Mika 1

Mika 1

Mapatilizo ya Samaria na ya Isiraeli.

1Hili ndilo neno la Bwana lililomjia Mika wa Moreseti siku zile, Yotamu na Ahazi na Hizikia walipokuwa wafalme wa Yuda, ni ono lake la mambo yatakayoijia miji ya Samaria na ya Yerusalemu.[#Yes. 1:1; Yer. 26:18.]

2Sikieni, ninyi makabila yote! Sikilizeni, nchi nao wote

walioko! Bwana Mungu na atoe ushahidi wa kuwashinda ninyi

akitokea katika Jumba lake takatifu.

3Kwani mtamwona Bwana, akiondoka mahali pake,

akishuka akikanyaga juu ya vilima vya nchi.

4Ndipo, milima itakapoyeyuka chini yake,

nayo mabonde yataatuka nyufa;

itayeyuka kama nta motoni,

iwe kama maji yaporomokayo magengeni.

5Hayo yote yatakuja kwa ajili ya upotovu wa Yakobo,

na kwa ajili ya makosa yao walio mlango wa Isiraeli.

Upotovu wa Yakobo ndio nini? Sio ule wa Samaria?

Napo pa kutambikia vilimani ndipo wapi? Sipo Yerusalemu?

6Kwa hiyo nitaugeuza Samaria, uwe chungu la mawe

shambani pa kupandia mizabibu,

nayo mawe yake nitayaporomosha bondeni,

niifunue misingi yake, iwe wazi.

7Vinyago vyao vyote vya kuchonga vitakatwakatwa,

nayo mishahara ya ugoni itateketezwa kwa moto;

vinyago vyao vyote pia nitavitoa, viharibiwe,

kwani wamevipata vyote kuwa mshahara wa ugoni,

navyo vitakuwa mshahara wa ugoni tena.

8Hayo ndiyo, ninayotaka kuyaombolezea na kupiga vilio

nikitembea pasipo nguo kuwa mwenye uchi kabisa,

nifanye maombolezo kama mbweha

na kupiga vilio kama wana wa mbuni.

9Kwani mapigo yako hayaponi, yatamfikia naye Yuda,

yatagonga hata malangoni kwao, walio ukoo wangu,

mle malangoni mwa Yerusalemu.

10Msiyasimulie Gati (Penye Masimulio), msilie kabisa! Gaagaeni uvumbini Beti-Leafura (Nyumba ya Uvumbi)![#2 Sam. 1:20.]

11Jiendeeni mkaao Safiri (Mji wa Mapambo) na kuona soni kwa kuwa wenye uchi! Wakaao Sanani (Matokeo) hawatoki tena, maombolezo ya Beti-Haeseli (Nyumba ya Wanyimaji) yatawanyima fikio.

12Wakaao Maroti (Uchungu) wanaona uchungu kwa ajili ya mema yao, kwani mabaya yameyashukia malango ya Yerusalemu toka kwa Bwana.

13Gari la vita lifungie farasi wenye mbio, ukaaye Lakisi (Panapopigwa Mbio)! Kwani huko ndiko, binti Sioni alikoanzia kukosa, kwani kwao ndiko, mapotovu ya Isiraeli yalikoonekana.

14Kwa hiyo huna budi kutoa vipaji vya kuachana, uwape wa Moreseti-Gati (Uchumba wa Gati). Nyumba za Akizibu (Madanganyo) zitawadanganya wafalme wa Isiraeli.

15Ninyi mkaao Maresa (Wenyeji) nitawaletea mwenyeji wa kweli, utukufu wa Isiraeli utajiendea mpaka Adulamu.

16Jikatie nywele, uwe mwenye kipara kwa ajili ya watoto wako waliokupendeza! Kikuze sana kipara chako, kiwe kama cha ngusu, kwani wametekwa na kuhamishwa kwako.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania