The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:
2Sema na mkutano wote wa wana wa Isiraeli, uwaambie: Sharti mwe watakatifu, kwani mimi Bwana Mungu wenu ni mtakatifu.[#3 Mose 11:44-45; Mat. 5:48; 1 Petr. 1:15-16.]
3Mtu sharti amche mama yake na baba yake. Nazo siku zangu za mapumziko sharti mziangalie. Mimi Bwana ni Mungu wenu.[#2 Mose 20:8,12.]
4Msivigeukie vinyago vilivyo vya bure, wala msijitengenezee miungu ya shaba au ya vinginevyo vilivyoyeyushwa. Mimi Bwana ni Mungu wenu.[#2 Mose 20:3; 34:17.]
5Mtakapomtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya shukrani, sharti mwitoe hivyo, atakavyopendezwa nanyi.[#3 Mose 22:18-20.]
6Siku ya kuitoa na iliwe, hata kesho yake; lakini nyama zitakazosalia mpaka siku ya tatu na ziteketezwe kwa moto.[#3 Mose 7:15-18.]
7Lakini ikiliwa siku ya tatu, itachukiza, haitapendeza.
8Naye atakayeila atakuwa amekora manza, kwa kuwa ameichafua iliyo takatifu ya Bwana, kwa hiyo yeye mwenyewe atang'olewa kwao walio ukoo wake.
9Mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, msikate napo pembeni penye mashamba yenu kupavunia napo, wala msiokoteze viokotezo vya mavuno yenu.[#3 Mose 23:22; 5 Mose 24:19; Ruti 2:2,15-16.]
10Wala usiipukuse mizabibu yako, wala zabibu zako zilizoanguka usiziokoteze, ila uziache, ziokotezwe na wakiwa na wageni. Mimi Bwana ni Mungu wenu.
11Msiibe, wala msidanganywe, wala msiongopeane wenyewe na wenyewe.[#2 Mose 20:15-16; 1 Tes. 4:6.]
12Msiape kiapo cha uwongo na kulitaja Jina langu. Maana hivyo utalichafua Jina la Mungu wako. Mimi ni Bwana.[#2 Mose 20:7; Mat. 5:33.]
13Usimkorofishe mwenzio na kumnyang'anya. Mshahara wa kazi, uliyofanyiziwa, usilale nao, mpaka kuche.[#5 Mose 24:14-15; Yer. 22:13; Yak. 5:4.]
14Usiapize kiziwi, wala usiweke makwazo, kipofu anapopitia, ila umwogope Mungu wako! Mimi ni Bwana.[#5 Mose 27:18.]
15Msifanye mapotovu mashaurini mkiupendelea uso wa mkiwa au mkimtukuza mkuu, ila umwamulie mwenzako kwa wongofu.[#2 Mose 23:6; 5 Mose 16:19-20.]
16usitembee kwa wenzako wa ukoo, upate mtu wa kumchongea. Usitoe ushahidi wa uwongo wa kumwua mwenzako. Mimi ni Bwana.
17Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Kuonya umwonye mwenzako, kusudi usijikoseshe kwa ajili yake.[#Sh. 141:5; Mat. 18:15.]
18Usijilipize mwenyewe, wala usiwakasirikie wana wa ukoo wako, ila umpende mwenzio, kama unavyojipenda mwwenyewe. Mimi ni Bwana.[#Mat. 5:43-48; 22:39; Luk. 10:25-37; Rom. 13:9; Gal. 5:14; Yak. 2:8; Yoh. 13:34.]
19Yaangalieni maongozi yangu! Usiwaache nyama wako wa kufuga, walale pamoja na nyama wengine, wala shamba lako usilipande mbegu za namna mbili, wala mwilini mwako usivae nguo iliyofumwa kwa nyuzi za namna mbili.
20Mtu akilala kwa mwanamke kijakazi na kumpa mimba, naye alikuwa ameposwa na mtu mwingine, basi, akiwa hakukombolewa wala hakufunguliwa kujiendea, na wapatilizwe, lakini wasiuawe, kwa kuwa yule mwanamke hakufunguliwa kujiendea.
21Naye mume sharti apeleke dume la kondoo hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi ya kumtolea Bwana kwa ajili ya manza, alizozikora.
22Naye mtambikaji na ampatie upozi na kumtoa yule dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi mbele ya Bwana kwa ajili ya kosa lake, alilolikosa; ndipo, atakapoondolewa hilo kosa lake, alilolikosa.[#3 Mose 5:17-18.]
23Mtakapoingia katika nchi ile mtapanda miti yo yote yenye matunda ya kula, lakini kwanza iacheni yenye magovi yao, ndio matunda yao, miaka mitatu mwiwazie kuwa haijatahiriwa, isiliwe.
24Katika mwaka wa nne matunda yao yote pia yawe matakatifu ya kumtolea Bwana shukrani.
25Katika mwaka wa tano mtaweza kuyala matunda yao; ndivyo, mtakavyojiongezea mapato yao. Mimi Bwana ni Mungu wenu.
26Msile cho chote kilicho chenye damu bado. Msipige bao, wala msiagulie mawingu.[#3 Mose 3:17.]
27Msichege nywele pembeni vichwani penu, wala ndevu zenu msizikate pembenipembeni.[#3 Mose 21:5; 5 Mose 14:1.]
28Msijichanje chale miilini mwenu kwa ajili ya wafu, wala msijiandike nembo miilini mwenu. Mimi ni Bwana.
29Mwanao wa kike usimtie uchafu na kumzinisha, hiyo nchi isipate kuwa yenye uzinzi, hiyo nchi ikijaa ugoni.
30siku zangu za mapumziko sharti mziangalie, napo Patakatifu pangu sharti mpache. Mimi ni Bwana.
31Msiwageukie waganga wa kutiisha mizimu wa waaguaji. Msiwatafute, mkajipatia uchafu kwao. Mimi Bwana ni Mungu wenu.[#3 Mose 20:6; 5 Mose 18:10-11; 1 Sam. 28:7.]
32Mbele yake mwenye mvi sharti uinuke, naye aliye mzee sharti umheshimu usoni pake kwa kumwogopa Mungu wako. Mimi ni Bwana.
33Mgeni akikaa ugenini kwenu katika nchi yenu, msimwonee,[#2 Mose 22:21.]
34ila awe kwenu kama mwenyeji, ijapo ni mgeni akaaye ugenini kwenu. Mmpende, kama mnavyojipenda; kwani nanyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Mimi Bwana ni Mungu wenu.
35Msifanye mapotovu wala mashaurini wala kwa kutumia vipimo vya kudanganya kama mizani au vibaba.[#5 Mose 25:13-16; Fano. 11:1.]
36Sharti mtumie mizani ya sawasawa na vyuma vya kupimia vya sawasawa na pishi za sawasawa na visaga vya sawasawa. Mimi Bwana ni Mungu wenu aliyewatoa katika nchi ya Misri.
37Yaangalieni maongozi yangu yote na maamuzi yangu, myafanye! Mimi ni Bwana.[#3 Mose 18:30.]