Luka 7

Luka 7

Mkubwa wa Kapernaumu.

(1-10: Mat. 8:5-13.)

1Alipokwisha kuyasema maneno yake yote, watu wakimsikiliza, akaenda, akaingia Kapernaumu.

2Kukawako mkubwa wa askari mwenye mtumwa, ambaye alipendezwa sana naye; huyu alikuwa mgonjwa wa kufa.

3Bwana wake aliposikia mambo ya Yesu akatuma kwake wazee wa Wayuda, wamwombe, aje, amponye mtumwa wake.

4Walipomfikia Yesu wakakaza kumbembeleza wakisema: Amepaswa, umfanyie hivyo;

5kwani anatupenda sisi taifa letu, hata nyumba ya kuombea ametujengea mwenyewe.

6Yesu akaenda pamoja nao; alipokuwa mbali kidogo kuifikia ile nyumba, yule mkubwa wa askari akatuma rafiki zake kumwambia: Bwana, usijisumbue! Kwani hainipasi, uingie kijumbani mwangu.

7Kwa hiyo nami sikujipa moyo wa kukujia mwenyewe. Ila sema neno tu! ndipo, mtoto wangu atakapopona!

8Kwani nami ni mtu mwenye kuitii serikali, ninao askari chini yangu. Nami nikimwambia huyu: Nenda! basi, huenda; na mwingine: Njoo! huja; nikimwagiza mtumishi wangu: Vifanye hivi! huvifanya.

9Yesu alipoyasikia hayo akamstaajabu, akaligeukia kundi la watu lililomfuata, akasema: Nawaambiani, hata kwa Waisiraeli sijaona bado mwenye kunitegemea kama huyu.

10Wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa, yuko amepona.

Kijana wa Naini.

11*Kisha punde kidogo akashika njia kwenda katika mji, jina lake Naini. Wakafuatana naye wanafunzi wake na kundi la watu wengi.

12Alipolikaribia lango la mji, panatolewa mfu; huyu alikuwa mwana wa pekee wa mama yake, naye alikuwa mjane. Kwa hiyo watu wengi wa mji ule walikwenda pamoja naye.[#1 Fal. 17:17.]

13Bwana alipomwona akamwonea uchungu, akamwambia: Usilie!

14Alipofika karibu, alishike jeneza, wachukuzi wakasimama. Akasema: Kijana, nakuambia: Inuka!

15Ndipo, yule mfu alipoinuka, akaanza kusema; kisha akampa mama yake.[#1 Fal. 17:23; 2 Fal. 4:36.]

16Woga ukawashika wote, wakamtukuza Mungu wakisema: Mfumbuaji mkuu ametutokea, naye Mungu amewakagua wao wa ukoo wake.[#Luk. 1:68.]

17Hili neno lake, alilolifanya, likaja kuenea Uyuda wote na nchi zote zilizoko pembenipembeni.*

Wajumbe wa Yohana.

(18-35: Mat. 11:2-19.)

18Wanafunzi wake walipomsimulia Yohana hayo yote, akaita wanafunzi wake wawili,

19akawatuma kwa Bwana, wamwulize: Wewe ndiwe mwenye kuja, au tungoje mwingine?

20Waume hao walipofika kwake wakasema: Yohana Mbatizaji ametutuma kwako, tuulize: Wewe ndiwe mwenye kuja, au tungoje mwingine?

21Saa ileile alikuwa akiponya wengi wenye magonjwa na maumivu na pepo wabaya; nao vipofu wengi akawapa kuona.

22Akajibu akiwaambia: Rudini, mmsimulie Yohana, mliyoyaona nayo mliyoyasikia: vipofu wanaona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanapigiwa mbiu njema.

23Tena mwenye shangwe ndiye asiyejikwaa kwangu.

Ufumbuaji wa Yohana.

24Wajumbe wa Yohana walipokwisha kwenda zao, akaanza kusema na yale makundi ya watu mambo ya Yohana: Mlipotoka kwenda nyikani mlikwenda kutazama nini? Mlikwenda kutazama utete unaotikiswa na upepo?

25Au mlitoka kutazama nini? Mlikwenda kutazama mtu aliyevaa mavazi mororo? Tazameni, wanaovaa mavazi yenye utukufu na kula vya mali wamo nyumbani mwa wafalme.

26Au mlitoka kutazama nini? Mlitaka kuona mfumbuaji? Kweli, nawaambiani: Ni mkuu kuliko mfumbuaji.[#Luk. 1:76.]

27Huyo ndiye aliyeandikiwa:

Utaniona, nikimtuma mjumbe wangu,

akutangulie, aitengeneze njia yako mbele yako.

28Nawaambiani: Miongoni mwao wote waliozaliwa na wanawake hakuna mkuu kuliko Yohana. Lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye.

29Watu wote waliomsikia, hata watoza kodi wakauitikia wongofu wake Mungu, wakabatizwa ubatizo wa Yohana.[#Luk. 3:7,12; Mat. 21:32.]

30Lakini Mafariseo na wajuzi wa Maonyo waliyatengua, Mungu aliyoyataka, wayafanye, wasibatizwe naye.[#Tume. 13:46.]

31Basi, wao wa kizazi hiki niwafananishe na nini? Au wamefanana na mtu gani?

32Wamefanana na watoto wanaokaa sokoni na kuitana wao kwa wao wakisema: Tumewapigia filimbi, nanyi hamkucheza; tena tumewaombolezea, nanyi hamkulia.

33Kwani Yohana Mbatizaji alikuja, hakula mkate, wala hakunywa mvinyo, nanyi mkasema: Ana pepo.

34Mwana wa mtu amekuja, akala, akanywa, nanyi mkasema: Tazameni mtu huyu mlaji na mnywaji wa mvinyo, mpenda watoza kodi na wakosaji![#Luk. 15:2.]

35Lakini werevu hutokezwa na watoto wake wote kuwa wa kweli.

Mwanamke mkosaji.

36*Fariseo mmoja alipomwalika, ale pamoja naye, akaingia nyumbani mwa yule Fariseo, akakaa chakulani.[#Luk. 11:37.]

37Mjini mle mlikuwa na mwanamke mkosaji. Naye alipotambua, ya kuwa yumo mwa yule Fariseo, amekaa chakulani, akaja na kichupa cha manukato,

38akamsimamia nyuma miguuni pake mwenye machozi, akaanza kuyadondosha miguuni pake, akayasugua kwa nywele za kichwani pake, akainonea miguu yake, kisha akaipaka manukato.[#Mat. 26:7-13; Yoh. 12:3-8.]

39Yule Fariseo aliyemwalika alipoviona akasema moyoni mwake: Huyu kama angekuwa mfumbuaji, angemtambua mwanamke huyu anayemgusa, kama ni nani, kama ni wa namna gani, kwamba ni mkosaji.

40Yesu akajibu akimwambia: Simoni, ninalo la kukuambia. Naye alipomwambia: Mfunzi, sema! akasema:

41Mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili. Wa kwanza deni lake ni shilingi 500, mwenzake 50.

42Walipokosa vya kulipa, akawaachilia wote wawili, wasilipe. Katika hao atakayempenda kumpita mwenziwe ni yupi?

43Simoni akajibu akisema: Nadhani, ni yule aliyeachiliwa nyingi. Naye akamwambia: Ulivyolikata shauri hili, ndivyo kweli.

44Kisha akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni: Unamtazama mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu; lakini huyu alinidondoshea machozi miguuni pangu, akayasugua kwa nywele za kichwani pake.[#1 Mose 18:4.]

45Hukuninonea, lakini huyu, tangu nilipoingia, hakuacha kuinonea miguu yangu.[#Rom. 16:16.]

46Wewe hukunipaka mafuta kichwani, lakini huyu ameipaka miguu yangu manukato.

47Kwa hiyo nakuambia: Ameondolewa makosa yake yaliyo mengi, kwani mapendo yake ni mengi. Lakini anayeondolewa machache tu, naye mapendo yake ni machache.

48Kisha akamwambia yule mwanamke: Wewe umeondolewa makosa yako.[#Luk. 5:20-21.]

49Ndipo, wale waliokaa chakulani pamoja naye walipoanza kusema mioyoni mwao: Huyu ni nani akiondoa hata makosa?

50Naye akamwambia yule mwanamke: Kunitegemea kwako kumekuokoa; nenda na kutengemana!*[#Luk. 8:48; 17:19; 18:42.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania