Luka 2

Luka 2

Kuzaliwa kwake Yesu.

1*Ikawa siku zile, amri ikitoka kwa Kaisari Augusto, walimwengu wote waandikiwe kodi;

2huko kuandikwa kulikuwa kwa kwanza, kukawa siku zile, Kirenio alipotawala Ushami.

3Ndipo, watu wote waliposhika njia za kwenda kuandikiwa kodi, kila mtu akaenda mjini kwao.

4Yosefu naye akaondoka Galilea katika mji wa Nasareti kwenda Yudea katika mji wa Dawidi unaoitwa Beti-Lehemu, kwa kuwa yeye alikuwa wa mlango na wa udugu wa Dawidi.

5Akaenda pamoja na mkewe Maria aliyeposwa naye, waandikiwe kodi; naye alikuwa ana mimba.[#Luk. 1:27.]

6Ikawa, walipokaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia.

7Akamzaa mwana wake wa kwanza, ni wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza waliamo ng'ombe, kwani hawakupata pengine nyumbani mwa wageni.[#Mat. 1:25.]

8Kulikuwa na wachungaji katika nchi ileile, walilala malishoni na kulilinda kundi lao kwa zamu ya usiku.

9Ndiko, malaika wa Bwana alikowatokea, nao utukufu wa Bwana ukawamulikia po pote, wakashikwa na woga mwingi.

10Lakini malaika akawaambia: Msiogope! kwani tazameni, ninawapigia mbiu njema yenye furaha kuu itakayowajia watu wote.

11Kwani mmezaliwa leo mwokozi wenu katika mji wa Dawidi, ndiye Bwana Kristo.

12Nacho kielekezo chenu ni hiki: mtaona kitoto kichanga, kimevikwa nguo za kitoto, kimelazwa waliamo ng'ombe.

13Mara wakawa pamoja na yule malaika wingi wa vikosi vya mbinguni, wakamsifu Mungu wakiimba:[#Dan. 7:10.]

14Utukufu ni wa Mungu mbinguni juu,

nchini uko utengemani kwa watu wampendezao.

15*Ikawa, malaika walipoondoka kwao kwenda mbinguni, wachungaji wakasemezana wao kwa wao: Haya! Twende, tufike hata Beti-Lehemu, tulitazame jambo hilo lililokuwapo, Bwana alilotutambulisha!

16Wakaenda mbio, wakawakuta, akina Maria na Yosefu na kitoto kichanga, kimelazwa waliamo ng'ombe.

17Walipokwisha kumwona wakalitambulisha lile neno, waliloambiwa na kitoto hiki.[#Luk. 2:10-12.]

18Ndipo, wote walioyasikia walipoyastaajabu, waliyoambiwa na wachungaji.

19Lakini Maria akayashika maneno hayo yote, akayaweka moyoni mwake na kuyawaza.[#Luk. 2:51.]

20Kisha wachungaji wakarudi wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa yote, waliyoyasikia, kwani waliona, ni vivyo, kama walivyoambiwa.*

Kutahiriwa.

21*Siku nane za kumtahiri zilipotimia, akaitwa jina lake YESU, lililotajwa na malaika, mama yake alipokuwa hajapata mimba yake.*[#Luk. 1:31,59; 1 Mose 17:12.]

Simeoni.

22*Siku zao zilipotimia za weuo, aliouagiza Mose, wakampeleka Yerusalemu, wamtokeze kwake Bwana.[#3 Mose 12.]

23Ndivyo, ilivyoandikwa katika Maonyo ya Bwana:

Kila mtoto mume atakayezaliwa wa kwanza na mama yake

aitwe mtakatifu wa Bwana!

24Wakatoa vipaji vya kumkomboa, kama ilivyoagizwa katika Maonyo ya Bwana, hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga.[#3 Mose 12:8.]

25*Huko Yerusalemu kulikuwa na mtu, jina lake Simeoni. Mtu huyo alikuwa mwongofu mwenye kumcha Mungu, akaungoja utulivu wa Isiraeli; nayo Roho takatifu ilikuwa naye.[#Yes. 40:1; 49:13.]

26Huyo alikuwa amefumbuliwa na Roho Mtakatifu kwamba: Hutaona kufa usipomwona kwanza Kristo wa Bwana.

27Basi, akaja Patakatifu kwa kuongozwa na Roho. Wazazi walipoingia na mtoto Yesu, wamfanyie, kama walivyozoezwa na Maonyo,

28mwenyewe akampokea mikononi pake, akamtukuza Mungu akisema:

29Bwana, sasa unampa mtumwa wako ruhusa,

aende zake na kutulia, kama ulivyosema.

30Kwani macho yangu yameuona wokovu wako,

31ulioutengeneza machoni pa makabila yote:

32ni mwanga wa kuwamulikia wamizimu,

ukoo wako wa Isiraeli utukuzwe.*

33Baba yake na mama yake walipokuwa wakiyastaajabu aliyosemewa,[#Yes. 8:14; Mat. 21:42; Tume. 28:22; 1 Kor. 1:23.]

34Simeoni akawabariki, akamwambia Maria, mama yake: Tazama, huyu ndiye aliyewekewa, wengi walio Waisiraeli waangushwe naye, nao wengine wengi wainuliwe naye; tena amewekewa kuwa kielekezo kinachobishiwa.

35Nawe wewe upanga utakuchoma moyoni, kusudi mawazo yao wengi yaliyomo mioyoni mwao yafunuke.

Ana.

36Kukawa na mfumbuaji wa kike, jina lake Ana, binti Fanueli, wa shina la Aseri. Huyo miaka yake ilikuwa mingi sana; alikuwa amekaa pamoja na mumewe miaka saba baada ya kuwa manamwali.

37Tena siku hizo alikuwa mjane mwenye miaka 84, lakini hakuondoka Patakatifu akimtumikia Mungu usiku na mchana kwa kufunga na kuombea watu.[#Tume. 26:7; 1 Tim. 5:5.]

38Naye akawajia saa ileile, akamshukuru Mungu waziwazi, akawaambia mambo ya huyo mtoto wote walioungoja ukombozi wa Yerusalemu.[#Yes. 52:9.]

39Walipokwisha kuyamaliza yote yaliyoagizwa na Maonyo ya Bwana wakarudi Galilea mjini kwao Nasareti.

40Lakini yule mtoto akakua, akapata nguvu ya Roho na werevu wote wa kweli, naye Mungu akamgawia mema yake.*[#Luk. 1:80; 2:52.]

Yesu mwenye miaka 12 Nyumbani mwa Mungu.

41*Wazazi wake huenda Yerusalemu kila mwaka kula sikukuu ya Pasaka.[#2 Mose 23:14-17.]

42Naye alipopata miaka 12, wakakwea naye, kama walivyozoea kwenye hiyo sikukuu.

43Zile siku zilipomalizika, wakarudi, lakini mtoto wao Yesu akasalia Yerusalemu, wazazi wake wasijue.[#2 Mose 12:18.]

44Wakadhani, yumo katika wenzake wa njiani. Wakaenda mwendo wa siku moja, kisha wakamtafuta kwa ndugu zao na kwa wenzi wao.

45Wasipomwona wakarudi Yerusalemu wakimtafuta.

46Siku tatu zilipopita, wakamwona Patakatifu, amekaa katikati ya wafunzi akiwasikiliza na kuulizana nao,

47nao wote waliomsikia wakaustukia sana ujuzi wake wa kujibu.

48Walipomwona wakashangaa, mama yake akamwmbia: Mwanangu, mbona umetufanyia hivyo? Tazama, baba yako na mimi tumekutafuta kwa uchungu.

49Akawaambia: Mwanitafutiani? Hamkujua, ya kuwa imenipasa kuwa mwake Baba yangu?[#Yoh. 2:16.]

50Wao hawakulijua maana neno hili, alilowaambia.

51Kisha akatelemka pamoja nao, akafika Nasareti, akakaa na kuwatii. Naye mama yake akayashika maneno hayo yote moyoni mwake.[#Luk. 2:19.]

52Yesu akakua na kuongezeka werevu wa kweli, mpaka akiwa mtu mzima, tena akawa akimpendeza Mungu na watu.*[#1 Sam. 2:26; Fano. 3:4.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania