Mateo 13

Mateo 13

Mwenye kumiaga mbegu.

(1-23: Mar. 4:1-20.)

1Siku ile Yesu alitoka nyumbani, akaenda kukaa kandokando ya bahari.

2Wakamkutanyikia makundi mengi ya watu, kwa hiyo akaingia chomboni, akakaa humo, watu wote wakisimama pwani.

3Akawaambia maneno mengi kwa mifano akisema: Tazameni, mpanzi alitoka kumiaga mbegu.

4Ikawa alipozimiaga, nyingine zikaangukia njiani; ndege wakaja, wakazila.

5Nyingine zikaangukia penye miamba pasipo na udongo mwingi. Kuota zikaota upesi kwa kuwa na udongo kidogo;

6lakini jua lilipokuwa kali, zikanyauka, kwa kuwa hazina mizizi.

7Nyingine zikaangukia penye miiba; nayo miiba ilipoota ikazisonga.

8Lakini nyingine zikaangukia penye mchanga mzuri, zikazaa, nyingine punje mia, nyingine sitini, nyingine thelathini.

9Mwenye masikio yanayosikia na asikie!

Sababu ya kusema kwa mifano.

10Wanafunzi wake wakamjia, wakamwambia: Sababu gani unasema nao kwa mifano?

11Naye akajibu akisema: Ninyi mmepewa kuyatambua mafumbo ya ufalme wa mbingu,[#1 Kor. 2:10.]

12lakini wale hawakupewa. Kwani ye yote aliye na mali atapewa, ziwe nyingi zaidi; lakini asiye na kitu atachukuliwa hata kile, alicho nacho.[#Mat. 25:14-30; Mar. 4:25; Luk. 8:18.]

13Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano, kwamba wakitazama wasione, wakisikiliza wasisikie na kujua maana.[#5 Mose 29:4; Yoh. 16:25.]

14Hivyo ufumbuo wa Yesaya unatimizwa kwao unaosema:

Kusikia mtasikia, lakini hamtajua maana;

kutazama mtatazama, lakini hamtaona.

15Kwani mioyo yao walio ukoo huu imeshupazwa,

hata kwa masikio yao yaliyo mazito hawasikii;

nayo macho yao wameyasinziza,

wasije wakaona kwa macho,

au wakasikia kwa masikio,

au wakajua maana kwa mioyo,

wakanigeukia, nikawaponya.

16Lakini yenye shangwe ni macho yenu, kwani huona, nayo masikio yenu, kwani husikia.[#Mat. 16:16-17; Luk. 10:23-24.]

17Kweli nawaambiani: Wengi waliokuwa wafumbuaji na waongofu waliyatunukia, wayaone, mnayoyaona ninyi, lakini hawakuyaona; waliyatunukia wayasikie, mnayoyasikia ninyi, lakini hawakuyasikia.

18Basi, ninyi usikieni mfano wa mpanzi!

19Kila anayelisikia Neno la ufalme asipolijua maana, huja yule Mbaya na kulinyakua lililomiagwa moyoni mwake. Hizo ndizo zilizomiagwa njiani.

20Lakini zilizomiagwa penye miamba ni kama mtu anayelisikia Neno na kulipokea papo hapo kwa furaha.

21Lakini hana mizizi moyoni mwake, ila analishika kwa kitambo kidogo tu. Yanapotukia maumivu au mafukuzo kwa ajili ya Neno, mara hujikwaa.

22Lakini zilizomiagwa penye miiba ni kama mtu anayelisikia Neno, lakini masumbuko ya dunia hii na udanganyifu wa mali hulisonga Neno, lisizae matunda.[#Mat. 6:19-34; 1 Tim. 6:9-10.]

23Lakini zilizomiagwa penye mchanga mzuri ni kama mtu anayelisikia Neno na kulijua maana. Ndiye mwenye kuzaa, mwingine huleta punje mia, mwingine sitini, mwingine thelathini.

Nyasi katikati ya ngano.

24*Akawatolea mfano mwingine akisema: Ufalme wa mbingu umefanana na mtu aliyemiaga mbegu nzuri katika shamba lake.[#Mat. 13:36-43.]

25Lakini watu walipolala, akaja mchukivu wake, akamiaga mbegu za nyasi katikati ya ngano, akaenda zake.

26Halafu majani ya ngano yalipoota na kuchanua, zikaonekana nazo nyasi.

27Watumwa wa mwenye shamba wakaja wakamwuliza: Bwana, hukumiaga mbegu nzuri katika shamba lako? Basi, nyasi limezipata wapi?

28Alipowaambia: Mtu aliye mchukivu amevifanya hivyo, watumwa wakamwambia: Unataka, twende, tuzing'oe na kuzikusanya?

29Akasema: Hapana, msije, mkazing'oa nazo ngano mkiwa mnakusanya nyasi.

30Acheni, zikue zote mbili pamoja, mpaka mavuno yatakapokuwa! Siku za kuvuna nitawaambia wavunaji: Kusanyeni kwanza nyasi, mzifunge matitatita, mziteketeze! Lakini ngano zitieni chanjani kwangu!*[#Mat. 3:12; Ufu. 14:15.]

Kipunje cha haradali.

(31-32: Mar. 4:30-32; Luk. 13:18-19.)

31*Akawatolea mfano mwingine akisema: Ufalme wa mbingu umefanana na kipunje cha haradali, alichokitwaa mtu na kukipanda katika shamba lake.

32Nacho ni kidogo kuliko mbegu zote. Lakini kinapokua ni mkubwa kuliko miboga yote inayopandwa, huwa mti mzima, hata ndege wa angani huja na kutua katika matawi yake.

Chachu.

33Akawaambia mfano mwingine: Ufalme wa mbingu umefanana na chachu, mwanamke akiitwaa akaichanganya na pishi tatu za unga, mpaka ukachachwa wote.[#Luk. 13:20-21.]

34Haya yote aliwaambia makundi ya watu kwa mifano, pasipo mfano hakuwaambia neno,[#Mar. 4:33-34.]

35kusudi litimie lililosemwa na mfumbuaji, akisema:

Nitakifumbua kinywa changu, kiseme mifano.

Nitatangaza mambo yaliyofichika

tangu hapo, ulimwengu ulipoumbwa.*

36Kisha Yesu akawaaga makundi ya watu, akaingia nyumbani. Ndipo, wanafunzi wake walipomjia wakisema: Tuelezee mfano wa nyasi za shambani![#Mat. 13:24-30.]

37Akajibu akisema: Mwenye kumiaga mbegu nzuri ni Mwana wa mtu.

38Nalo shamba ndio ulimwengu. Nazo mbegu nzuri ndio wana wa ufalme. Lakini nyasi ndio wana wa yule Mbaya.[#1 Kor. 3:9.]

39Naye mchukivu aliyezimiaga ndiye Msengenyaji. Nayo mavuno ndio mwisho wa dunia. Nao wavunaji ndio malaika.

40Kama nyasi zinavyokusanywa na kuteketezwa motoni, ndivyo, itakavyokuwa katika mwisho wa dunia hii:

41Mwana wa mtu atawatuma malaika zake, nao watakusanya na kuyatoa katika ufalme wake makwazo yote nao waliofanya maovu,[#Mat. 7:23; 25:31-46; Sef. 1:3.]

42wawatupe shimoni mwa moto; ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno.[#Mat. 8:12.]

43Ndipo, waongofu watakapoangaza kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio yanayosikia na asikie![#Dan. 12:3.]

Fedha katika shamba.

44*Ufalme wa mbingu umefanana na fedha zilizofukiwa shambani. Mtu alipoziona akazifukia, akaenda kwa furaha yake, akaviuza vyote, alivyokuwa navyo, akalinunua shamba lile.[#Mat. 19:29; Luk. 14:33; Fil. 3:7.]

45Tena ufalme wa mbingu umefanana na mchuuzi aliyetafuta ushanga wa lulu nzuri.

46Naye alipoona lulu moja yenye bei kubwa akaenda, akaviuza vyote alivyokuwa navyo, akainunua.*[#Fano. 8:10-11; Fil. 3:7-8.]

Wavu wa kuvulia samaki.

47Tena ufalme wa mbingu umefanana na wavu uliotupwa baharini, ukakusanya samaki wa kila mtindo.[#Mat. 22:9-10.]

48Hata ulipojaa, wakauvuta pwani, wakakaa, wakawachagua samaki, walio wazuri wakawaweka vyomboni, lakini walio wabaya wakawatupa.

49Hivyo ndivyo, itakavyokuwa katika mwisho wa dunia hii: Malaika watatokea, watawatenga wabaya kati ya waongofu,[#Mat. 25:32.]

50wawatupe shimoni mwa moto. Ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno.

51Mmeijua maana ya hayo yote? Walipomwambia: Ndio,

52akawaambia: Kwa sababu hii kila mwandishi aliyefundishiwa ufalme wa mbingu amefanana na mtu mwenye nyumba anayetoa mawekoni mwake mambo mapya na ya kale.

Yesu mjini mwa Nasareti.

(53-58: Mar. 6:1-6; Luk. 4:15-30.)

53Ikawa, Yesu alipokwisha kuisema mifano hiyo akatoka, akaenda zake.

54Alipofika kwao, alikokulia, akawafundisha katika nyumba yao ya kuombea, nao wakashangaa wakisema: Huyu amepata wapi werevu huu ulio wa kweli na nguvu hizi?

55Huyu si mwana wa seremala? Mama yake si yeye anayeitwa Maria? Nao ndugu zake sio akina Yakobo na Yosefu na Simoni na Yuda?

56Nao maumbu zake hawako wote kwetu? Basi, huyu amepata wapi haya yote? Wakajikwaa kwake.[#Yoh. 7:15,52.]

57Yesu akawaambia: Mfumbuaji habezwi, isipokuwa kwao, alikokulia, namo nyumbani mwake.[#Yoh. 4:44.]

58Kwa hiyo hakufanya kule ya nguvu mengi, kwa sababu walikataa kumtegemea.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania