The chat will start when you send the first message.
1Kama toleo lake ni ng'ombe ya tambiko ya shukrani, aliyoitoa katika ng'ombe wake, kama ni wa kiume au wa kike, sharti apeleke asiye na kilema, apate kumtoa mbele ya Bwana.
2Kisha aubandike mkono wake kichwani pake toleo lake, amchinje hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, nayo damu wana wa Haroni walio watambikaji na wainyunyize pande zote juu ya meza ya kutambikia.
3Kisha na atoe katika huyo ng'ombe aliyechinjwa kuwa ng'ombe ya tambiko ya shukrani vile vipande vya kumchomea Bwana kwa moto, ni mafuta yanayoufunika utumbo pamoja na mafuta yote yanayoshikamana na utumbo,
4tena mafigo yake mawili pamoja na mafuta yanayoshikamana nayo penye nyama za viuno na kipande cha ini kilicho pamoja na mafigo; basi, haya yote na ayaondoe.
5Kisha wana wa Haroni na wayachome moto mezani pa kutambikia juu ya ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima iliyowekwa juu ya kuni zilizopangwa motoni; huu ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana.
6Lakini kama ng'ombe yake ya tambiko, anayotaka kumtolea Bwana, ameitoa katika mbuzi au kondoo, kama ni wa kiume au wa kike, sharti apeleke asiye na kilema.
7Kama anapeleka kondoo kuwa toleo lake, sharti ampeleke kumtoa mbele ya Bwana.
8Kisha aubandike mkono wake kichwani pake toleo lake, amchinje mbele ya Hema la Mkutano, nayo damu yake wana wa Haroni na wainyunyize pande zote juu ya meza ya kutambikia.
9Kisha na atoe katika kondoo aliyechinjwa kuwa ng'ombe ya tambiko ya shukrani vile vipande vya kumchomea Bwana kwa moto, ni mafuta yake: mkia wenye mafuta, wote mzima auondoe kwa kuukata hapo, ulipoungwa na mifupa ya mgongoni, tena yale mafuta yanayoufunika utumbo pamoja na mafuta yote yanayoshikamana na utumbo,
10tena mafigo yake mawili pamoja na mafuta yanayoshikamana nayo penye nyama za viuno na kipande cha ini kilicho pamoja na mafigo; basi, haya yote na ayaondoe.
11Kisha mtambikaji na ayachome moto mezani pa kutambikia; hivyo yatakuwa vilaji vya moto wa Bwana.
12Lakini kama toleo lake ni mbuzi, sharti ampeleke kumtoa mbele ya Bwana.
13Kisha aubandike mkono wake kichwani pake, amchinje mbele ya Hema la Mkutano, nayo damu yake wana wa Haroni na wainyunyize pande zote juu ya meza ya kutambikia.
14Kisha na atoe katika hilo toleo lake vile vipande vya kumchomea Bwana kwa moto: mafuta yanayoufunika utumbo pamoja na mafuta yote yanayoshikamana na utumbo,
15tena mafigo yake mawili pamoja na mafuta yanayoshikamana nayo penye nyama za viuno na kipande cha ini kilicho pamoja na mafigo; basi, haya yote na ayaondoe.
16Kisha mtambikaji na ayachome moto mezani pa kutambikia; hivyo yatakuwa vilaji vya moto vyenye mnuko unaopendeza. Mafuta yote ni yake Bwana.
17Huu ndio mwiko wa vizazi vyenu wa kale na kale mahali po pote, mtakapokaa: msile mafuta yo yote wala damu yo yote![#1 Mose 9:4; 3 Mose 7:23,26; 17:10-14; 5 Mose 12:16,23; Tume. 15:20,29.]