The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:
2Ikiwa, mtu akose na kumvunjia Bwana Agano akimdanganya mwenziwe kwa kuchukua amana au mengine, aliyoyaweka mkononi mwake, au akimwibia au akimwonea mwenziwe,
3au akiokota kitu kilichopotea na kuvibisha na kuapa kiapo cha uwongo, akiwa amekosa moja tu katika mambo haya, watu wanayoyakosa,
4basi, akiwa amekora manza kwa kukosa hivyo, sharti ayarudishe aliyoyakwiba nayo aliyojipatia kwa kumwonea mwenziwe, nazo amana zilizowekwa kwake, nacho kilichopotea alichokiokota,[#2 Mose 22:1-9; Ez. 33:15.]
5nayo yote, aliyoyachukua kwa kuapa kiapo cha uwongo, yote pia ayalipe swasawa, kama yalivyokuwa, kisha sharti aongeze fungu la tano. Sharti mpe yeye aliye mwenye mali hizo siku hiyo, atakapotoa ng'ombe yake ya tambiko ya upozi.[#3 Mose 5:16.]
6Hiyo ng'ombe yake ya tambiko ya upozi ampelekee Bwana akitoa katika kundi lake dume la kondoo asiye na kilema, utakayemwona, ya kama anatosha kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi; huyo na ampeleke kwa mtambikaji.[#3 Mose 5:15.]
7Naye mtambikaji atampatia upozi mbele ya Bwana; ndipo, atakapoondolewa kosa lake, alilolikosa kuliko mengine yote kwa kukora zile manza.
8Bwana akamwambia Mose:
9Umwagize Haroni nao wanawe kwamba: Haya ndiyo maongozi ya ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima: ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima sharti ikae hapo, ilipowashiwa moto juu ya meza ya kutambikia usiku kucha, nao moto wa mezani pa kutambikia sharti uangaliwe, uwake vivyo hivyo.[#3 Mose 1.]
10Naye mtambikaji na avae vazi lake la ukonge, hata suruali za ukonge na avae mwilini wake, nayo majivu ya ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima yaliyopo hapo juu ya meza ya kutambikia ayazoe, ayaweke kando ya meza ya kutambikia.[#2 Mose 28:42.]
11Kisha na ayavue mavazi yake na kuvaa mavazi mengine, ayaondoe yale majivu na kuyapeleka nje ya makambi mahali panapotakata.[#3 Mose 4:12.]
12Nao moto ulioko juu ya meza ya kutambikia uangaliwe, uwake hapo vivyo hivyo, usizimike. Kila kunapokucha mtambikaji ateketeze kuni juu yake, kisha juu yao apange ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, nayo mafuta ya ng'ombe za tambiko za shukrani ayachome moto juu yake.
13Moto na uangaliwe, uwake pasipo kukoma mezani pa kutambikia, usizimike.
14Nayo haya ndiyo maongozi ya vilaji vya tambiko: wana wa Haroni na wavipeleke kumtolea Bwana hapo mbele ya meza ya kutambikia.[#3 Mose 2.]
15Kisha atanyanyua katika unga mwembamba wa kilaji cha tambiko wa kulijaza gao lake pamoja na mafuta yake na uvumba wote ulioko juu ya kilaji cha tambiko, auvukize mezani pa kutambikia, uwe mnuko upendezao wa kumkumbushia Bwana.
16Nao unga utakaosalia wataula Haroni na wanawe, uliwe hapo mahali patakatifu pasipo kutiwa chachu; waule uani penye Hema la Mkutano.
17Usiokwe ukiwa umechachuka. Kwani nimeutoa katika mioto yangu na kuwapa, uwe fungu lao, ndio mtakatifu mwenyewe kama ng'ombe ya tambiko ya weuo nayo ya upozi.
18Wana wa Haroni wote walio wa kiume wataula; hii na iwe haki ya kale na kale ya vizazi vyenu kuupata kwenye mioto ya Bwana. Kila atakayeugusa sharti awe ametolewa kuwa mtakatifu.
19Bwana akamwambia Mose kwamba:[#2 Mose 29.]
20Hili ndilo toleo lao Haroni na wanawe, watakalomtolea Bwana siku hiyo, mmoja wao atakapopakwa mafuta: unga mwembamba pishi mbili na nusu na ziwe vilaji vyao vya tambiko vya kila siku nusu yao asubuhi, nusu yao nyingine jioni.
21Sharti uandaliwe kaangoni na kutiwa mafuta kuwa vitumbua. Kisha avipeleke na kuvimega vipandevipande; hivi ndivyo vilaji vya tambiko, utakavyovitoa, viwe mnuko wa kumpendeza Bwana.
22Mtambikaji aliyepakwa mafuta mahali pake Haroni miongoni mwa wanawe ndiye atakayevitoa; hii na iwe haki ya kale na kale ya Bwana, navyo sharti vichomwe moto vyote vizima.
23Kwani vilaji vya tambiko vyote, mtambikaji atakavyovitoa, sharti vichomwe moto vyote vizima, visiliwe.
24Bwana akamwambiaa Mose kwamba:[#3 Mose 4.]
25Mwambie Haroni na wanawe: Haya ndiyo maongozi ya ng'ombe za tambiko za weuo: mahali hapo, ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima zinapochinjwa, nazo ng'ombe za tambiko za weuo zichinjwe papo hapo mbele ya Bwana, maana nazo ni takatifu zenywe.
26Mtambikaji atakayeitoa hiyo ng'ombe ya tambiko ya weuo ndiye atakayeila; sharti iliwe mahali patakatifu uani penye Hema la Mkutano.
27Kila atakayezigusa nyama zake sharti awe ametolewa kuwa mtakatifu. Tena kama iko damu yake iliyonyunyizika katika nguo, basi, hiyo nguo iliyonyunyizwa damu sharti aifue mahali patakatifu.
28Nacho chungu, nyama zake zilimopikwa, sharti kivunjwe; kama ni cha shaba, sharti kisuguliwe na kuoshwa kwa maji.
29Watambikaji wote walio wa kiume watazila nyama zake, nazo ni takatifu zenyewe.
30Lakini ng'ombe za tambiko za weuo zote, ambazo damu zao nyingine ziliingizwa Hemani mwa Mkutano, zitumiwe za upozi mle Patakatifu, nyama zao zisiliwe, ila ziteketezwe kwa moto.