3 Mose 26

3 Mose 26

Mbaraka ya Mungu.

(Taz. 5 Mose 28.)

1Msijitengenezee vinyago vilivyo vya bure! Wala msijisimamishie mifano ya Mungu iliyochongwa kwa miti wala ya nguzo zilizoyeyushwa kwa shaba, wala msijipatie katika nchi yenu mawe yenye machorochoro ya kuyaangukia. Kwani mimi Bwana ni Mungu wenu.[#2 Mose 20:4-5.]

2Siku zangu za mapumziko sharti mziangalie, napo Patakatifu pangu sharti mpache. Mimi ni Bwana.[#2 Mose 20:8.]

3Kama mtayafuata maongozi yangu, myaangalie maagizo yangu na kuyafanya,

4nitawapa mvua zenu, siku zao zitakapotimia, nchi ipate kuyatoa mazao yake, nayo miti ya mashambani ipate kuyatoa matunda yao.[#5 Mose 11:14.]

5Ndipo, siku za kupura zitakapopokelewa na siku za kuchuma zabibu, nazo siku za hayo machumo zitapokelewa na siku za kupanda, nanyi mtakula chakula chenu na kushiba, mkae katika nchi yenu na kutulia.

6Maana hiyo nchi nitaipatia utengemano, mpate kulala pasipo kustushwa, nao nyama wabaya nitawatoa katika hiyo nchi, wala upanga hautapita katika nchi yenu.

7Mtakapowakimbiza adui zenu, wataangushwa kwa panga mbele yenu.

8Watu watano wa kwenu watakimbiza mia, nao mia wa kwenu watakimbiza maelfu kumi; ndivyo, adui zenu watakavyoangushwa kwa panga mbele yenu.

9Nami nitwageukia, niwape kuzaa, mpate kuwa wengi, kwani nitalitimiza Agano langu, nililolisimika nanyi.

10Mtakula ngano za kale zilizowekwa kale, tena hizo za kale mtaziondoa tu, mpate pa kuziwekea mpya.

11Nalo Kao langu nitaliweka katikati yenu, kwa kuwa Roho yangu haitawachukia.

12Nitatembea katikati yenu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa ukoo wangu.[#2 Kor. 6:16.]

13Mimi Bwana ni Mungu wenu aliyewatoa katika nchi ya Misri, msiwe watumwa wao, nayo miti ya makongwa yenu nikaivunja, nikawapa kujiendea na kujinyosha.

Matisho ya Mungu.

14Lakini msiponisikia, msiyafanye maagizo haya yote,

15myakatae maongozi yangu, roho zenu zikichukiwa na maamuzi yangu, msiyafanye maagizo yangu yote na kulivunja Agano langu,

16ndipo, mimi nitakapowafanyizia haya: nitatuma kwenu mastusho na kifua kikuu na homa; magonjwa haya yatawapofusha macho yenu na kuzizimiza roho zenu. Mtakapopanda mbegu zenu, itakuwa ya bure, kwani adui zenu watazila.

17Nao uso wangu nitaugeuza, uwapingie, mpigwe mbele ya adui zenu, nao wachukivu wenu wawatwale; nanyi mtajikimbilia pasipo kuona aliyewakimbiza.

18Ijapo msinisikie napo hapo, nitaendelea kuwapatiliza mara saba kwa ajili ya ukosaji wenu,

19niyavunje majivuno yenu yaliyo na nguvu nikizifanya mbingu za kwenu kuwa kama chuma nayo nchi yenu kuwa kama shaba.[#5 Mose 11:17; 1 Fal. 17:1.]

20Ndipo, kazi zenu zitakapokuwa za kusumbuka bure tu, kwani nchi yenu haitatoa mazao yake, wala miti ya hiyo nchi haitazaa matunda yao.

21Ijapo hapo napo mwendelee kupingana na mimi na kukataa kusikia, nitaendelea kuwapatia mapigo yaliyo makali mara saba kwa ajili ya ukosaji wenu.

22Nitatuma kwenu nyama wa porini, wawaue watoto wenu, wawatoweshe nao nyama wenu wa kufuga, nanyi wenyewe watawapunguza, mwe wachache, nazo njia za kwenu ziwe pasipo watu.

23Ijapo hapo napo msionyeke, mkaendelea kupingana na mimi,

24basi, mimi nami nitaendelea kupingana nanyi mimi mwenyewe nikiwapiga tena mapigo yaliyo makali mara saba kwa ajili ya ukosaji wenu:[#2 Sam. 22:27.]

25nitapeleka kwenu upanga utakaowalipiza kisasi kwa kulivunja Agano; tena mtakapokusanyika mijini mwenu nitatuma kwenu ugonjwa uuao upesi, kisha mtatiwa mikononi mwa adui zenu.[#Yes. 1:20.]

26Kisha nitawanyang'anya nacho chakula kilichowaegemeza, wanawake kumi wawaokee mikate katika jiko moja, kisha watawarudishia mikate yenu na kuwapimia kwa mizani, mle pasipo kushiba.

27Ijapo hapo napo msinisikie, mkaendelea kupingana na mimi,

28nami nitaendelea kupingana nanyi kwa ukali nikiwachapua machapuo yaliyo makali zaidi mara saba kwa ajili ya ukosaji wenu,

29mzile nyama za miili yao wana wenu wa kiume nazo nyama za wana wenu wa kike.[#2 Fal. 6:28.]

30Napo penu pa kutambikia vilimani nitapabomoa, nayo mifano yenu ya jua nitaitowesha, nayo mizoga yenu nitaitupa juu ya vipande vya magogo yenu ya kutambikia, kwani Roho yangu itakuwa imechukizwa nanyi.

31Hata miji yenu nitaigeuza kuwa mabomoko tu, nazo nyumba zenu takatifu nitaziacha, ziwe peke yao tu, nisiusikie tena mnuko wenu ulionipendeza.

32Hata nchi yenu nitaiacha, iwe peke yake tu, adui zenu wapate kuistukia watakapokaa huko.

33Nanyi wenyewe nitawatawanya kwao wamizimu, kisha na mimi nitauchomoa upanga nyuma yenu; ndipo, nchi yenu itakapokuwa pori tupu, nayo miji yenu itakuwa mabomoko tu.

34Ndipo, nchi yenu itakapopendezwa na kuipata miaka yake ya mapumziko siku zile zote, itakapokuwa pori tupu, ninyi mkikaa katika nchi ya adui zenu. Hapo ndipo, hiyo nchi itakapopumzika kweli na kuilipa miaka yake ya mapumziko.[#3 Mose 25:2; 2 Mambo 36:21.]

35Siku hizo zote za kuwa pori tupu itapata kupumzika, kwa kuwa haikupumzika, ninyi mlipokaa huko na kuinyima miaka ya mapumziko.

36Nao watakaosalia kwenu nitawalegeza mioyo yao, wakikaa katika nchi ya adui zao, shindo la jani kavu linalopeperushwa na upepo liwakimbize, wakimbie, kama watu wanavyokimbizwa na upanga, waanguke, pasipo kuona aliyewakimbiza.

37Wataangukiana wenyewe kwa wenyewe, kama watu wanavyoangukiana kwa kukimbia upanga, lakini hatakuwako mwenye kuwakimbiza; nanyi hamtaweza kuwainukia adui zenu.

38Kule kwa wamizimu ndiko, mtakakoangamia, nayo nchi ya adui zenu ndiyo itakayowala.

39Nao watakaosalia watazimia na kuyeyuka katika nchi ya adui zenu kwa ajili ya manza zao, walizozikora, hata kwa ajili ya manza, baba zao walizozikora, watayeyuka na kuzimia pamoja nao.

Kwa kujuta kwao Mungu huwapokea tena.

40Ndipo, watakapoungama, ya kuwa walikora manza, baba zao walizozikora nao, walipoyavunja maagano yangu kwa kuendelea kupingana na mimi.[#5 Mose 4:30; 30:2.]

41Kwa hiyo mimi nami naliendelea kupingana nao na kuwapeleka katika nchi ya adui zao; lakini hapo, mioyo yao iliyokuwa haikutahiriwa itakapojinyenyekeza kuitikia, ya kuwa walikora manza,[#Yer. 9:26; Luk. 23:41.]

42ndipo, nami nitakapolikumbuka agano, nililolifanya na Yakobo, nalo agano, nililolifanya na Isaka, nalo agano, nililolifanya na Aburahamu, nayo nchi hiyo nitaikumbuka.[#2 Mose 2:24; 2 Fal. 13:23.]

43Lakini kwanza sharti nchi itokwe nao, ipate kuifurahia miaka yake ya mapumziko ikiwa pori tupu kwa kuachwa nao; nao kwanza sharti waitikie, ya kuwa walikora manza walipoyatupa maamuzi yangu, roho zao zikayachukia maongozi yangu.

44Lakini hapo napo, watakapokuwa katika nchi ya adui zao, mimi sitawatupa, wala sitawachukia, niwamalize kabisa na kulivunja Agano langu, nililolifanya nao, kwani mimi Bwana ni Mungu wao.

45Ila kwa kuwatakia wokovu nitalikumbuka Agano, nililolifanya na baba zao wa kwanza nilipowatoa katika nchi ya Misri machoni pa wamizimu, niwe Mungu wao mimi Bwana.[#1 Mose 15:18; 2 Mose 12:33,51.]

46Haya ndiyo maongozi na maamuzi na maonyo, Bwana aliyoyatoa kinywani mwa Mose mlimani kwa Sinai kuwa katikati yake yeye nao wana wa Isiraeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania