Luka 1

Luka 1

Matangulizi.

1Wengi walijaribu kuandika masimulio ya mambo yale yaliyotimilika kwetu.

2Waliyafuatafuata yale waliyoambiwa na wenye kuyaona yote kwa macho yao, yalivyokuwa tangu mwanzo, kwani walikuwa wamelitumikia lile Neno.

3Sasa nami nimeyafuata na kuyachungua yote mpaka hapo, yalipoanzia, nikaona, inafaa, nikuandikie sawasawa, kama yalivyofuatana, mwenzangu Teofilo,[#Tume. 1:1.]

4upate kutambua, ya kuwa mambo yale uliyofundishwa ni ya kweli.

Zakaria na Elisabeti.

5Siku zile, Herode alipokuwa mfalme wa Wayuda, palikuwa na mtambikaji wa chama cha Abia, jina lake Zakaria, naye mkewe alikuwa na wana wa Haroni, jina lake Elisabeti.[#1 Mambo 24:10,19.]

6Wote wawili walikuwa waongofu machoni pa Mungu, wakaendelea na kuyashika maagizo na maongozi yote ya Bwana, watu wasione la kuwaonya.

7Lakini walikuwa hawana mtoto, kwani Elisabeti alikuwa mgumba, nayo miaka yao wote wawili ilikuwa mingi.

Zakaria Nyumbani mwa Mungu.

8Chama chake kilipofikiwa na zamu, akaenda kufanya kazi yake ya utambikaji mbele ya Mungu;

9kwa desturi yao ya utambikaji yeye akapata kuvukiza, akaingia katika Jumba la Bwana.[#2 Mose 30:7.]

10Nalo kundi lote la watu wengi lilikuwa nje, wakiombea saa ileile ya kuvukiza.

11Malaika wa Bwana akamtokea akisimama mezani pa kuvukizia kuumeni kwake.

12Zakaria alipomwona akahangaika, woga ukamguia;

13lakini malaika akamwambia: Usiogope, Zakaria! Kwani ombo lako limesikiwa: mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, nawe utamwita jina lake Yohana.

14Wewe utafurahi na kushangilia, hata wengine wengi watakufurahia kuzaliwa kwake.

15Kwani atakuwa mkubwa machoni pa Bwana; pombe na vileo vyo vyote hatakunywa, lakini atajazwa Roho takatifu papo hapo, atakapozaliwa na mama yake.[#4 Mose 6:3; Amu. 13:4-5.]

16Atageuza wana wa Isiraeli wengi, warudi kwa Bwana Mungu wao.

17Mwenyewe atamtangulia Bwana akiwa mwenye roho na nguvu za Elia, aigeuze mioyo ya baba, warudi kwa watoto, awageuze nao wabishi, waufuate ujuzi wa waongofu, amlinganyizie Bwana watu waliojitengeneza.[#Mal. 3:1; 4:5-6; Mat. 17:11-13.]

18Zakaria akamwambia malaika: Haya nitayatambuaje? Maana mimi ni mzee, nayo miaka ya mke wangu imekuwa mingi.[#1 Mose 18:11; Rom. 4:19.]

19Malaika akajibu, akamwambia: Mimi ni Gaburieli ninayesimama mbele ya Mungu; nimetumwa kusema na wewe, nikupigie mbiu hii njema.[#Dan. 8:16; Ebr. 1:14.]

20Tazama, utakuwa bubu, usiweze kusema mpaka siku hiyo, hayo yatakapokuwapo, kwa sababu hukuyaitikia maneno yangu; nayo yatatimia, siku zao zitakapofika.

21Wale watu waliokuwa wakimngoja Zakaria, wakastaajabu kukawia kwake katika Jumba la Mungu.

22Alipotoka hakuweza kusema nao; ndipo, walipotambua, ya kuwa yako mambo, aliyoyaona katika Jumba la Mungu. Naye akawapungia kwa mkono, akakaa kuwa bubu.

23Ikawa, siku za utambikaji wake zilipomalizika, akaondoka, akaenda nyumbani mwake.

24Lakini baada ya siku zile mkewe Elisabeti akapata mimba, akajificha miezi mitano, akasema:

25Ndivyo, alivyonitendea Bwana siku hizi akinitazama, aiondoe soni, niliyokuwa nayo kwa watu.[#1 Mose 30:23.]

26Mwezi wa sita malaika Gaburieli akatumwa na Mungu kwenda katika mji wa Galilea, jina lake Nasareti,

27amfikie mwanamwali aliyeposwa na mume, jina lake Yosefu, wa mlango wa Dawidi; yule mwanamwali jina lake Maria.[#Luk. 2:5; Mat. 1:16,18.]

28Alipoingia mwake akasema: Salamu kwako, kwani yako uliyogawiwa! Bwana yuko pamoja na wewe uliye mwenye kipaji kinachovipita vya wanawake wengine.

29Alipohangaika kwa neno hili akifikiri kwamba: Huyu ananiamkia kwa namna gani?

30malaika akamwambia: Usiogope, Maria! Kwani umepata gawio jema kwa Mungu.

31Tazama, utapata mimba, utazaa mtoto mwana mume, nalo jina lake utamwita YESU.[#Yes. 7:14; Mat. 1:21-23.]

32Ndiye atakayekuwa mkuu, ataitwa Mwana wake Alioko huko juu, naye Bwana Mungu atampa kiti cha kifalme cha baba yake Dawidi,[#2 Sam. 7:12-13,16.]

33atautawala mlango wa Yakobo kale na kale, ufalme wake usiwe na mwisho.

34Maria akamwambia malaika: Hili litakuwaje? kwani sijajua mume.

35Malaika akajibu akimwambia: Roho Mtakatifu atakujia, nguvu zake Alioko huko juu zitakufunika kama wingu; kwa hiyo hata mtakatifu atakayezaliwa ataitwa Mwana wake Mungu.[#Mat. 1:18,20; Yoh. 8:23.]

36Tazama, naye ndugu yako Elisabeti ana mimba ya mtoto mume katika uzee wake, mwezi huu ni wake wa sita, tena alikuwa ameitwa mgumba;

37kwani hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.[#1 Mose 18:14.]

38Maria akasema: Tazama, mimi ni kijakazi wa Bwana! Yaniwie, kama ulivyosema! Kisha malaika akaondoka kwake.

39Siku hizo Maria akainuka, akaenda upesi milimani kufika katika mji wa Yuda.

40Akaingia nyumbani mwa Zakaria, akamwamkia Elisabeti.

41Ikawa, Elisabeti aliposikia, Maria anavyomwamkia, kitoto kikarukaruka tumboni mwake, kisha Elisabeti akajazwa Roho takatifu,[#Luk. 1:15.]

42akapaza sauti kwa nguvu akisema: Wewe umebarikiwa kuliko wanawake wengine, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa.[#Luk. 1:28; 11:27-28.]

43Tena ni kwa sababu gani, mama yake Bwana wangu akinijia?

44Kwani sauti yako ya kuniamkia iliponiingia masikioni, mara kitoto tumboni mwangu kilirukaruka kwa kushangilia.

45Wewe uliyemtegemea Mungu utakuwa mwenye shangwe, kwani yatatimizwa hayo, uliyoambiwa na Bwana.[#Luk. 11:28.]

Wimbo wa Maria.

46Maria akasema:

Bwana ndiye, moyo wangu unayemkuza,

47roho yangu humshangilia Mungu, mwokozi wangu.

48Maana ameutazama unyenyekevu wa kijakazi wake;

kwani tokea sasa itakuwa, wao wa vizazi vyote wanishangilie.

49Amenifanyia makuu kwa kuwa mnguvu, Jina lake ni

takatifu.

50Huruma yake huwajia vizazi kwa vizazi wamwogopao.[#Sh. 103:13,17.]

51Hufanya ya nguvu kwa mkono wake

akiwatawanya waliojikweza katika mawazo ya mioyo yao.

52Huangusha wenye nguvu katika viti vya kifalme,

lakini wao walio wanyenyekevu huwapandisha.

53Walio wenye njaa huwashibisha mema,

lakini wenye mali huwaacha, wajiendee mikono mitupu.

54Alipokumbuka huruma, akamsaidia mtoto wake Isiraeli,

55kama alivyowaambia baba zetu, akina Aburahamu

nao walio uzao wake kwamba: Wawe wa kale na kale!

56Maria akakaa kwake, yapata miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani kwake.

Kuzaliwa kwake Yohana.

57Elisabeti siku zake za kuzaa zilipotimia, akazaa mtoto mume.

58Majirani zake na ndugu zake waliposikia, ya kuwa Bwana amemwonea huruma nyingi, wakafurahi pamoja naye.

59Ilipokuwa siku ya nane, wakaja kumtahiri mtoto, wakamwita jina la baba yake: Zakaria.[#1 Mose 17:12.]

60Lakini mama yake akakataa akisema: Sivyo, sharti aitwe Yohana![#Luk. 1:13.]

61Wakamwambia: Hakuna mtu katika ndugu zako aitwaye jina hili.

62Walipompungia baba yake na kumwuliza jina, alilolitaka, mtoto aitwe,

63akataka kibao, akaandika na kusema: Yohana ndilo jina lake. Wakastaajabu wote.

64Mara hiyo akafunguka kinywa chake na ulimi wake, akasema na kumtukuza Mungu.

65Ndipo, woga ulipowashika wote waliokaa kando kando yao; mambo hayo yote yakasimuliwa milimani po pote pa Yudea.

66Wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakasema: Basi, huyu mtoto atakuwa wa namna gani? Kwani mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.

Wimbo wa Zakaria.

67Baba yake Zakaria akajazwa Roho takatifu, akafumbua yatakayokuwa akisema:

68*Atukuzwe Bwana Mungu wa Isiraeli! kwani amewakagua wao wa ukoo wake na kuwapatia ukombozi.[#Luk. 7:16.]

69Ametusimikia pembe ya wokovu katika mlango wa mtoto wake Dawidi,[#1 Sam. 2:10; Sh. 132:17.]

70kama alivyosema kale kwa vinywa vya wafumbuaji wake watakatifu.

71Akatupatia wokovu kwao walio adui zetu namo mikononi mwao wote wanaotuchukia.

72Aliwahurumia baba zetu, akalikumbuka Agano lake takatifu[#1 Mose 17:7; 3 Mose 26:42.]

73nacho kiapo chake, alichomwapia baba yetu Aburahamu kwamba:[#1 Mose 22:16-17; Mika 7:20.]

74Tupate kukombolewa mikononi mwa adui zetu, tukae pasipo woga na kumtumikia siku zetu zote[#Tit. 2:12,14.]

75tukiwa mbele yake wenye utakaso na wongofu.

76Nawe kitoto, utaitwa mfumbuaji wake Alioko huko juu, utatangulia mbele ya Bwana, uzitengeneze njia zake[#Mal. 3:1; Mat. 3:3.]

77na kuwatambulisha wao wa ukoo wake wokovu wao, ya kuwa uko katika kuondolewa makosa yao.[#Yer. 31:34.]

78Tukivipata hivi, ni kwa huruma zilizomo moyoni mwake Mungu wetu; kwa hiyo umetukagua mwanga unaotoka juu,[#4 Mose 24:17; Yes. 60:1-2; Mal. 4:2.]

79uwaangaze wanaokaa gizani kwenye kivuli kuuacho, uelekeze miguu yetu, ishike njia ya utengemano.[#Yes. 9:1-2.]

80Yule mtoto alipokua akapata nguvu Rohoni, akakaa nyikani mpaka siku, alipowatokea Waisiraeli.*[#Mat. 3:1.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania