Mika 2

Mika 2

Mabaya yatakayowapata wapotovu.

1Yatawapata wanaowaza maovu,

watungao mabaya vitandani mwao,

wayafanye asubuhi kutakapopambazuka,

mikono yao ikiweza kuyamaliza.

2Kwa kutamani mashamba huyanyang'anya;

ikiwa nyumba, huzichukua nazo,

humkorofisha mwenye nyumba pamoja nao waliomo,

vilevile mwenye shamba, ijapo liwe fungu lake.

3Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Mtayaona mabaya, ninayouwazia mlango huu!

Yakiwapata, hamtaweza kuzitoa shingo zenu mle,

wala hamtaweza kwenda na kuzinyosha shingo zenu,

kwani siku hizo zitakuwa mbaya kweli.

4Siku hiyo watawatungia ninyi mfano,

wataomboleza ombolezo la kwamba:

Imefanyika! Tumeangamizwa!

Mafungu yao walio ukoo wangu anawapa wengine!

Kumbe mimi ameninyang'anya mashamba yetu,

awagawie wao wamkataao!

5Kwa hiyo hamtapata tena katika mkutano wa Bwana

atakayempimia mtu fungu, alilolipata kwa kura.

6Wao huhubiri: Msihubiri! Haifai kuhubiri mambo kama hayo, matusi nayo hayakomi![#Amo. 7:16.]

7Je? Sio walio mlango wa Yakobo wanaosema: Inakuwaje? Roho yake Bwana ni nyepesi ya kukasirika? Au matendo yake ni yayo hayo? Hasemi: Ninamwendea kwa wema ashikaye njia inyokayo?[#Amo. 6:3.]

8Lakini tangu kale mmewainukia walio ukoo wangu, kama ni adui zenu; wapitao pasipo mawazo mabaya mwawavua kanzu za juu na mavazi ya ndani, kama ni mateka ya vitani.

9Wanawake wao walio ukoo wangu mwawafukuza katika nyumba zao zilizowapendeza, watoto wachanga wao mkawanyang'anya utukufu wangu, wasiupate kale na kale.

10Kwa hiyo: Ondokeni! Nendeni! Kwani huku hakuna pa kutulia kwa ajili ya uchafu unaowaangamiza, mwangamie kabisa kabisa.

11Kama angekuja mtu anayegeukageuka kama upepo, anayedanganya watu kwa kuwaongopea, kama angesema: Nitawahubiri mambo ya mvinyo na ya vileo, basi, yeye angekuwa mhubiri, watu hawa wanayemtaka.

Kiagio cha wokovu wa masao ya Isiraeli.

12Kweli nitawaokota nyote pia mlio wa Yakobo;

kweli nitawakusanya mlio masao ya Isiraeli,

niwaweke pamoja zizini kama kondoo,

wawe kama kundi la kondoo walioko katikati ya malisho

yao,

wafanye mtutumo kwa kuwa watu wengi.

13Mwenye kuwavunjia njia atawatangulia,

wapite langoni kwa kupavunja, watoke nje papo hapo;

ndipo, mfalme wao atakapowaongoza,

lakini atakayekwenda mbele yao wote ni Bwana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania