Mateo 19

Mateo 19

Cheti cha kuachana.

(1-9: Mar. 10:1-12.)

1Ikawa, Yesu alipoyamaliza maneno hayo, akaondoka Galilea, akaja mipakani kwa Yudea ng'ambo ya Yordani.

2Wakamfuata makundi mengi ya watu akawaponya huko.

3Nao Mafariseo wakamjia, wakamjaribu wakimwuliza: Iko ruhusa, mtu amwache mkewe kwa sababu yo yote?[#Mat. 5:31-32.]

4Naye akajibu akisema: Hamkusoma, ya kuwa Muumbaji hapo mwanzo aliwaumba mume na mke, akasema:[#1 Mose 1:27.]

5Kwa sababu hii mtu atamwacha baba yake na mama yake,

agandamiane na mkewe, nao hao wawili watakuwa mwili

mmoja?

6Kwa hiyo sio wawili tena, ila wamekuwa mwili mmoja tu. Basi, Mungu alichokiunga, mtu asikiungue![#1 Kor. 7:10-11.]

7Wakawambia: Mose aliagiziaje tena kuwapa watu cheti cha kuachana, kisha kuwaacha?[#5 Mose 24:1.]

8Akawaambia: kwa ajili ya ugumu wa mioyo yenu Mose aliwapa ruhusa ya kuwaacha wake zenu. Lakini tokea hapo mwanzo havikuwapo hivyo.

9Nami nawaambiani: Mtu akimwacha mkewe, isipokuwa kwa ajili ya ugoni, akaoa mwingine, anazini; naye anayeoa mke aliyeachwa anazini.[#Mat. 14:4; Luk. 16:18.]

10Wanafunzi wakamwambia: Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa.

11Naye akawaambia: Sio wote wanaoweza kuitambua maana yake neno hili, ni wale tu waliofunuliwa.[#1 Kor. 7:7,11.]

12Kwani katika watu wasiozaa, wako waliozaliwa hivyo tangu tumboni mwa mama zao. Tena wako wengine waliokomeshwa na watu, wasizae. Tena wako wengine waliojikomesha wenyewe, wasizae kwa ajili ya ufalme wa mbingu. Anayeweza kuitambua maana na aitambue!

Kuwabariki watoto.

(13-15: Mar. 10:13-16; Luk. 18:15-17.)

13Hapo ndipo, alipoletewa vitoto, awabandikie mikono na kuwaombea. Lakini wanafunzi waliwatisha.

14Ndipo, Yesu aliposema: Waacheni vitoto, msiwazuie kuja kwangu! Kwani walio hivyo ufalme wa mbingu ni wao[#Mat. 18:2-3.]

15Akawabandikia mikono; kisha akaondoka pale, akaenda zake.

Mwenye mali nyingi.

(16-30: Mar. 10:17-31; Luk. 18:18-30.)

16Hapo ndipo mmoja alipomjia na kusema: Mfunzi mwema, nifanye jambo jema gani, niupate uzima wa kale na kale?

17Naye akamwambia: Unaniulizaje jambo lililo jema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia uzimani yashike maagizo![#Luk. 10:26-28.]

18Alipomwuliza: Yapi? Yesu akasema: Ni haya: Usiue! Usizini! Usiibe! Usisingizie![#2 Mose 20:12-16; 5 Mose 5:17-20.]

19Mheshimu baba na mama! nalo hilo: Umpende mwenzio, kama unavyojipenda mwenyewe![#2 Mose 20:12; 3 Mose 19:18; 5 Mose 5:16.]

20Yule kijana akamwambia: Hayo yote nimeyashika; ninalolisaza la kulifanya ni nini tena?

21Yesu akamwambia: Ukitaka kuyatimiza yote nenda, uviuze, ulivyo navyo, uvigawie maskini! Hivyo utakuwa na kilimbiko mbinguni. Kisha uje, unifuate![#Mat. 6:20; Luk. 12:33.]

22Lakini yule kijana alipolisikia neno hili akaenda zake na kusikitika, kwani alikuwa mwenye mali nyingi.[#Sh. 62:11.]

23Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: Kweli nawaambiani: Ni vigumu, mwenye mali aingie katika ufalme wa mbingu.

24Tena nawaambiani: Masumbuko ya ngamia ya kupenya tunduni mwa sindano ni madogo kuliko yake mwenye mali ya kuingia ufalme wa Mungu.[#Mat. 7:14.]

25Wanafunzi walipoyasikia wakastuka sana, wakasema: Ikiwa hivyo, yuko nani awezaye kuokoka?

26Yesu akawachungua, akawaambia: Kwa watu neno hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana.[#1 Mose 18:14; Iy. 42:2; Zak. 8:6.]

27Hapo Petero akamjibu akimwambia: Tazama, sisi tumeviacha vyote, tukakufuata wewe; basi, tutapata nini?[#Mat. 4:20.]

28Ndipo, Yesu alipowaambia: Kweli nawaambiani: Siku, ulimwengu utakapopata kuwa mpya, Mwana wa mtu atakapokaa katika kiti cha utukufu wake, hapo ndipo nanyi mlionifuata mimi mtakapokaa katika viti vya kifalme kumi na viwili, myahukumu hayo mashina kumi na mawili ya Isiraeli.[#Luk. 22:30; 5 Mose 7:9-10; 1 Kor. 6:2.]

29Ndipo, kila mtu aliyeacha nyumba au kaka au dada au baba au mama au wana au mashamba kwa ajili ya Jina langu atakapoyapata tena na kuongezwa mara nyingi, kisha ataurithi nao uzima wa kale na kale.[#Ebr. 10:34.]

30Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, nao walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.[#Mat. 20:16; Luk. 13:30.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania