3 Mose 5

3 Mose 5

Mambo mengine ya ng'ombe za tambiko za weuo.

1Tena mtu anaweza kukosa hivi: akisikia shaurini sauti ya mwenye kuapiza, naye ni shahidi kwa kuliona lile jambo au kwa kulijua, basi, asipolieleza, atakuwa amekora manza zitakazomkalia.[#5 Mose 19:15-21.]

2Au hivi: mtu akigusa cho chote kisichotakata, kama ni mzoga wa nyama chafu wa porini au mzoga wa nyama chafu wa kufugwa au mzoga wa dudu chafu, asijue, ya kuwa amejipatia uchafu, basi, naye ni mwenye manza.[#3 Mose 11:24.]

3Au hivi: mtu akigusa uchafu wo wote wa mtu au kichafu cho chote, basi, hapo atakapokijua atakuwa ni mwenye manza.

4Au hivi: mtu akiapa kwa upuzi wa midomo tu, kama ni kwamba kufanya mabaya au mema, kwa hayo yote, mtu anayoyaapa kwa kujipuza, asijue, ya kwamba amekosa, basi, hapo atakapoyajua atakuwa ni mwenye manza kwa kosa moja kama hilo kuliko mengine.

5Na viwe hivyo: mtu, aliyekora manza kwa kosa moja kama hilo kuliko mengine, na aungame aliyoyakosea,

6kisha ampelekee Bwana malipo ya manza zake, alizozikora kwa ajili ya kosa lake, alilolikosa, akitoa katika kundi lake jike la kondoo au la mbuzi kwa ajili ya kosa lake. Ndipo, mtambikaji atakapompatia upozi, aondolewe kosa lake.

7Lakini mkono wake usipomfikilia kondoo, na ampelekee Bwana hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga kuwa ng'ombe yake ya tambiko ya weuo kwa ajili ya hilo kosa, alilolikosa, mmoja wa weuo, mmoja wa kuteketezwa nzima.

8Akiwapeleka kwa mtambikaji, huyo atatoa kwanza yule wa weuo akivunja kichwa chake hapo, kinaposhikamana na shingo, lakini hatakiondoa kabisa.[#3 Mose 1:15.]

9Nayo damu yake nyingine ya yule wa weuo atainyunyizia ukutani pake meza ya kutambikia, nyingine itakayosalia na imwagike misingini pake meza ya kutambikia. Hivyo ndivyo, anavyokuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo.

10Yule wa pili atamfanya kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima kama desturi. Hivyo ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi, aondolewe kabisa kosa lake, alilolikosa.[#3 Mose 1:14.]

11Lakini mkono wake usipowafikilia hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga, basi, toleo lake, atakalopeleka, kwa kuwa alikosa, na liwe vibaba viwili na nusu vya unga mwembamba kuwa kipaji chake cha tambiko cha weuo; asiumiminie mafuta, wala asitie uvumba juu yake, kwani ndio kipaji cha tambiko cha weuo.[#3 Mose 2:1.]

12Akiupeleka kwa mtambikaji, huyo mtambikaji na achukue humo wa kulijaza gao lake, uwe wa kumkumbushia Bwana, akiuchoma moto hapo pa kutambikia juu ya mioto ya Bwana. Hivyo nao utakuwa kipaji cha tambiko cha weuo.

13Hivyo ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi kwa ajili ya kosa lake, alilolikosa kuliko mengine, aondolewe kabisa kosa lake; nao unga uliosalia utakuwa wake mtambikaji kama ule wa vilaji vya tambiko.[#3 Mose 2:3.]

Maagizo ya ng'ombe za tambiko za upozi.

14Bwana akamwambia Mose kwamba:

15Mtu akilivunja Agano, akikosa kwa kuchukua kitu kilicho mali ya Bwana, asipovijua, na ampelekee Bwana ng'ombe yake ya tambiko ya upozi, akitoa katika kundi lake dume la kondoo asiye na kilema, unayemwona kuwa wa fedha mbili tatu zilizopimwa kwa kipimo cha Patakatifu; huyo atakuwa ng'ombe yake ya tambiko ya upozi.

16Kisha nazo mali za Patakatifu, alizozikosea kwa kuzichukua, atazilipa na kuongeza fungu la tano; zote ampe mtambikaji. Ndipo, mtambikaji atakapompatia upozi na kumtoa yule dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi, kisha ataondolewa kosa lake.[#3 Mose 6:4-5; 22:14.]

17Hata mtu akikosea agizo lo lote la Bwana, ijapo ni moja tu, kwa kufanya yasiyofanywa, asipovijua, naye atakuwa amekora manza, nao uovu wake utamkalia.

18Kwa hiyo na atoe katika kundi lake dume la kondoo asiye na kilema, unayemwona, ya kama anatosha kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi. Kisha ampeleke kwa mtambikaji, naye mtambikaji atampatia upozi kwa ajili ya kosa lake, alilolikosa pasipo kulijua kuwa ni kosa; naye akiwa hakuvijua kweli ataondolewa kosa lake.

19Basi, hii ni ng'ombe ya tambiko ya upozi, kwa maana manza, alizozikora, alizikora kwake Bwana.[#Yes. 53:10.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania