye mapezi na magamba wawe tapisho kwenu.

13Namo katika ndege wamo, mtakaowaona kuwa tapisho, hawaliki kwa kuwa tapisho: kozi na pungu na furukombe,

14na tumbuzi na mwewe na ndugu zake,

15na makunguru yote na ndugu zao,

16na mbuni na kinega na dudumizi na kipanga na ndugu zake,

17na mumbi na shakwe na bundi,

18na yangeyange na korwa na tai,

19na korongo na kitwitwi na ndugu zake na hudihuda na popo.

20Wadudu wote wenye mabawa wanaokwenda kwa miguu minne wawe tapisho kwenu.

21Katika wadudu wote wenye mabawa wanaokwenda kwa miguu minne mtawala wao tu walio wenye miguu miwili mirefu ya kurukia nchini inayokaa penye miguu yao mingine juu kidogo.

22Mtakaowala miongoni mwao, ndio panzi na ndugu zao na nzige na ndugu zao na senene na ndugu zao na funutu na ndugu zao.

23Lakini wadudu wote wengine wenye mabawa wanaokwenda kwa miguu minne wawe tapisho kwenu.

24Kwao hao mtajipatia uchafu; kila atakayegusa mizoga yao atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.[#3 Mose 5:2; 14:46.]

25Naye kila atakayechukua mzoga wao mmoja miongoni mwao sharti azifue nguo zake, naye atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

26Kila nyama mwenye kwato zilizopasuka pasipo kutengeka kabisa nao wasiocheua ndio walio wachafu kwenu; kila atakayewagusa atakuwa mwenye uchafu.

27Nao nyama wote wenye miguu minne wanaokanyaga kwa nyayo ndio walio wachafu kwenu; kila atakayegusa mizoga yao atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

28Naye atakayechukua mizoga yao sharti azifue nguo zake, naye atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Hao ndio walio wachafu kwenu.

29Tena katika nyama wadogo wanaotambaa juu ya nchi ndio hawa watakaokuwa wachafu kwenu: Fuko na panya ma mjusi na ndugu zao:

30guruguru na kenge na mbulu na goromoha na kinyonga.

31Hawa ndio walio wachafu kwenu katika nyama watambaao. Kila atakayewagusa wakiisha kufa atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

32Hata kila kitu, hawa watakachokiangukia wakifa, kitakuwa chenye uchafu kama ni chombo chochote cha mti au nguo au ngozi au gunia. Nacho kila chombo kinachotumiwa cha kufanyizia kazi kitiwe majini, nacho kitakuwa chenye uchafu mpaka jioni; ndipo, kitakapokuwa kimetakata tena.

33Lakini kila chombo cha udongo, ambacho mmoja wao ataanguka ndani yake, sharti wakivunje, nayo yote yaliyomo yatakuwa yenye uchafu.

34Vilaji vyote vinavyoliwa vikiingiwa na maji kama hayo ni vyenye uchafu; navyo vinywaji vyote vinavyonywewa vikiwa katika chombo kama hicho ni vyenye uchafu.

35Nacho cho chote, mzoga mmoja tu miongoni mwao utakachokiangukia, ni chenye uchafu; kama ni jiko la kuchomea mikate au la kupikia, sharti libomolewe, maana ni lenye uchafu, hata kwenu sharti liwe lenye uchafu.

36Lakini chemchemi na mashimo, maji yalimokusanyika, yatakuwa yametakata; lakini atakayeigusa mizoga yao akiyatoa humo atakuwa mwenye uchafu.

37Tena kama mzoga mmoja miongoni mwao utaangukia mbegu zo zote za kupanda, watu wanazotaka kuzipanda, zitakuwa zimetakata.

38Lakini kama mzoga mmoja miongoni mwao utaziangukia hizo mbegu, zikiisha lowekwa, sharti ziwe chafu kwenu.

39Tena mmoja wao hao nyama, mnaowala, akifa, atakayeugusa mzoga wake atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

40Atakayekula nyama ya mzoga wake sharti azifue nguo zake, tena atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni. Naye atakayeuchukua mzoga wake sharti azifue nguo zake, tena atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.[#2 Mose 22:31.]

41Nyama wadogo wanaotambaa juu ya nchi wote pia wawe tapisho kwenu, wasiliwe.

42Wote wanaojikokota tumboni nao wote wanaokwenda kwa miguu minne nao wote wenye miguu mingi zaidi, wale wadudu wote wanaotambaa juu ya nchi msiwale, kwani ndio tapisho.

43Msijifanye wenyewe kuwa tapisho kwa ajili ya hao wadudu watambaao, wala msijipatie uchafu kwa ajili yao mkichafuliwa nao.

44Kwani mimi ni Bwana, Mungu wenu, kwa hiyo sharti mjitakase, mwe watakatifu, kwani mimi ni mtakatifu. Msijipatie uchafu wenyewe kwao hao wadudu wote wanaotambaa juu ya nchi.[#3 Mose 19:2.]

45Kwani mimi ndiye Bwana aliyewatoa ninyi katika nchi ya Misri na kuwapandisha kuja huku, niwe Mungu wenu; kwa hiyo sharti mwe watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu!

46Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya nyama na ya ndege na ya viumbe vyote vyenye uzima vinavyotembea majini na ya wadudu wote watambaao juu ya nchi,

47mpate kuwapambanua walio wachafu nao wanaotakata, ndio nyama wanaoliwa nao wasioliwa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania