The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:
2Sema na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Mimi Bwana ni Mungu wenu.[#2 Mose 23:24.]
3Msifanye matendo kama yale ya nchi ya Misri, mlikokaa, wala msifanye matendo kama yale ya nchi ya Kanaani, nitakakowapeleka kukaa huko, wala msiyafuate maongozi yao.
4Mtakapoyafanya maamuzi yangu na kuyaangalia maongozi yangu, myafuate, mimi Bwana nitakuwa Mungu wenu.
5Kwa hiyo yaangalieni maongozi yangu! Naye mtu ye yote atakayeyafanya maamuzi yangu atapata uzima kwa njia hiyo, maana mimi ni Bwana.[#Neh. 9:29; Ez. 20:11; Rom. 10:5; Gal. 3:12.]
6Mtu ye yote asiingie kwa mwenziwe aliye ndugu yake wa kuzaliwa naye, amfunue uchi wake. Maana mimi ni Bwana.
7Uchi wa baba yako wala uchi wa mama yako usiufunue; aliye mama yako usimfunue uchi wake.
8Uchi wa mkewe baba yako usiufunue. Kwani ndio uchi wa baba yako.[#1 Mose 35:22; 5 Mose 27:20; 1 Kor. 5:1.]
9Uchi wa umbu lako aliye binti baba yako au binti mama yako, kama amezaliwa nyumbani mwenu au nje, usiufunue uchi wao hao.
10Uchi wa binti mwanao, wa kiume au wa kike, usifunue uchi wao hao, kwani ni uchi wako mwenyewe.[#5 Mose 27:22.]
11Uchi wake binti mkewe baba yako, aliyezaliwa na baba yako, usiufunue huo uchi wake, maana ni umbu lako.
12Uchi wake umbu lake baba yako usiufunue, maana ni ndugu ya baba yako wa kuzaliwa naye.
13Uchi wa ndugu ya mama yako usiufunue. Kwani ni ndugu ya mama yako wa kuzaliwa naye.
14Uchi wa baba yako mkubwa au mdogo usiufunue, wala mkewe usimkaribie, maana ni mama yako.
15Uchi wa mkweo aliye mke wa mwanao wa kiume usiufunue huo uchi wake.[#1 Mose 38:16.]
16Uchi wa mkewe mkubwa au mdogo wako usiufunue, maana ni uchi wa ndugu yako wa kuzaliwa naye.[#Mar. 6:18.]
17Uchi wa mwanamke usiufunue pamoja nao wa mwanawe wa kike. Wala usimchukue binti mwanawe wa kiume wala binti mwanawe wa kike kuufunua uchi wake. Maana hao wanawake ni ndugu wa kuzaliwa pamoja; huo ndio uzinzi.[#5 Mose 27:23.]
18Wala usichukue mwanamke ukiwa na ndugu yake wa kike, umtie yule wivu kwa kuufunua uchi wake huyu siku zile, yule akiwa angaliko yu hai.
19Usimkaribie mwanamke aliye mwenye uchafu kwa kuwa miezini, uufunue uchi wake.[#3 Mose 15:24; Ez. 18:6; 22:10.]
20Usiingie kwa mkewe mwenzako, ulale naye na kumpa mimba, usijipatie uchafu kwake.[#2 Sam. 11:4.]
21Namo miongoni mwao walio wa uzao wako usitoe hata mmoja wa kumpa Moloki, wamwingize motoni, usipate kulichafua Jina la Mungu wako. Mimi ni Bwana.[#5 Mose 18:10; 2 Fal. 21:6; Sh. 106:37; Yer. 7:31.]
22Aliye wa kiume usilale naye, kama unavyolala na mwanamke, maana hayo ni matapisho.[#1 Mose 19:5; Rom. 1:27; 1 Kor. 6:9.]
23Wala usije kulala na nyama ye yote ukijipatia uchafu kwake, wala mwanamke asisimame mbele ya nyama kupata mimba kwake; huo ndio uchafu mbaya zaidi.
24Usijichafue kwa mambo hayo yote! Kwani kwa kuyafanya hayo yote walijichafua wamizimu wote, nitakaowafukuza mbele yenu.
25Kwa kuwa nchi ilipata kuwa yenye uchafu, nitailipisha huu uovu wake, iwatapike waliokuwa wenyeji huko.
26Lakini ninyi yaangalieni maongozi yangu na maamuzi yangu, msiyafanye hayo matapisho yote, wala ninyi mlio wenyeji wala wageni watakaokuwa kwenu.
27Kwani matapisho hayo yote waliyafanya wao waliokuwako mbele yenu katika nchi hiyo, hata nchi ikapata kuwa yenye uchafu.
28Nanyi mtakapoyafanya, nchi itawatapika kwa kuichafua, kama ilivyowatapika wamizimu waliokuwako mbele yenu.
29Kwani wote watakaoyafanya matapisho hayo, basi, wao watakaoyafanya watang'olewa kwao walio ukoo wao.
30Kwa hiyo yaangalieni, niliyowaambia, yanayowapasa kuyaangalia, msiyafuate na kuyafanya yale maongozi yatapishayo, yaliyofanywa mbele yenu, msijipatie uchafu kwa kuyafanya. Mimi Bwana ni Mungu wenu.