The chat will start when you send the first message.
1*Hapo ufalme wa mbingu utafanana na wanawali kumi walioshika taa zao, wakatoka kwenda kumpokea bwana arusi.[#Luk. 12:35-36; Ufu. 19:7.]
2Watano wao walikuwa wajinga, wenzao watano walikuwa werevu.
3Kwani wale wajinga walizishika taa zao tu, wasichukue na mafuta.
4Lakini wale werevu walichukua mafuta katika vichupa pamoja na taa zao.
5Bwana arusi alipokawia, wakasinzia wote, wakalala usingizi.
6Kati ya usiku pakawa na kelele: Tazameni, bwana arusi huyo! Tokeni, mmpokee!
7Ndipo, wanawali wale wote walipoinuka, wakazitengeneza taa zao.
8Lakini wajinga wakawaambia wenzao werevu: Tugawieni mafuta yenu! kwani taa zetu zinazimika.
9Lakini wale werevcu wakajibu wakisema: Sivyo, hayatatutosha sisi na ninyi; sharti mwende kwa wachuuzi, mjinunulie wenyewe!
10Walipokwenda kununua, bwana arusi akafika, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini, kisha mlango ukafungwa.
11Halafu wakaja nao wanawali wale wengine wakasema: Bwana, Bwana, tufungulie![#Luk. 13:25,27.]
12Lakini akajibu akisema: Kweli nawaambiani: Siwajui ninyi.[#Mat. 7:23.]
13Kwa hiyo kesheni! Kwani hamwijui siku wala saa, Mwana wa mtu atakapojia.*[#Mat. 24:42.]
14Kwani vinafanana na mtu aliyefunga safari, akawaita watumwa wake mwenyewe, akawapa mali zake kuzitunza.[#Mat. 21:33.]
15Akampa kila mtu fungu, aliwezalo mwenyewe kulitunza, mmoja fedha elfu tano, mmoja elfu mbili, mmoja elfu moja, kisha akaenda zake.[#Rom. 12:6.]
16Yule aliyepokea elfu tano akaenda, akazichuuzia, akachuma nazo nyingine elfu tano.
17Vile vile na yule aliyepokea elfu mbili, naye akachuma nazo nyingine elfu mbili.
18Lakini yule aliyepokea elfu moja akaenda, akachimba shimo, akazifukia mle fedha za bwana wake.
19Siku zilipopita nyingi, akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao.
20Akaja yule aliyepokea elfu tano, akaleta elfu tano nyingine akasema: Bwana, umenipa elfu tano; tazama, nimechuma elfu tano nyingine.
21Bwana wake akamwambia: Vema, wewe mtumwa mwema na mwelekevu, ulikuwa mwelekevu wa machache, nitakupa kutunza mengi. Ingia penye furaha ya bwana wako![#Mat. 24:45-47; 25:23; Luk. 16:10; 2 Tim. 4:7-8.]
22Akaja na yule aliyepokea elfu mbili, akasema: Bwana, umenipa elfu mbili. Tazama, nimechuma elfu mbili nyingine.
23Bwana wake akamwambia: Vema, wewe mtumwa mwema na mwelekevu, ulikuwa mwelekevu wa machache, nitakupa kutunza mengi. Ingia penye furaha ya bwana wako![#Mat. 25:21.]
24Akaja na yule aliyekuwa amepokea elfu moja, akasema: Bwana, nalitambua, ya kuwa wewe u mkorofi; huvuna, usipopanda, hukusanya, usipotandaza.
25Nikaogopa, nikaenda, nikazifukia fedha zako shimoni. Tazama, hizi mali zako, uzichukue!
26Lakini bwana wake akajibu akimwambia: Mtumwa mbaya wewe! U mvivu! Ulinijua, ya kuwa navuna, nisipopanda, nakusanya nisipotandaza?
27Basi, ilikupasa kuziweka fedha zangu kwao wenye maduka, nami nilipokuja ningalizichukua zilizo zangu pamoja na faida.
28Kwa hiyo ichukueni elfu yake ya fedha, mmpe mwenye elfu kumi!
29Kwani kila mwenye mali atapewa, ziwe nyingi zaidi; lakini asiye na kitu atachukuliwa hata kile, alicho nacho.[#Mat. 13:11-12.]
30Lakini huyu mtumwa asiyefaa mtupeni penye giza lililoko nje! Ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno.[#Mat. 8:12.]
31*Hapo, atakapokuja Mwana wa mtu mwenye utukufu wake na malaika wote pamoja naye, ndipo, atakapokalia kiti cha utukufu wake,[#Mat. 16:27; Zak. 14:5; Ufu. 20:11-13.]
32nayo mataifa yote yatakusanywa mbele yake; naye atawabagua, kama mchungaji anavyowabagua kondoo na mbuzi.[#Mat. 13:48-49; Rom. 14:10; Ufu. 20:12.]
33Atawaweka kondoo kuumeni kwake, nao mbuzi kushotoni.[#Ez. 34:17.]
34Hapo mfalme atawaambia walioko kuumeni kwake: Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme, mliotengenezewa tangu hapo, ulimwengu ulipoumbwa!
35Kwani nilipokuwa na njaa, mlinipa chakula; nilipokuwana kiu, mlininywesha; nilipokuwa mgeni, mlinipokea;[#Yes. 58:7.]
36nilipokuwa uchi, mlinivika; nilipokuwa mgonjwa, mlinikagua; nilipokuwa kifungoni mlinijia.
37Ndipo wale waongofu watakapomjibu: Bwana, ni lini, tulipokuona na njaa, tukakulisha? Au tulipokuona na kiu, tukakunywesha?[#Mat. 6:3.]
38Tena ni lini, tulipokuona mgeni, tukakupokea? Au tulipokuona uchi, tukakuvika?
39Ni lini tena, tulipokuona mgonjwa au kifungoni, tukakujia?
40Naye mfalme atawajibu akisema: Kweli nawaambiani: Yote, mliyomtendea mwenzao mmoja wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.[#Mat. 10:42; Fano. 19:17; Ebr. 2:11.]
41Kisha atawaambia walioko kushotoni: Ondokeni kwangu, mlioapizwa, mwingie kwenye moto usiozimika, uliowashiwa Satani na malaika zake![#Mat. 7:23; Ufu. 20:10,15.]
42Kwani nilipokuwa na njaa, hamkunipa chakula; nilipokuwa na kiu, hamkuninywesha;
43nilipokuwa mgeni, hamkunipokea; nilipokuwa uchi, hamkunivika; nilipokuwa mgonjwa na kifungoni, hamkuja kunikagua.
44Ndipo, nao wale watakapojibu wakisema: Bwana, ni lini, tulipokuona na njaa au na kiu au mgeni au mwenye uchi au mgonjwa au kifungoni, tusikutumikie?
45Hapo atawajibu akisema: Kweli nawaambiani: Yote, msiyomtendea mwenzao mmoja tu wa hawa ndugu zangu wadogo, basi hamkunitendea hata mimi.
46Kisha hawa watakwenda kuingia penye maumivu ya kale na kale. Lakini wale waongofu watakwenda kuingia penye uzima wa kale na kale.*[#Dan. 12:2; Yoh. 5:29; Yak. 2:13.]