The chat will start when you send the first message.
1Akawa akipita katika mashamba siku ya mapumziko; l nao wanafunzi wake wakakonyoa masuke, wakayafikicha kwa mikono, wakala.
2Lakini walikuwako Mafariseo waliosema: Mbona mnafanya yaliyo mwiko siku ya mapumziko?
3Yesu akawajibu akisema: Hamkuvisoma hata hivyo, Dawidi alivyovifanya, walipoona njaa yeye nao wenziwe waliokuwa pamoja naye?[#1 Sam. 21:6.]
4Hapo aliingia Nyumbani mwa Mungu, akaitwaa mikate aliyowekewa Bwana, akaila, akawapa nao wenziwe. Nayo kuila ni mwiko, huliwa na watambikaji peke yao.[#3 Mose 24:9.]
5Akawaambia: Mwana wa mtu ni bwana wa siku ya mapumziko.
6Ikawa siku nyingine ya mapumziko, akaingia nyumbani mwa kuombea, akafundisha. Mle mlikuwa na mtu, ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umekaukiana.[#Luk. 13:10-17.]
7Waandishi na Mafariseo wakamtunduia, kama atamponya siku ya mapumziko, waone neno la kumsuta.[#Luk. 14:1-6.]
8Naye akayajua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliokaukiana: Inuka, usimame hapa katikati! Akainuka, akasimama hapo.
9Kisha Yesu akawaambia: Nawauliza ninyi: Iko ruhusa siku ya mapumziko kufanya mema au kufanya maovu? kuponya roho ya mtu au kuiangamiza?
10Akawatazama wote waliokuwako, akamwambia: Unyoshe mkono wako! Alipovifanya, huo mkono wake ukageuka kuwa mzima.
11Wale wakawa kama wenye wazimu, wasijue kitu, wakasemezana wao kwa wao, watakayomtendea Yesu.
12Ikawa siku zile, akatoka kwenda mlimani kuomba; akakesha kucha katika kumwomba Mungu.
13Kulipokucha, akawaita wanafunzi wake, akachagua miongoni mwao kumi na wawili; ndio aliowapa jina la Mitume.[#Mat. 10:2-4; Tume. 1:13.]
14Ni Simoni, aliyempa jina la Petero, na Anderea nduguye, na Yakobo na Yohana na Filipo na Bartolomeo
15na Mateo na Toma na Yakobo wa Alfeo na Simoni aliyeitwa Zelote
16na Yuda wa Yakobo na Yuda Iskariota, ndiye aliyekuwa mchongezi.
(17-19: Mat. 4:23-5:1; Mar. 3:7-12.)17Akashuka pamoja nao, akasimama mahali penye uwanda; hapo palikuwa na kundi zima la wanafunzi wake wengi na watu wengine wengi sana waliotoka Yudea po pote na Yerusalemu na pwani pa Tiro na Sidoni;
18ndio waliokuja, wamsikilize yeye, waponywe magonjwa yao. Nao waliosumbuliwa na pepo wachafu wakaponywa.
19Wale watu wote wakatafuta kumgusa tu, kwani nguvu zilizotoka kwake ziliwaponya wote.
20Kisha akainua macho, akawatazama wanafunzi wake, akasema: Wenye shangwe ni ninyi mlio maskini, maana ufalme wa Mungu ni wenu.[#Yak. 2:5.]
21Wenye shangwe ni ninyi mnaoona njaa sasa, maana mtashibishwa.[#Sh. 126:5-6; Yes. 61:3; Ufu. 7:16-17.]
22Wenye shangwe ni ninyi, watu watakapowachukia na kuwatenga kwao na kuwatukana na kuyakataa majina yenu kwa kuwa mabaya kwa ajili ya Mwana wa mtu.[#Yoh. 15:18.]
23Furahini siku ile na kurukaruka! Kwani tazameni, mshahara wenu ni mwingi mbinguni! Kwani hivyo ndivyo, baba zao walivyowafanyia wafumbuaji.
24Lakini yatawapata ninyi wenye mali, kwani mmekwisha upata utulivu wenu.[#Mat. 19:23; Yak. 5:1.]
25Yatawapata nanyi mnaoshiba sasa, kwani mtaona njaa. Yatawapata ninyi mnaocheka sasa, kwani mtasikitika na kulia.[#Yes. 5:22.]
26Yatawapata ninyi, watu wote wanapowaendea kwa maneno mazuri, kwani hivyo ndivyo, baba zao walivyowafanyia wafumbuaji wa uwongo.[#Mika 2:11; Yak. 4:4.]
27Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu! Wafanyieni mazuri wanaowachukia![#1 Kor. 4:12.]
28Wabarikini wanaowaapiza! Waombeeni wanaowabeza!
29Mtu akikupiga kofi shavu moja, umgeuzie la pili, alipige nalo! Mtu anayekunyang'anya kanzu yako, usimkataze kuichukua hata shuka!
30Kila anayekuomba umpe, naye akunyang'anyaye mali zako, usizitake tena kwake!
31Kama mnavyotaka, watu wawafanyie ninyi, nanyi mwafanyie vivyo hivyo![#Mat. 7:12.]
32Maana mkiwapenda wanaowapendani mnawagawia nini? Kwani nao wakosaji huwapenda wawapendao.
33Nanyi mnapowafanyia mema wanaowafanyia mema ninyi mnawagawia nini? Nao wakosaji hufanya hivyo hivyo.
34Nanyi mnapokopesha watu, mnaowangojea kurudishiwa nao, mnawagawia nini? Nao wakosaji huwakopesha wakosaji wenzao, warudishiwe yaleyale.[#3 Mose 25:35-36.]
35Lakini wapendeni wachukivu wenu! Wafanyieni mema na kuwakopesha, msiowangojea kurudishiwa cho chote! Hivyo mshahara wenu utakuwa mwingi, nanyi mtakuwa wana wake Alioko huko juu. Kwani yeye huwagawia nao wenye majivuno nao wenye ubaya.
36*Mgeuke kuwa wenye huruma, kama Baba yenu alivyo mwenye huruma!
(37-49: Mat. 7:1-5,16-27.)37Msiumbue watu, nanyi msije mkaumbuliwa! Msionee watu, nanyi msije mkaonewa! Wafungueni watu, nanyi mje mkafunguliwa![#Mat. 6:14.]
38Wapeni watu, nanyi mje mkapewa! Kipimo kizuri kilichoshindiliwa na kutingishwa na kumwagika mtapewa, mfutikie katika nguo zenu. Kwani kipimo, mnachokipimia wengine, ndicho, mtakachopimiwa nanyi tena.[#Mar. 4:24.]
39Akawaambia mfano: Je? Kipofu aweza kumwongoza kipofu mwenziwe? Hawatatumbukia wote wawili shimoni?[#Mat. 15:14.]
40Mwanafunzi hampiti mfunzi wake, lakini kila aliyekwisha fundishwa atakuwa, kama mfunzi wake alivyo.[#Mat. 10:24-25; Yoh. 15:20.]
41Nawe unakitazamiani kibanzi kilichomo jichoni mwa ndugu yako, lakini gogo lililomo jichoni mwako wewe mwenyewe hulioni?
42Unawezaje kumwambia ndugu yako: Ngoja, ndugu yangu, nikitoe kibanzi kilichomo jichoni mwako? Nalo gogo lililomo jichoni mwako mwenyewe hulioni? Mjanja, kwanza litoe gogo katika jicho lako! Kisha utazame vema, ndivyo upate kukitoa kibanzi kilichomo jichoni mwa ndugu yako!*
43Kwani hakuna mti mzuri unaozaa matunda maovu; tena hakuna mti mwovu unaozaa matunda mazuri.[#Mat. 7:17-18.]
44Kwani kila mti hutambulikana kwa matunda yake mwenyewe. Kwani hawachumi kuyu miibani, wala hawachumi zabibu katika mikunju.
45Mtu mwema hutoa mema katika kilimbiko chake chema cha moyo, lakini naye mbaya hutoa mabaya katika mabaya yake. Kwani moyo unayoyajaa ndiyo, kinywa cha mtu kinayoyasema.[#Mat. 12:34-35.]
46Tena mnaniitiani: Bwana! Bwana! msipoyafanya, ninayoyasema?[#Mal. 1:6.]
47Kila anayekuja kwangu na kuyasikia maneno yangu na kuyafanyiza, nitawaonyesha, anavyofanana navyo.
48Amefanana na mtu aliyejenga nyumba, akiichimbia chini vizuri na kuweka msingi mwambani. Maji yalipojaa yakatoka mto, ukapasua penye ile nyumba, lakini haukuweza kuitingisha, kwa kuwa ilikuwa imejengwa vizuri.
49Lakini anayeyasikia asipoyafanyiza amefanana na mtu aliyejenga nyumba mchangani pasipo msingi. Basi, mto ulipotokea na kupasua hapo, ilianguka papo hapo, kupasuka kwake ile nyumba kukawa kukubwa.