Luka 9

Luka 9

Kuwatuma mitume.

(1-6: Mat. 10:1,7,9-11,14; Mar. 6:7-13.)

1Akawaita wale kumi na wawili, wakusanyike, akawapa uwezo na nguvu za kufukuza pepo wote na za kuponya magonjwa.

2Akawatuma, wautangaze ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa.

3Akawaambia: Msichukue kitu cha njiani, wala fimbo wala mkoba wala chakula wala shilingi, tena mtu asiwe na nguo mbili!

4Nyumbani mo mote mtakamoingia, kaeni humo! Namo ndimo, mtakamotoka tena![#Luk. 10:5-7.]

5Nao wote wasiowapokea, basi, utokeni mji wao na kuyakung'uta mavumbi yaliyoishika miguu yenu, yaje yanishuhudie kwao![#Luk. 10:11.]

6Wakatoka, wakapita vijijini wakiipiga hiyo mbiu njema na kuponya wagonjwa po pote.

Herode amtafuta Yesu.

(7-9: Mat. 14:1-2; Mar. 6:14-16.)

7Mfalme Herode alipoyasikia mambo yote yaliyokuwapo, akahangaika, maana wengine walisema: Yohana amefufuka katika wafu,

8wengine: Elia ametokea, wengine: Mmoja wao wafumbuaji wa kale amefufuka.

9Lakini Herode akasema: Yohana mimi nimemkata kichwa. Lakini huyo ni nani, ninayemsikia mambo kama hayo? Akatafuta kumwona.

Kulisha watu 5000.

(10-17: Mat. 14:13-21; Mar. 6:30-44; Yoh. 6:1-13.)

10Mitume waliporudi, wakamsimulia mambo yote, waliyoyafanya. Kisha akawachukua, akaondoka kwenda nao peke yao, wakaingia mji, jina lake Beti-Saida.

11Makundi ya watu walipovitambua wakamfuata, naye akawapokea, akasema nao mambo ya ufalme wa Mungu, akawaponya waliopaswa na kuponywa.

12Jua lilipotaka kuchwa, wale kumi na wawili wakamjia, wakamwambia: Uliage kundi la watu, waende zao vijijini na mashambani huko pembenipembeni, waone ulalo na vyakula, kwani hapa tulipo ni nyika.

13Akawaambia: Wapeni ninyi vyakula! Wakasema: Sisi hatuna kitu hapa kuliko mikate mitano na visamaki viwili; au twende sisi kuwanunulia watu hawa wote vyakula?

14Kwani waume tu waliokuwako walipata 5000. Akawaambia wanafunzi wake: Mwaagize, wakae mafungumafungu kama hamsinihamsini!

15Wakafanya hivyo, wakawakalisha wote.

16Akaitwaa ile mikate mitano na vile visamaki viwili, akatazama juu mbinguni, akaviombea, akawamegeamegea, akawapa wanafuanzi, wawapangie hao watu wengi.

17Wakala, wakashiba wote, pakaokotwa makombo yaliyowasalia vikapu kumi na viwili.

Kuungama kwa Petero.

(18-27: Mat. 16:13-28; Mar. 8:27-9:1.)

18*Ikawa, alipokuwa akiomba peke yake, wakawapo pamoja naye wanafunzi wake, akawauliza akisema: Makundi ya watu hunisema kuwa ni nani?

19Nao wakajibu wakisema: Wanakusema kuwa u Yohana Mbatizaji, wengine: Elia, wengine husema: Amefufuka mmoja wao wafumbuaji wa kale.

20Kisha akawauliza: Lakini ninyi mnanisema kuwa ni nani? Petero akajibu akisema: Kristo wa Mungu.

21Ndipo, alipowatisha na kuwakataza, wasimwambie mtu neno hilo.

Ufunuo wa Mateso.

22Akawaambia: Imempasa Mwana wa mtu kutwa mengi na kukataliwa nao wazee na watambikaji wakuu na waandishi, mpaka auawe, kisha afufuliwe siku ya tatu.[#Luk. 9:44; 18:32-33.]

Kujiokoa.

23Akawaambia wote: Mtu akitaka kunifuata mimi ajikataze mapenzi yake, ajitwishe kila siku nao msalaba wake, kisha anifuate![#Luk. 14:26-27.]

24Maana mtu anayetaka kuiokoa roho yake ataiangamiza. Lakini mtu atakayeiangamiza roho yake kwa ajili yangu mimi, huyo ataiokoa.[#Luk. 17:33; Mat. 10:39; Yoh. 12:25.]

25Kwani mtu vinamfaa nini, avichume vya ulimwengu wote, akijiangamiza mwenyewe, au akiponzwa navyo?

26Kwani mtu atakayenionea soni mimi na maneno yangu, basi, naye Mwana wa mtu atamwonea soni huyo atakapokuja mwenye utukufu wake yeye na wa Baba yake na wa malaika watakatifu.*[#Mat. 10:33.]

27Lakini nawaambiani lililo kweli: Miongoni mwao wanaosimama hapa wamo wengine, ambao hawatakuonja kufa, mpaka watakapouona ufalme wa Mungu.

Yesu anageuzwa sura.

(28-36: Mat. 17:1-9; Mar. 9:1-9.)

28Ikawa, walipokwisha kuyasema hayo, zikipita kama siku nane, akamchukua Petero na Yohana na Yakobo, wakapanda mlimani kuomba

29Alipokuwa akiomba, sura ya uso wake ikawa nyingine, nazo nguo zake zikawa nyeupe na kumerimeta.

30Walipotazama, wakawako waume wawili wakiongea naye, nao walikuwa Mose na Elia.

31Wakawatokea wenye utukufu, wakasema naye, ndivyo aende kuyatimiza mambo ya kufa kwake kule Yerusalemu.[#Luk. 9:22.]

32Lakini Petero na wenziwe walikuwa wamelemewa na usingizi. Walipoamka wakauona utukufu wake na wale waume wawili waliosimama naye.

33Ikawa, walipotengwa naye, Petero akamwambia Yesu: Bwana, hapa ni pazuri kuwapo sisi, na tujenge vibanda vitatu, kimoja chako, na kimoja cha Mose, na kimoja cha Elia! kwani hakujua, alilolisema.

34Angali akiyasema haya, pakawa na wingu, likawatia kivuli, wakashikwa na woga walipoingiwa na wingu lile.

35Sauti ikatoka winguni, ikasema: Huyu ndiye mwanangu, niliyemchagua, msikilizeni yeye![#Luk. 3:22.]

36Sauti hiyo iliposikilika, Yesu akaonekana, yuko peke yake. Siku zile wakanyamaza, wasimsimulie mtu hata moja lao hayo waliyoyaona.

Kijana mwenye pepo.

(37-45: Mat. 17:14-23; Mar. 9:14-32.)

37Ikawa siku ya kesho, waliposhuka mlimani wakakutana na kundi la watu wengi.

38Mle kundini mkawamo mwanamume, akapaza sauti akisema: Mfunzi, nakuomba, umtazame huyu mwanangu, kwani ni wangu wa pekee!

39Tazama, pepo humpagaa, naye mara moja hulia kwa kukumbwa, mpaka akitoka pofu; akiisha kumlegeza hukawia kumwondokea.

40Nikawaomba wanafunzi wako, wamfukuze, lakini hawakuweza.

41Yesu akajibu akisema: Enyi wa kizazi kisichomtegemea Mungu kwa kupotoka! Nitakuwapo nanyi na kuwavumilia mpaka lini? Umlete mwana wako, aje hapa!

42Alipokuwa akija, pepo akamkamata kwa nguvu, akamkumba. Lakini Yesu akamkaripia huyo pepo mchafu, akamponya mtoto, akamrudishia baba yake.[#Luk. 7:15.]

43Ndipo, wote walipoingiwa na kituko kwa ajili ya ukubwa wa nguvu yake Mungu.

Ufunuo wa pili wa mateso.

Wao wote walipoyastaajabu yote, aliyoyafanyiza, akawaambia wanafunzi wake:

44Myaweke vema maneno haya masikioni mwenu! Maana Mwana wa mtu atatiwa mikononi mwa watu.[#Luk. 9:22.]

45Lakini hawakulitambua neno hili, likawa limefichiwa wao, wasilione maana. Nao wakaogopa kumwuliza tena neno hilo.[#Luk. 18:34.]

Mkubwa ni nani?

(46-50: Mat. 18:1-5; Mar. 9:33-40.)

46Wakawa wakiwaza mioyoni mwao kwamba: Aliye mkuu kwetu ni nani?

47Lakini Yesu akayajua, waliyoyawaza mioyoni mwao, akatwaa kitoto, akamsimamisha kando yake,

48akawaambia: Mtu atakayempokea kitoto huyu kwa Jina langu hunipokea mimi. Tena akinipokea mimi humpokea yule aliyenituma mimi. Kwani aliye mdogo kwenu ninyi wote, huyo ndiye mkuu.[#Mat. 10:40.]

49Yohana akajibu akisema: Bwana, tuliona mtu anayefukuza pepo kwa Jina lako; tukamzuia, kwani hafuatani nasi.

50Yesu akamwambia: Msimzuie! Kwani asiyewakataa yuko upande wenu.[#Luk. 11:23; Mat. 12:30; Fil. 1:18.]

Wasamaria wanamkataa Yesu.

51*Ikawa, zilipotimia siku zake za kuchukuliwa mbinguni, mwenyewe akauelekeza uso kwenda Yerusalemu,

52akatanguliza wajumbe mbele yake. Hao walipokwenda, kuingia kijiji cha Wasamaria, wamtengenezee mahali,

53hawakumpokea, kwani uso wake ulikuwa umeelekea kwenda Yerusalemu.

54Wanafunzi akina Yakobo na Yohana walipoviona wakasema: Bwana, wataka, tuseme, moto ushuke toka mbinguni, uwamalize, kama Elia naye alivyofanya?

55Lakini akapinduka, akawatisha akiwaambia: Hamjui, kama m wenye Roho gani?

56Mwana wa mtu hakujia kuangamiza roho za watu, ila kuziokoa. Kisha wakaenda zao, wakafikia kijiji kingine.*

Kumfuata Yesu.

(57-60: Mat. 8,19-22.)

57Walipokuwa wakienda njiani, palikuwapo aliyemwambia: Nitakufuata po pote, utakapokwenda.

58Yesu akamwambia: Mbweha wanayo mapango, nao ndege wa angani wanavyo vituo, lakini Mwana wa mtu hana pa kukilazia kichwa chake.

59Alipomwambia mtu mwingine akasema: Nifuate! huyo akasema: Nipe ruhusa, kwanza niende nimzike baba yangu!

60Naye akamwambia: Waache wafu, wazike wao kwa wao! Lakini wewe nenda, uutangaze ufalme wa Mungu!

61Mtu mwingine akasema: Nitakufuata, Bwana, lakini kwanza nipe ruhusa, niwaage waliomo nyumbani mwangu!

62Yesu akamwambia: Mtu ashikaye jembe mkononi na kuvitazama vya nyumba, huyo hatauweza ufalme wa Mungu.*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania