Mateo 10

Mateo 10

Kuwatuma mitume.

(1-15: Mar. 6:7-13; Luk. 9:1-15.)

1Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa nguvu za kufukuza pepo wachafu na za kuponya wagonjwa wo wote na wanyonge wo wote.

Majina yao.

2Majina yao wale mitume kumi na wawili ndiyo haya: Wa kwanza Simoni anayeitwa Petero na Anderea nduguye, Yakobo wa Zebedeo na Yohana nduguye,[#Mar. 3:14-19; Luk. 6:13-16; Yoh. 1:40-49.]

3Filipo na Bartolomeo, Toma na Mateo, mtoza kodi, Yakobo wa Alfeo na Tadeo,

4Simoni wa Kana na Yuda Iskariota aliye mchongea halafu.

Maagizo ya mitume.

5Hao kumi na wawili Yesu aliwatuma na kuwaagiza akisema: Msiende katika njia za wamizimu, wala mji wowote wa Wasamaria msiuingie![#Mat. 15:24; Tume. 13:46.]

6Lakini mwende kwa kondoo waliopotea wa mlango wa Isiraeli!

7Tena mnapokwenda pigeni mbiu mkisema: Ufalme wa mbingu umekaribia![#Mat. 4:17; Luk. 10:9.]

8Walio wagonjwa waponyeni, waliokufa wafufueni, wenye ukoma watakaseni, nazo pepo zifukuzeni! Bure mmeyapata, tena yatoeni bure![#Tume. 20:33.]

9Msichukue mishipini mwenu dhahabu wala shilingi wala senti!

10Msichukue mkoba wa njiani wala nguo mbili wala viatu wala fimbo! Kwani mtenda kazi hupaswa na kupewa chakula chake.[#4 Mose 18:31; Luk. 10:4; 1 Kor. 9:7-11; 1 Tim. 5:18.]

11Lakini mji au kijiji mtakamoingia ulizeni, kama yumo mtu anayepaswa na kuwapokea! Kaeni mwake, mpaka mtakapotoka tena!

12Tena mkiingia nyumbani wapeni salamu![#Luk. 10:5-6.]

13Ikiwa wamepaswa nao, utengemano wenu utakaa humo. Lakini ikiwa hawakupaswa nao, utengemano wenu utawarudia ninyi.

14Tena mtu asipowapokea wala asipoyasikia maneno yenu, basi, kama ni nyumba au mji, mtokeni na kuyakung'uta mavumbi ya miguuni penu![#Luk. 10:10-12; Tume. 13:51; 18:6.]

15Kweli nawaambiani: Siku ya hukumu nchi ya Sodomu na Gomora itapata mepesi kuliko mji ule.[#Mat. 11:24; Luk. 20:47.]

Kusumbuliwa

(16-22: Mar. 13:9-13; Luk. 21:12-17.)

16Tazameni, mimi nawatuma, mwe kama kondoo walio katikati ya mbwa wa mwitu. Kwa hiyo mwe wenye mizungu kama nyoka, tena mwe wakweli, kama njiwa walivyo! Jilindeni kwa ajili ya watu![#Luk. 10:3; Rom. 16:19; Ef. 5:15.]

17Kwani watawapeleka barazani kwao wakuu na kuwapiga katika nyumba zao za kuombea.[#Mat. 24:9; Tume. 5:40.]

18Kwa ajili yangu watawavuta kwa mabwana wakubwa na kwa wafalme, mje mnishuhudie kwao na kwa wamizimu.[#Mat. 24:14; Tume. 25:23; 27:24.]

19Lakini hapo watakapowatoa, msihangaikie wala mizungu wala maneno ya kuwajibu! Kwani saa ileile mtapewa maneno, mtakayoyasema.[#Luk. 12:11-12; Tume. 4:8.]

20Kwani si ninyi mnaosema, ila ni Roho wa Baba yenu; ndiye anayesema vinywani mwenu.[#1 Kor. 2:4.]

21Ndugu na ndugu watatoana, wauawe, hata baba watawatoa watoto wao, hata watoto watawainukia wazazi wao, wawaue.[#Mat. 10:35; Mika 7:6.]

22Nanyi mtakuwa mmechukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka.[#Mat. 24:9-13.]

23Lakini watakapowafukuza mjini humu kimbilieni mwingine! Kwani nawaambiani iliyo kweli: Hamtaimaliza miji ya Isiraeli, mpaka Mwana wa mtu atakapokuja.[#Mat. 16:28.]

Mategemeo.

24*Mwanafunzi hampiti Mfunzi wake, wala mtumwa hampiti bwana wake.[#Luk. 6:40; Yoh. 13:16; 15:20.]

25Inamtosha mwanafunzi kuwa, kama mfunzi wake alivyo, vilevile mtumwa inamtosha kuwa, kama bwana wake alivyo. Kama Mwenye nyumba walimwita Belzebuli (Mkuu wa pepo), hawatazidi kuwaita hivyo waliomo nyumbani mwake?[#Mat. 12:24.]

(26-33: Luk. 12:2-9.)

26Msiwaogope! Kwani hakuna lililofunikwa lisilofunuliwa halafu, wala hakuna lililofichwa lisilotambulikana halafu.[#Mar. 4:22; Luk. 8:17.]

27Ninalowaambia gizani lisemeni mwangani! Tena ninalowanong'oneza masikioni, litangazeni barazani!

28Tena msiwaogope wanaoweza kuiua miili tu, wasiweze kuziua nazo roho! Lakini mfulize kumwogopa anayeweza kuziangamiza roho pamoja na miili shimoni mwa moto![#Yak. 4:12.]

29Je? Videge viwili haviuzwi kwa senti moja? Lakini hata mmoja wao haanguki chini, Baba yenu asipojua.

30Lakini kwenu ninyi hata nywele za vichwani zimehesabiwa zote.[#Tume. 27:34.]

31Kwa hiyo msiogope ninyi mnapita videge vingi![#Ufu. 3:5.]

32Kila atakayeungama mbele ya watu, kwamba ni mtu wangu, nami nitaungama mbele ya Baba yangu wa mbinguni, kwamba ni mtu wangu.

33Lakini atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu wa mbinguni.*[#Luk. 9:26.]

Magombano na Malipizano.

(34-36: Luk. 12:51-53.)

34Msidhani, ya kuwa nimejia kuiletea nchi utengemano! Sikujia kuleta utengemano, ila upanga.

35Kwani nimejia kutenga watu, wagombane mtu na baba yake, mwana wa kike na mama yake, vilevile mkwe na mkwewe,[#Mika 7:6.]

36nao watakaomchukia mtu ndio waliomo mwake.[#5 Mose 33:9; Luk. 14:26-27.]

37Anayempenda baba yake au mama yake kuliko mimi hanipasi; anayempenda mwanawe wa kiume au wa kike kuliko mimi hanipasi.

38Tena asiyejitwisha msalaba wake na kunifuata nyuma yangu hanipasi.[#Mat. 16:24-25.]

39Mwenye kuiponya roho yake ataiangamiza; mwenye kuiangamiza roho yake kwa ajili yangu ataiponya.[#Luk. 17:33; Yoh. 12:25.]

40Anayewapokea ninyi hunipokea mimi; naye anayenipokea mimi humpokea aliyenituma.[#Mat. 18:5; Luk. 10:16; Yoh. 13:20.]

41Anayepokea mfumbuaji, kwa kuwa ni mfumbuaji, atapata mshahara kama wa mfumbuaji; naye anayepokea mwongofu, kwa kuwa ni mwongofu, atapata mshahara kama wa mwongofu.[#1 Fal. 17.]

42Tena mtu akinywesha mmoja wao walio wadogo kinyweo cha maji mazizima tu, kwa kuwa ni mwanafunzi, kweli nawaambiani: Mshahara wake hautampotea kamwe.[#Mat. 25:40; Mar. 9:41.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania