The chat will start when you send the first message.
1*Alipotelemka mlimani, makundi mengi ya watu wakamfuata.
2Mara akaja mwenye ukoma, akamwangukia akisema: Bwana, ukitaka waweza kunitakasa.
3Ndipo, Yesu aliponyosha mkono, akamgusa akisema: Nataka, utakaswe. Mara ukoma ukatakaswa.
4Kisha Yesu akamwambia: Tazama, usimwambie mtu! Ila uende, ujionyeshe kwa mtambikaji, ukitoe kipaji, Mose alichokiagiza, kije kinishuhudie kwao.[#Mat. 9:30; Mar. 7:36; Luk. 17:14; 3 Mose 14:2-32.]
5Yesu alipoingia Kapernaumu, mkubwa wa askari akamjia, akambembeleza akisema:
6Bwana, mtoto wangu amelala nyumbani, anaumia vibaya kwa kulemaa.
7Yesu akamwambia: Mimi ninakuja kumponya
8Lakini yule mkubwa wa askari akamjibu akisema: Bwana, hainipasi, uingie kijumbani mwangu, ila sema neno tu! ndipo, mtoto wangu atakapopona!
9Kwani nami ni mtu wa serikali, ninao askari chini yangu. Nami nikimwambia huyu: Nenda! basi, huenda; na mwingine: Njoo! huja; nikimwagiza mtumishi wangu: Vifanye hivi! huvifanya.
10Yesu alipoyasikia akastaajabu, akawaambia waliomfuata: Kweli nawaambiani: Kwa Waisiraeli sijaona bado mtu mwenye kunitegemea kama huyu.[#Mat. 15:28.]
11Lakini nawaambiani: Wengi watatoka maawioni na machweoni kwa jua, watakaa chakulani pamoja na Aburahamu na Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbingu,[#Yes. 49:12; Luk. 13:28-29.]
12lakini wana wa huo ufalme watatupwa penye giza lililoko nje; ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno.[#Mat. 22:13; 24:51; 25:30.]
13Kisha Yesu akamwambia mkubwa wa askari: Nenda kwenu, na uyapate uliyoyategemea! Saa ileile mtoto wake akapona.*[#Mat. 9:29; 15:28.]
14Ikawa, Yesu alipoingia nyumbani mwa Petero, akamwona mama ya mkewe Petero, amelala kwa kuwa na homa.[#1 Kor. 9:5.]
15Alipomgusa mkono, homa ikamwacha, akainuka, akamtumikia.
16Ilipokuwa jioni, wakampelekea wengi waliopagawa na pepo; naye akawafukuza pepo kwa neno tu. Nao wote waliokuwa hawawezi akawaponya,
17kusudi litimizwe lililosemwa na mfumbuaji Yesaya:
Yeye ameyachukua manyonge yetu, akajitwisha maumivu yetu.
(18-22: Luk. 9:57-60.)18Lakini Yesu alipoona, watu wengi wakimzunguka, akaagiza, wavuke kwenda ng'ambo.[#Mar. 4:35; Luk. 8:22.]
19Ndipo, mwandishi mmoja alipomjia, akamwambia: Mfunzi, nitakufuata po pote, utakapokwenda.
20Yesu akamwambia: Mbweha wanayo mapango, nao ndege wa angani wanavyo vituo, lakini Mwana wa mtu hana pa kukilazia kichwa chake.[#2 Kor. 8:9.]
21Mwanafunzi wake mwingine akamwambia: Bwana, nipe ruhusa, kwanza niende, nimzike baba yangu![#1 Fal. 19:20.]
22Yesu akamwambia: Nifuata mimi, waache wafu, wazikane wao kwa wao![#Mat. 10:37; Fil. 3:13.]
23*Alipoingia chomboni, wanafunzi wake wakafuatana naye.
24Mara kukawa na msukosuko mkubwa baharini, hata chombo kilifunikizwa na mawimbi, lakini yeye alikuwa amelala usingizi.
25Ndipo, walipomjia, wakamwamsha wakisema: Bwana, tuokoe, tunaangamia!
26Yesu akawaambia: Mbona mnaogopa hivyo? Mbona mnanitegemea kidogo tu? Kisha akainuka, akaukaripia upepo na bahari, kukawa kimya kabisa.[#Mat. 14:31; 16:8; Sh. 107:23-31.]
27Lakini watu wakastaajabu wakisema: Ni mtu gani huyu, ya kuwa hata upepo na bahari zinamtii?*
28Alipofika ng'ambo katika nchi ya Wagadara, watu wawili waliopagawa na pepo wakakutana naye wakitoka penye makaburi, ni wakorofi mno; kwa hiyo mtu hakuweza kuipita njia ile.
29Mara wakapiga kelele wakisema: Tuko na jambo gani sisi na wewe, mwana wa Mungu? Umejia hapa kutuumiza, siku zetu zikiwa hazijatimia bado?[#Luk. 4:41; 2 Petr. 2:4.]
30Mbali yao kulikuwako kundi la nguruwe wengi waliokuwako malishoni.
31Wale pepo wakambembeleza wakisema: Ukitufukuza, tutume, tuliingie lile kundi la nguruwe!
32Yesu alipowaambia: Haya! Nendeni! ndipo, pepo walipowatoka, wakawaingia nguruwe. Mara kundi lote likatelemka mbio mwambani, wakaingia baharini, wakafa majini;
33lakini wachungaji wakakimbia, wakaenda zao mjini, wakayatangaza yote, hata mambo ya wenye pepo.
34Mara watu wa mji wakatoka wote, wakutane na Yesu. Walipomwona wakambembeleza, atoke mipakani kwao.