3 Mose 14

3 Mose 14

Weuo wa mtu aliyekuwa mwenye ukoma.

1Bwana akamwambia Mose kwamba:[#Mat. 8:4.]

2Haya ndiyo maonyo yampasayo mtu mwenye ukoma siku ya kueuliwa kwake: sharti apelekwe kwa mtambikaji.

3Naye mtambikaji na amtokee nje ya makambi; mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama huyu mwenye ukoma amepona ugonjwa mbaya wa ukoma,

4mtambikaji na aagize, wamletee huyo mwenye kueuliwa ndege wawili walio wazima walio wenye kutakata, tena kipande cha mwangati na nyuzi nyekundu na kivumbasi.

5Kisha mtambikaji na aagize, ndege mmoja achinjwe juu ya mtungi wenye maji ya mtoni.

6Naye ndege wa pili aliye mzima na amshike pamoja na kile kipande cha mwangati na zile nyuzi nyekundu na kile kivumbasi, avichovye vyote pamoja na ndege aliye mzima katika damu ya ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni.

7Kisha amnyunyizie mara saba yule mwenye kueuliwa aliyepona ukoma. Akiisha kumweua hivyo na amwachilie huyo ndege aliye mzima, ajiendee maporini.[#3 Mose 16:22.]

8Kisha mwenye kueuliwa na azifue nguo zake, tena na azinyoe nywele zake zote, hata koga na aoge majini. Ndipo, atakapokuwa ametakata. Baadaye ataweza kuingia makambini na kukaa siku saba nje penye hema lake.[#4 Mose 8:7.]

9Siku ya saba na azinyoe nywele zake zote za kichwani pake na ndevu zake na nyushi za macho yake, nywele zake zote pia na azinyoe, nazo nguo zake na azifue, nao mwili wake auogeshe majini; ndipo, atakapokuwa ametakata.

10Siku ya nane na achukue wana kondoo wawili wasio na kilema na kondoo jike mmoja wa mwaka mmoja asiye na kilema na vibaba kumi vya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko na nusu kibaba ya mafuta.

11Kisha mtambikaji anayeeua na amsimamishe mwenye kueuliwa pamoja na hivyo vitu vyake mbele ya Bwana penye kuliingilia Hema la Mkutano.

12Kisha mtambikaji na achukue mwana kondoo mmoja, amtoe kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi pamoja na ile nusu kibaba ya mafuta, ampitishe motoni mbele ya Bwana kuwa kipaji cha tambiko cha kupitishwa motoni.

13Kisha na amchinje huyu mwana kondoo hapo mahali patakatifu, wanapochinja ng'ombe za tambiko za weuo nazo za kuteketezwa nzima. Kwani ng'ombe ya tambiko ya upozi ni yake mtambikaji kama ile ya weuo, ni takatifu yenyewe.[#3 Mose 7:7.]

14Kisha mtambikaji na achukue damu kidogo ya ng'ombe ya tambiko ya upozi, yeye mtambikaji ampake mwenye kueuliwa pembe ya chini ya sikio lake la kuume na dole gumba la mkono wake wa kuume nalo dole gumba la mguu wake wa kuume.

15Kisha mtambikaji na achukue mafuta kidogo ya ile nusu kibaba, ayamimine katika gao lake mtambikaji la mkono wake wa kushoto.

16Kisha mtambikaji na akichovye kidole chake cha kuume katika mafuta yaliyomo katika gao lake la kushoto, ayanyunyize mara saba mafuta hayo kwa kidole chake mbele ya Bwana.[#3 Mose 4:6,17.]

17Nayo mafuta yatakayosalia gaoni mwake mtambikaji mengine na ayatumie kumpaka mwenye kueuliwa pembe ya chini ya sikio lake la kuume na dole gumba la mkono wake wa kuume nalo dole gumba la mguu wake wa kuume juu ya damu ya ng'ombe ya tambiko ya upozi.

18Nayo mafuta mengine yatakayosalia gaoni mwake mtambikaji na ampake mwenye kueuliwa kichwani; ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi mbele ya Bwana.

19Kisha mtambikaji na aitengeneze ng'ombe ya tambiko ya weuo, ampatie huyo mwenye kueuliwa upozi, uchafu wake umtoke. Baadaye na aichinje ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima.

20Kisha mtambikaji na aitoe hiyo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima pamoja na vilaji vya tambiko mezani pa kutambikia. Mtambikaji atakapokwisha kumpatia upozi hivyo, yule atakuwa ametakata.

21Lakini akiwa mkiwa, mkono wake usiyafikilie haya, basi, na achukue mwana kondoo mmoja tu kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi ya kupitishwa motoni, ajipatie upozi, na vibaba vitatu tu vya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa kilaji cha tambiko na nusu kibaba ya mafuta,

22tena hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga, kama mkono wake unavyoweza kufikilia, mmoja awe ng'ombe ya tambiko ya weuo, wa pili awe ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima.[#3 Mose 5:7.]

23Siku ya nane akiisha kuambiwa, ya kama ni mwenye kutakata, awapeleke kwa mtambikaji hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, mbele ya Bwana.

24Naye mtambikaji na amchukue mwana kondoo aliye ng'ombe ya tambiko ya upozi pamoja na ile nusu kibaba ya mafuta, yeye mtambikaji ampitishe motoni mbele ya Bwana kuwa kipaji cha tambiko cha kupitishwa motoni.

25Kisha na amchinje huyu mwana kondoo aliye ng'ombe ya tambiko ya upozi, kisha mtambikaji na achukue damu kidogo ya hiyo ng'ombe ya tambiko ya upozi, ampake mwenye kueuliwa pembe ya chini ya sikio lake la kuume na dole gumba la mkono wake wa kuume nalo dole gumba la mguu wake wa kuume.

26Kisha mtambikaji na amimine mafuta kidogo katika gao lake mtambikaji la mkono wake wa kushoto.

27Kisha mtambikaji na anyunyize kwa kidole chake cha kuume mara saba mbele ya Bwana mafuta yaliyomo katika gao lake.

28Kisha mtambikaji hayo mafuta yaliyomo katika gao lake mengine na ayatumie kumpaka mwenye kueuliwa pembe ya chini ya sikio lake la kuume, nalo dole gumba la mkono wake wa kuume, nalo dole gumba la mguu wake wa kuume hapo penye damu ya ng'ombe ya tambiko ya upozi.

29Nayo mafuta mengine yatakayosalia gaoni mwake mtambikaji na ampake mwenye kueuliwa kichwani, ampatie upozi mbele ya Bwana.

30Kisha mtambikaji na atengeneze hua mmoja au kinda moja la njiwa manga, mkono wake yule ulioweza kuwatoa.

31Hawa, mkono wake yule ulioweza kuwatoa, mmoja awe ng'ombe ya tambiko ya weuo, wa pili awe ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima pamoja na vilaji vya tambiko; hivyo ndivyo, mtambikaji atakavyompatia mwenye kueuliwa upozi mbele ya Bwana.

32Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya mtu aliyepatwa na ugonjwa huo mbaya wa ukoma, ambaye mkono wake hauwezi kuyatoa yaupasayo weuo wake.

Weuo wa nyumba iliyokuwa yenye ukoma.

33Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba:

34Mtakapoiingia nchi ya Kanaani, nitakayowapa kuwa yenu, itakuwa, nipige nyumba ya hiyo nchi, ikiisha kuwa yenu, hiyo nyumba ipatwe na ukoma;

35ndipo mwenye nyumba na afike kwa mtambikaji kumpasha habari kwamba: Nyumbani mwangu mna kitu kinachoonekana kuwa kama ugonjwa mbaya.[#3 Mose 13:2.]

36Naye mtambikaji na aagize, watoe humo nyumbani yaliyomo, yeye mtambikaji akiwa hajafika bado kuutazama huo ugonjwa mbaya, kusudi yote yaliyomo humo nyumbani yasipate kuwa yenye uchafu. Baadaye mtambikaji na aingie kuitazama hiyo nyumba.

37Akipatazama hapo palipopatwa na ugonjwa huo mbaya na kuona, ya kama ugonjwa huo mbaya umezipata kuta za hiyo nyumba na kutia vishimoshimo vyenye madoadoa ya kimajanijani au ya damudamu, navyo vikionekana kuwa vinabonyea ukutani,[#3 Mose 13:3.]

38mtambikaji na atoke humo nyumbani na kupitia hapo pa kuiingilia nyumba hiyo, kisha hiyo nyumba na aifunge siku saba.

39Mtambikaji atakaporudi siku ya saba, akiitazama na kuona, ya kama huo ugonjwa mbaya umeendelea katika kuta za nyumba hiyo,

40mtambikaji na aagize, wayatoe hayo mawe yaliyopatwa na huo ugonjwa mbaya, wayatupie mahali penye uchafu nje ya mji.

41Kisha hiyo nyumba na waikwangue po pote upande wa ndani, nazo takataka, watakazokwangua, na wazimwage mahali penye uchafu nje ya mji.

42Kisha na wachukue mawe mengine, wayatie hapo, yale mawe yalipokuwa, kisha wachukue udongo mwingine wa kuipaka hiyo nyumba.

43Ugonjwa huo mbaya utakaporudi na kutokea tena humo nyumbani, wakiisha kuyatoa mawe yote na kuikwangua hiyo nyumba na kuipaka tena,

44mtambikaji sharti aje tena; akiitazama na kuona, ya kama ugonjwa huo mbaya umeendelea humo nyumbani, basi, ndio ukoma unaokula humo nyumbani, kwa hiyo nyumba ni yenye uchafu.

45Kwa sababu hii hawana budi kuibomoa hiyo nyumba, nayo mawe yake na miti yake na takataka zote za hiyo nyumba sharti wazipeleke nje ya mji na kuzitupia mahali penye uchafu.

46Naye atakayeingia humo nyumbani, siku zote ikiwa imefungwa, atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.[#3 Mose 11:24.]

47Naye atakayelala humo nyumbani sharti azifue nguo zake, naye atakayekula humo nyumbani sharti azifue nguo zake.

48Lakini mtambikaji akiingia humo na kutazama, basi, akiona, ya kama huo ugonjwa mbaya haukuendelea humo nyumbani, walipokwisha kuipaka tena, mtambikaji hana budi kusema, ya kama hiyo nyumba imekwisha kutakata, kwa kuwa ugonjwa huo mbaya umepona.

49Kisha na achukue ndege wawili na kipande cha mwangati na nyuzi nyekundu na kivumbasi.

50Ndege mmoja na amchinje juu ya mtungi wenye maji ya mtoni.[#3 Mose 14:5-6.]

51Kisha na akichukue kile kipande cha mwangati na kile kivumbasi na hizo nyuzi nyekundu pamoja na yule ndege aliye mzima, vyote pamoja avichovye katika damu ya ndege aliyechinjwa, hata katika yale maji ya mtoni, kisha ainyunyizie hiyo nyumba mara saba.

52Ndivyo, atakavyoieua hiyo nyumba kwa damu ya ndege na kwa maji ya mtoni na kwa ndege aliye mzima na k kipande cha mwangati na kwa kivumbasi na kwa nyuzi nyekundu.

53Kisha na amwachilie yule ndege aliye mzima, ajiendee nje ya mji maporini. Ndivyo, atakavyoipatia hiyo nyumba upozi, ipate kuwa yenye kutakata.[#3 Mose 14:7.]

54Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya kila namna ya ugonjwa huo mbaya wa ukoma na wa upele mbaya,

55hata wa ukoma wa nguo na wa nyumba na wa kivimbe na wa kipele na wa balanga, watu wapate kufundishwa siku za kuwa wenye uchafu nazo siku za kuwa wenye kutakata. Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya ukoma.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania