Mateo 16

Mateo 16

Kutaka kielekezo.

(1-12: Mar. 8:11-12.)

1Wakaja Mafariseo na Masadukeo, wakamjaribu wakitaka, awaonyeshe kielekezo kitokacho mbinguni.[#Mat. 12:38.]

2Naye akajibu akiwaambia: Kukichwa mnasema: Kutakucha na kianga, kwani mbingu ni nyekundu.[#Luk. 12:54-56.]

3Tena kukicha mnasema: Leo itakunya mvua, kwani mbingu ni nyekundu, tena kumetanda mawinguwingu. Enyi wajanja! Mnayoyaona ya mbinguni, mnajua kuyatambua, lakini vielekezo vya siku hizi vinawashindani?[#Mat. 11:4.]

4Wao wa ukoo huu mbaya wenye ugoni wanataka kielekezo, lakini hawatapata kielekezo, ila kielekezo cha mfumbuaji Yona. Kisha akawaacha, akaenda zake.*[#Mat. 12:39-40.]

Chachu ya Mafariseo.

5Wanafunzi walipofika ng'ambo walikuwa wamesahau kuchukua mikate.

6Yesu akawaambia: Tazameni, jilindeni kwa ajili ya chachu yao Mafariseo na Msadukeo![#Luk. 12:1.]

7Ndipo, walipoyafikiri na kusemeza wao kwa wao: Ni kwa sababu hatukuchukua mikate;

8Lakini Yesu akawatambua, akawaambia: Enyi mnaonitegemea kidogo tu, mbona mnafikiri hivyo mioyoni mwenu ya kuwa hamnayo mikate?[#Mat. 6:30.]

9Hamjaerevuka bado? Wala hamwikumbuki mikate ile mitano ya wale 5000 na makapu, mliyoyachukua, kama ni mangapi?[#Mat. 14:17-21.]

10Wala hamwikumbuki ile mikate saba ya wale 4000 na makanda, mliyoyachukua, kama ni mangapi?[#Mat. 15:34-38.]

11Kwa sababu gani hamtambui, ya kuwa sikuwaambia kwa ajili ya mikate niliposema: Jilindeni kwa ajili ya chachu yao Mafariseo na Masadukeo?

12Ndipo, walipotambua, ya kuwa hakusema, wajilinde kwa ajili ya chachu ya mikate, ila wajilinde kwa ajili ya ufundisho wao Mafariseo na Masadukeo.

Kuungama kwa Petero.

(13-20: Mar. 8:27-30; Luk. 9:18-21.)

13Yesu akaenda pande za mji wa Kesaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akisema: Watu humsema Mwana wa mtu kuwa ni nani?

14Nao wakajibu: Wengine husema kuwa u Yohana Mbatizaji, wengine: Elia, wengine: Yeremia au mmoja wao wafumbuaji.[#Mat. 14:2; 17:10; Luk. 7:16.]

15Yesu akawauliza: Lakini ninyi mnanisema kuwa ni nani?

16Simoni Petero akajibu akisema wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mungu Mwenye uzima.[#Yoh. 6:69.]

17Yesu akajibu akimwambia: U mwenye shangwe, Simoni wa Yona, kwani mwenye mwili na damu hakukufunulia hili, ila Baba yangu alioko mbinguni.[#Mat. 11:27; Gal. 1:15-16.]

18Nami nakuambia: Wewe ndiwe Petero, juu ya mwamba huu nitalijenga kundi la wateule wangu, nayo malango ya kuzimu hayatawashinda.[#Yoh. 1:42; Ef. 2:20.]

19Nitakupa funguo za ufalme wa mbingu: lo lote, utakalolifunga nchini, litakuwa limefungwa hata mbinguni; nalo lo lote, utakalolifungua nchini, litakuwa limefunguliwa hata mbinguni.[#Mat. 18:18.]

20Ndipo, alipowatisha wanafunzi, wasimwambie mtu ya kuwa yeye ndiye Kristo.[#Mat. 17:9.]

Ufunuo wa mateso.

(21-28: Mar. 8:31-9; 1 Luk. 9:22-27.)

21*Tokea hapo Yesu Kristo akaanza kuwaonyesha wanafunzi wake, ya kuwa imempasa kwenda Yerusalemu ateswe mengi nao wazee na watambikaji wakuu na waandishi, mpaka auawe, kisha afufuliwe siku ya tatu.[#Mat. 12:40; Yoh. 2:19.]

22Ndipo, Petero alipomchukua pembeni, akaanza kumtisha akisema: Jionee uchungu, wewe Bwana, haya yasikupate!

23Naye akageuka, akamwambia Petero: Niondokea hapa nyuma yangu, wewe Satani! Wewe wataka kunikwaza, kwani wewe huyawazi mambo ya Kimungu, ila unayawaza ya kiwatu tu.

Kujiokoa.

24Ndipo, Yesu alipowaambia wanafunzi wake: Mtu akitaka kunifuata mimi ajikataze mapenzi yake, ajitwishe nao msalaba wake, kisha anifuate![#Mat. 10:38-39; 1 Petr. 2:21.]

25Maana mtu anayetaka kuikoa roho yake ataiangamiza. Lakini mtu atakayeiangamiza roho yake kwa ajili yangu mimi ataiponya.

26Kwani mtu vitamfaa nini, hata avichume vya ulimwengu wote, roho yake ikiponwa navyo? Au mtu atatoa nini, aikomboe roho yake?*

27Kwani Mwana wa mtu atakapokuja mwenye utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, ndipo, atakapomlipa kila mtu, kama matendo yake yalivyo.[#Mat. 26:64; Rom. 2:6,16.]

28Kweli nawaambiani: Miongoni mwao wanaosimama hapa wamo wengine, ambao hawatakuonja kufa, mpaka watakapomwona Mwana wa mtu, akija mwenye ufalme wake.[#Mat. 10:23.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania