The chat will start when you send the first message.
1Akaondoka huko, akaja mipakani kwa Yudea na ng'ambo ya Yordani. Walipomkusanyikia tena makundi ya watu, akawafundisha tena, kama alivyozoea.[#Mar. 9:33.]
2Mafariseo wakamjia, wakamwuliza, kama iko ruhusa, mwanamume amwache mkewe.
3Naye akajibu akiwaambia: Mose aliwaagiza nini?
4Nao wakasema: Mose alitupa ruhusa kuandika cheti cha kuachana, kisha kumwacha.[#5 Mose 24:1; Mat. 5:31-32.]
5Yesu akawaambia: Kwa ajili ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia agizo hilo.
6Lakini tokea hapo mwanzo wa viumbe aliwaumba mume na mke.[#1 Mose 1:27.]
7Kwa sababu hii mtu atamwacha baba yake na mama yake,
8nao hao wawili watakuwa mwili mmoja.
9Kwa hiyo sio wawili tena, ila wamekuwa mwili mmoja tu. Basi, Mungu alichokiunga, mtu asikiungue!
10Nyumbani wanafunzi wakamwuliza tena kwa ajili ya neno hilo.
11Akawaambia: Mtu akimwacha mkewe na kuoa mwingine anazini naye.[#Luk. 16:18.]
12Naye mke akimwacha mumewe na kuolewa na mwingine anazini.
13*Wakamletea vitoto, awaguse. Lakini wanafunzi waliwatisha waliowaleta.
14Yesu alipoviona akachukizwa, akawaambia: Waacheni vitoto, waje kwangu, msiwazuie! Kwani walio hivyo ufalme wa Mungu ni wao.
15Kweli nawaambiani: Mtu asiyeupokea ufalme wa Mungu kama kitoto hatauingia kamwe.[#Mat. 18:3.]
16Kisha akawakumbatia, akawabariki akiwabandikia mikono.*[#Mar. 9:36.]
17*Alipotoka na kufika njiani, mmoja akamjia mbio, akampigia magoti, akamwuliza: Mfunzi mwema, nifanye nini, niurithi uzima wa kale na kale?
18Yesu akamwambia: Unaniitaje mwema? Hakuna aliye mwema, asipokuwa Mungu peke yake tu.
19Maagizo unayajua, ya kwamba: Usiue! Usizini! Usiibe! Usisingizie! Usipunje! Mheshimu baba yako na mama yako![#2 Mose 20:12-16; 5 Mose 5:16-20.]
20Naye akamwambia: Mfunzi, hayo yote nimeyashika, tangu nilipokuwa kijana.
21Yesu akamtazama, akampenda, akamwambia: Umesaza kimoja: nenda, uviuze vyote, ulivyo navyo, uvigawie maskini! Hivyo utakuwa na kilimbiko mbinguni. Kisha uje, ujitwishe msalaba wako, unifuate![#Mar. 8:34; Mat. 10:38.]
22Lakini alipolisikia neno hili alikunjamana uso, akaenda zake na kusikitika, kwani alikuwa mwenye mali nyingi.
23Kisha Yesu akatazama huko na huko, akawaambia wanafunzi wake: Vitazameni vigumu vinavyowazuia waegemeao mali kuingia katika ufalme wa Mungu!
24Wanafunzi walipoingiwa na kituko kwa hayo mnaneno yake, Yesu akajibu, akawaambia tena: Wanangu, vitazameni vigumu vinavyozuia kuingia katika ufalme wa Mungu![#Sh. 62:11; 1 Tim. 6:17.]
25Masumbuko ya ngamia ya kupenya tunduni mwa sindano ni madogo kuliko yake mwenye mali ya kuuuingia ufalme wa Mungu.
26Nao wakastuka mno, wakasemezana wao kwa wao: Ikiwa hivyo, yuko nani awezaye kuokoka?
27Yesu akawachungua, akasema: Kwa watu haliwezekani, lakini kwa Mungu linawezekana, kwani kwa Mungu mambo yote huwezekana.*[#1 Mose 18:14; Iy. 42:2.]
28Petero akaanza kumwambia: Tazama, sisi tumeviacha vyote, tukakufuata wewe.
29Ndipo, Yesu aliposema: Kweli nawaambiani: Hakuna mtu aliyeacha nyumba au kaka au dada au mama au baba au wana au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Utume mwema,
30asiporudishiwa na kuongezwa mara mia siku hizi za kuwapo huku nchini nyumba na kaka na dada na mama na wana na mashamba, hata akiwa anafukuzwafukuzwa. Tena siku zile zitakazokuja ataupata nao uzima wa kale na kale.
31Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, nao walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.
32Walipokuwa njiani wakipanda kwenda Yerusalemu, Yesu alikuwa anatangulia mbele yao. Nao wakashikwa na kituko, wakamfuata na kuogopa. Akawachukua tena wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia mambo yatakayompata,[#Mar. 9:31; Yoh. 11:16,55.]
33akasema: Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu. Huko Mwana wa mtu atatiwa mikononi mwao watambikaji wakuu na waandishi, nao watamhukumu, auawe; kwa hiyo watamtia mikononi mwa wamizimu.
34Ndio watakaomfyoza na kumtemea mate na kumpiga viboko na kumwua. Naye, siku tatu zitakapopita, atafufuka.
35*Yakobo na Yohana, wana wa Zebedeo, wakamsogelea wakimwambia: Mfunzi, twataka, ufufanyie lo lote, tutakalokuomba.
36Alipowauliza: Mwataka, niwafanyie nini?
37wakamwambia: Utuketishe mmoja kuumeni na mmoja kushotoni kwako katika utukufu wako!
38Yesu akawaambia: Hamjui, mnaloliomba. Mwaweza kukinywa kinyweo, ninachokinywa mimi, au kubatizwa ubatizo, ninaobatizwa mimi?[#Mar. 14:36; Luk. 12:50; Rom. 6:3.]
39Walipomwambia: Twaweza, Yesu akawaambia: Kinyweo, ninachokinywa mimi, mtakinywa nao ubatizo, ninaobatizwa mimi, mtabatizwa;[#Tume. 12:2; Ufu. 1:9.]
40lakini kumketisha mtu kuumeni au kushotoni kwangu hii si kazi yangu, ila hupewa walioandaliwa.
41Wenzao kumi walipoyasikia wakaanza kumkasirikia Yakobo na Yohana.
42Yesu akawaita, wamjongelee, akawaambia: Mnajua: wanaotazamwa kuwa wafalme wa mataifa huwatawala, nao wakubwa wao huwatumikisha kwa nguvu. Kwenu ninyi visiwe hivyo![#Luk. 22:25-27.]
43Ila mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu sharti awe mtumishi wenu![#Mar. 9:35.]
44Naye anayetaka kuwa wa kwanza kwenu sharti awe mtumwa wao wote!
45Kwani naye Mwana wa mtu hakuja, atumikiwe, ila amekuja kutumika na kuitoa roho yake kuwa makombozi ya watu wengi.
46Wakafika Yeriko. Nao walipotoka Yeriko, yeye na wanafunzi wake na kundi la watu wengi, Bartimeo, mwana wa Timeo, aliyekuwa kipofu alikaa njiani kando akiomba sadaka.
47Aliposikia, ya kuwa Yesu wa Nasareti yuko, akaanza kupaza sauti na kusema: Yesu, mwana wa Dawidi, nihurumie!
48Wengi walipomkaripia, anyamaze, yeye akakaza sana kupaza sauti: Mwana wa Dawidi, nihurumie!
49Ndipo, Yesu aliposimama, akasema: Mwiteni! Wakamwita kipofu, wakamwambia: Tulia moyo, inuka! anakuita.
50Naye akaitupa kanzu yake, akainuka upesi, akaja kwa Yesu.
51Yesu alipomwuliza akisema: Wataka, nikufanyie nini? kipofu akamwambia: Mfunzi mkuu, nataka, nipate kuona.
52Yesu akamwambia: Enenda! Kunitegemea kwako kumekuponya. Mara akapata kuona, akamfuata njiani.