The chat will start when you send the first message.
1Mwisho wa siku utakapotimia,
mlima wenye Nyumba ya Bwana utakuwa umeshikizwa na nguvu,
uwe wa kwanza wa milima, uende juu kuliko vilima vingine;
ndiko, makabila ya watu watakakokimbilia.
2Nao wamizimu wengi watakwenda huko wakisema:
Njoni, tupande mlimani kwa Bwana
kwenye Nyumba ya Mungu wa Yakobo!
Atufundishe, njia zake zilivyo,
tupate kwenda na kuifuata mikondo yake!
Kwani Maonyo yatatoka Sioni,
namo Yerusalemu mtatoka Neno lake Bwana.
3Ndipo, atakapoamulia makabila mengi
na kuwapatiliza wamizimu wenye nguvu wakaao mbali;
nao watazifua panga zao kuwa majembe,
hata mikuki yao kuwa miundu,
kwani hakuna taifa tena litakalochomolea jingine panga,
wala hawatajifundisha tena mapigano ya vita.
4Watakaa kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya
mkuyu wake
pasipo kuona atakayewastusha,
kwani kinywa cha Bwana Mwenye vikosi kimeyasema.
5Kwani makabila yote kila moja
hujiendea katika jina la mungu wake,
lakini sisi tutakwenda kwa Jina la Bwana Mungu wetu
siku zote kale na kale.
6Ndivyo, asemavyo Bwana:
Siku hiyo nitawaokota wachechemeao,
niwakusanye waliotawanyika nao niliowafanyizia mabaya.
7Kisha nitawaweka wachechemeao kuwa masao,
nao walioko mbali kuwa taifa lenye nguvu,
naye Bwana atakuwa mfalme wao mlimani kwa Sioni
toka sasa hata kale na kale.
8Nawe mnara wa kulindia makundi, wewe kilima cha binti Sioni,
kwako wewe utarudi tena, ukufikie,
ule utawalaji wa kwanza, ndio ufalme wa binti
Yerusalemu.
9Mbona unapiga makelele sasa? Je? Mfalme hayumo mwako?
Au ameangamia akuongozaye,
uchungu ukikupata kama wa mwanamke anayezaa?
10Jipinde na kupiga kite kama mwanamke anayezaa, binti
Sioni!
Kwani sasa huna budi kutoka mjini,
ukae porini, mpaka ufike Babeli;
huko ndiko, Bwana atakakokuponya
akikukomboa mikononi mwa adui zako.
11Lakini sasa wamizimu wengi watakukusanyikia wakisema:
Sioni na uchafuliwe, macho yetu yaufurahie.
12Lakini wao hawayajui mawazo ya Bwana,
wala hawalitambui shauri lake,
ya kuwa ni yeye aliyewakusanya kama miganda penye
kupuria.
13Inuka, binti Sioni, uwapure!
Kwani pembe zako nitazigeuza kuwa chuma
nayo kwato zako kuwa shaba,
upate kuponda makabila mengi,
umtolee Bwana mapato yao, yawe yake,
nazo mali zao, ziwe zake yeye aliye Bwana wa nchi zote.
14Sasa jikusanyeni, wana wa mkutano!
Kwani wametujengea boma, watusonge,
naye mwamuzi wa Isiraeli wanampiga shavuni kwa fimbo.