The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:
2Waambie wana wa Isiraeli kwamba: Mtu akikosea agizo lo lote la Bwana asilikosee kwa kusudi, akifanya yasiyofanywa, ingawa ayafanye mara moja tu, na afanye hivyo:
3Mtambikaji aliyepakwa mafuta akiwaponza watu hawa, wakore manza kwa ajili ya kukosa kwake, basi, kwa ajili ya hilo kosa lake, alilolikosa, na apeleke dume la ng'ombe aliye mwana bado, asiye na kilema, wa kumtolea Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo.
4Huyo dume atakapomfikisha mbele ya Bwana pa kuliingilia Hema la Mkutano au aubandike mkono wake kichwani pake huyo dume, kisha amchinje huyo dume mbele ya Bwana.
5Naye mtambikaji aliyepakwa mafuta na atwae damu nyingine ya huyo dume na kuiingiza Hemani mwa Mkutano.
6Kisha mtambikaji na achovye kidole chake katika damu, anyunyize damu kidogo mara saba mbele ya Bwana penye lile pazia la kupakingia Patakatifu.[#3 Mose 8:11; 14:7.]
7Kisha pembe zile za meza ya kumvukizia Bwana manukato iliyomo Hemani mwa Mkutano mtambikaji na azipake damu. Damu nyingine yote ya huyo dume aimwagie misingi ya meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko iliyopo hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano.[#2 Mose 30:1-6; 40:6.]
8Mafuta yote ya huyu dume aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo sharti ayaondoe kwake, ni yale mafuta yanayoufunika utumbo pamoja na mafuta yote yanayoshikamana na utumbo,
9tena mafigo yake mawili pamoja na mafuta yanayoshikamana nayo penye nyama za viuno na kipande cha ini kilicho pamoja na mafigo; basi, haya yote na ayaondoe.
10Kama anavyoyanyanyua katika ng'ombe aliyechinjwa kuwa ng'ombe ya tambiko ya shukrani, ndivyo, mtambikaji ayachome moto mezani pa kuteketezea ng'ombe za tambiko.
11Nayo ngozi ya huyu dume na nyama zake pamoja na kichwa chake na miguu yake na utumbo wake na mavi yake,[#3 Mose 8:17.]
12haya yote pia ya huyu dume sharti ayatoe nje ya makambi na kuyapeleka mahali panapotakata, wanapomwagia majivu ya mafuta; ndipo ayaweke juu ya kuni, ayateketeze moto. Sharti yateketezwe papo hapo, wanapomwagia majivu ya mafuta.[#3 Mose 6:11; Ebr. 13:11.]
13Mkutano wote wa Waisiraeli wakikosa neno, isipokuwa kwa kusudi, nalo hilo neno halikujulikana machoni pao wote, ya kuwa wamelikosea agizo moja tu katika maagizo yote ya Bwana wakifanya yasiyofanywa, basi, kama wamekora manza hivyo,[#4 Mose 15:24.]
14hapo kosa lao, walilolikosa, litakapojulikana, wao wa mkutano na watoe dume la ng'ombe aliye mwana bado kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, wamfikishe mbele ya Hema la Mkutano.[#Rom. 8:3.]
15Kisha wazee wa mkutano na waibandike mikono yao kichwni pake huyo dume mbele ya Bwana, kisha wamchinje huyo dume mbele ya Bwana.
16Kisha mtambikaji aliyepakwa mafuta na aiingize damu nyingine ya huyo dume Hemani mwa Mkutano.
17Kisha mtambikaji na achovye kidole chake katika damu, anyunyize mara saba mbele ya Bwana penye lile pazia la kupakingia Patakatifu.
18Kisha pembe zile za meza ya Bwana iliyomo Hemani mwa Mkutano mbele ya Bwana na azipake damu, damu nyingine yote aimwagie misingi ya meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko iliyopo hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano.
19Mafuta yake yote sharti ayaondoe kwake, ayachome moto hapo mezani pa kutambikia,
20akimfanyizia huyu dume, kama anavyomfanyizia dume mwingine aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo; hivyo ndivyo, amfanyizie huyu naye. Hivyo mtambikaji atawapatia upozi, waondolewe makosa yao.
21Kisha na amtoe huyo dume nje ya makambi, amteketeze, kama alivyomteketeza yule dume wa kwanza. Hivyo ndivyo, ng'ombe ya tambiko ya weuo wa mkutano wote inavyotolewa.[#3 Mose 4:11-12.]
22Mkuu wa watu atakapokosea agizo lo lote la Bwana Mungu wake na kufanya tendo moja tu lisilofanywa, kama hakulifanya kwa kusudi, basi, akikora manza hivyo,
23au hapo kosa lake, alilolikosa, litakapojulikana kwake kuwa ni kosa, na apeleke dume la mbuzi asiye na kilema kuwa toleo lake.
24Kisha na aubandike mkono wake kichwani pake huyo dume, kisha amchinje mahali hapo, wanapochinja mbele ya Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima; hivyo naye atakuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo.
25Kisha mtambikaji na atwae damu nyingine ya huyu ng'ombe ya tambiko ya weuo kwa kidole chake, azipake pembe za meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, nayo damu yake nyingine aimwagie misingi ya meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko.
26Nayo mafuta yake yote na ayachome moto mezani pa kutambikia kama mafuta ya ng'ombe ya tambiko ya shukrani. Ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi, aondolewe kosa lake.
27Lakini mtu aliye mtumtu tu katika nchi hii akikosa, asipokosea agizo la Bwana kwa kusudi, akifanya tendo moja tu lisilofanywa, basi, akikora manza hivyo,
28au hapo kosa lake, alilolikosa, litakapojulikana kwake kuwa ni kosa, na apeleke jike la mbuzi asiye na kilema kuwa toleo lake kwa ajili ya kosa lake, alilolikosa.
29Kisha na aubandike mkono wake kichwani pake huyo ng'ombe ya tambiko ya weuo, kisha amchinje huyo ng'ombe ya tambiko ya weuo mahali hapo, wanapochinja ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima.
30Kisha mtambikaji na atwae damu yake nyingine kwa kidole chake, azipake pembe za meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, nayo damu yake nyingine yote aimwagie misingi ya meza ya kutambikia.
31Nayo mafuta yake yote na ayaondoe, kama mafuta yanavyoondolewa katika ng'ombe ya tambiko ya shukrani. Kisha mtambikaji na ayachome moto mezani pa kutambikia, yawe mnuko wa kumpendeza Bwana. Ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi, aondolewe kosa lake.[#3 Mose 3:14-15.]
32Lakini kama anapeleka kondoo, amtoe kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo sharti apeleke jike asiye na kilema.
33Kisha na aubandike mkono wake kichwani pake huyo ng'ombe ya tambiko ya weuo kisha amchinje huyo ng'ombe ya tambiko ya weuo mahali hapo, wanapochinja ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima.
34Kisha mtambikaji na atwae damu nyingine ya huyo ng'ombe ya tambiko ya weuo kwa kidole chake, azipake pembe za meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, nayo damu yake nyingine yote aimwagie misingi ya meza ya kutambikia.
35Nayo mafuta yake yote na ayaondoe, kama mafuta ya kondoo aliye ng'ombe ya tambiko ya shukrani yanavyoondolewa, kisha mtambikaji na ayachome moto mezani pa kutambikia juu ya mioto ya Bwana. Ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi, aondolewe kosa lake, alilolikosa.