3 Mose 2

3 Mose 2

Vilaji vya tambiko.

1Mtu akimpelekea Bwana toleo la vilaji vya tambiko sharti hilo toleo lake liwe unga mwembamba sana, alioumiminia mafuta na kuweka uvumba juu yake.

2Kisha aupeleke kwa wana wa Haroni walio watambikaji; ndipo, mtambikaji atakapochukua katika huo unga mwembamba wa kulijaza gao lake pamoja na mafuta, lakini uvumba atauchukua wote, kisha atauvukiza mezani pa kutambikia, uwe wa kumkumbushia Bwna, maana ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana.

3Lakini masao ya vilaji vya tambiko ni yao Haroni na wanawe, ndiyo matakatifu yenyewe yatokayo kwenye mioto ya Bwana.

4Lakini ukipeleka toleo la vilaji vya tambiko vilivyookwa jikoni, liwe la vikate vilivyotengenezwa pasipo chachu kwa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta au la maandazi yasiyochachwa yaliyopakwa mafuta.

5Lakini kama toleo lako ni vilaji vya tambiko vilivyokaangwa, liwe la maandazi yaliyotengenezwa pasipo chachu kwa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta;

6nawe uyakatekate vipande, kisha uvimiminie mafuta; ndivyo, vitakavyokuwa vilaji vya tambiko.

7Lakini kama toleo lako ni vilaji vya tambiko vilivyookwa katika chungu, na vitengenezwe kwa unga mwembamba na kutiwa mafuta.

8Ukitaka kumtolea Bwana vilaji vya tambiko vilivyotengenezwa hivyo, uvipeleke kwa mtambikaji, naye ataviweka mezani pa kutambikia.

9Kisha humo katika hivyo vilaji mtambikaji atanyanyua vingine, viwe vya kumkumbushia Bwana, atavivukiza mezani pa kumtambikia; ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana.

10Navyo vilaji vya tambiko vitakavyosalia vitakuwa vyao Haroni na wanawe, ndivyo vitakatifu vyenyewe, vitokavyo kwenye mioto ya Bwana.

11Vilaji vyote vya tambiko, mtakavyomtolea Bwana, visitengenezwe na kuchachwa. Kwani yote yaliyo yenye chachu au asali msiyavukize kuwa moto wa Bwana.[#3 Mose 6:17.]

12Yakiwa ni matoleo ya malimbuko, basi, nayo mtamtolea Bwana, lakini penye meza ya kutambikia yasifike juu yake kuwa mnuko wa kumpendeza.[#4 Mose 18:12.]

13Vilaji vyote vya tambiko, utakavyovitoa, uvitie chumvi, usiache kabisa, vilaji vyako vya tambiko vikose chumvi ya agano la Mungu wako, ila vilaji vyako vyote vya tambiko uvitoe, vikiwa vyenye chumvi.[#Mar. 9:49.]

14Lakini ukimtolea Bwana vilaji vya tambiko vya malimbuko, yawe masuke yaliyochomwa moto au chenga za ngano mpya, basi, hayo utayatoa kuwa vilaji vya tambiko vya malimbuko.

15Utayatia hata mafuta, kisha utaweka uvumba juu yao; ndivyo, yatakavyokuwa vilaji vya tambiko.

16Humo katika hizo chenga na yale mafuta mtambikaji atachukua mengine pamoja na uvumba wote, ayavukize yote, yawe ya kumkumbushia Bwana, maana ndio moto wa Bwana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania