Marko 13

Marko 13

Mambo yatakayokuja.

(1-37: Mat. 24; Luk. 21:5-36.)

1Alipotoka Patakatifu, mwanafunzi wake mmoja akamwambia: Mfunzi, yatazame mawe hayo makubwa na majengo hayo makubwa!

2Yesu akamwambia: Je? Wayatazama majengo haya makubwa? Halitaachwa hata jiwe moja juu ya jiwe lenziwe lisiloporomoshwa chini.

3Kisha alipokaa mlimani pa michekele kupaelekea Patakatifu, ndipo, Petero na Yakobo na Yohana na Anderea walipomwuliza walipokuwa peke yao wakisema:

4Tuambie, hayo yatakuwapo lini? Tena kielekezo ni nini, hayo yote yatakapotimia?

5Yesu akaanza kuwaambia: Angalieni, mtu asiwapoteze!

6Wengi watakuja kwa jina langu na kusema: Mimi ndiye,

7nao watapoteza wengi. Nanyi mtakaposikia vita na mavumi ya vita msivihangaikie! Hivyo sharti viwepo, lakini huo sio mwisho.

8Kwani watainukiana taifa na taifa, tena wafalme na wenzao wafalme. Mahali penginepengine patakuwa na matetemeko, pengine na njaa. Hayo ni mwanzo tu wa uchungu.[#2 Mambo 15:6; Yes. 19:2.]

(9-13: Mat. 10:17-22; Luk. 21:12-17.)

9Lakini ninyi jiangalieni wenyewe! Watawapeleka barazani kwao wakuu namo nyumbani mwa kuombea, mpigwe, kisha mtasimamishwa kwa ajili yangu mbele ya mabwana wakubwa na mbele ya wafalme, mje mnishuhudie kwao.

10Nao Utume mwema sharti utangazwe kwanza kwa mataifa yote.[#Mar. 16:15.]

11Napo hapo, watakapowatoa na kuwapeleka, msianze kuyahangaikia maneno ya kusema, ila maneno mtakayopewa saa ile yasemeni yaleyale! Kwani si ninyi mnaosema, ila ni Roho Mtakatifu.

12Itakuwa hivi: ndugu na ndugu watatoana, wauawe, hata baba watawatoa watoto wao, hata watoto watawainukia wazazi wao, wawaue.

13Nanyi mtakuwa mmechukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka.[#Yoh. 15:18,21.]

14Hapo ndipo, mtakapochafukwa mioyo mkiona, mwangamizaji atapishaye akisimama mahali pasipompasa; mwenye kupasoma hapa sharti aangalie, ajue maana! Siku zile watakaokuwako Yudea na wakimbilie milimani![#Dan. 9:27; 11:31; 12:4,10.]

15Mtu atakayekuwapo nyumbani juu asishuke na kuingia nyumbani mwake kuchukua kilichomo!

16Naye atakayekuwako shambani asiyarudie yaliyoko nyuma, aichukue nguo yake!

17Lakini watakaoona vibaya zaidi ndio wenye mimba na wenye kunyonyesha siku zile.

18Lakini ombeni, hayo yasitimie siku za kipupwe![#Dan. 12:1; Yoe. 2:2.]

19Kwani siku zile zitakuwa na maumivu makuu kuyapita yote yaliyopatikana tangu mwanzo wa viumbe, Mungu alivyoviumba, mpaka sasa, hata halafu hayatapatikana tena kama hayo.

20Nazo siku zile kama Bwana hangalizipunguza, hangaliokoka mtu hata mmoja. Lakini kwa ajili ya wale, waliochaguliwa, aliowachagua, amezipunguza siku zile.

21Hapo mtu akiwaambia: Tazama, huyu hapa ni Kristo! au: Tazama, yule kule! msiitikie!

22Watainuka makristo wa uwongo na wafumbuaji wa uwongo; nao watafanya vielekezo na vioja, wawapoteze waliochaguliwa, kama inawezekana.[#5 Mose 12:32; 13:1-3.]

23Lakini ninyi angalieni! Nimetangulia kuwaambia yote.

24Lakini siku zile, yale maumivu yatakapopita, jua litakuwa jeusi lenye giza, nao mwezi hautaumulikisha mwanga wake.[#Yes. 13:10.]

25Nazo nyota zitakuwa zinaanguka toka mbinguni, nazo nguvu za mbingu zitatukutishwa.[#Yes. 34:4.]

26Hapo ndipo, watakapomwona Mwana wa mtu, anavyokuja katika mawingu mwenye nguvu na utukufu mwingi.[#Dan. 7:13.]

27Ndipo, atakapowatuma malaika, awakusanye waliochaguliwa naye toka pande zote nne, upepo unapotokea, aanzie mwanzoni kwa nchi, aufikishe mwisho wa mbingu.[#5 Mose 30:4; Zak. 2:6; Mat. 13:41.]

28Jifundisheni mfano kwa mkuyu: matawi yake yanapochipua na kuchanua majani, mnatambua, ya kuwa siku za vuli ziko karibu.

29Vivyo hivyo nanyi mtakapoyaona hayo, yakiwapo, tambueni, ya kuwa mwisho umewafikia milangoni!

30Kweli nawaambiani: Kizazi hiki hakitakoma mpaka hapo, yatakapokuwapo hayo yote.

31Mbingu na nchi zitakoma, lakini maneno yangu hayatakoma.

32Lakini ile siku au saa yake itakapofikia, mtu hapajui, wala malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba tu.

33Angalieni! Kesheni! Kwani hamjui, siku zake zitakapokuwapo. Vinafanana na mtu mwenye kufunga safari aliyeiacha nyumba yake, akawapa watumishi wake nguvu akimgawia kila mtu kazi yake, naye mlinda mlango akamwagiza, akeshe.

34Basi, hivyo kesheni! Kwani hamjui, mwenye nyumba atakaporudia, kama atakuja jioni au kati ya usiku au jogoo awikapo au mapema.[#Mat. 25:14; Luk. 19:12.]

35Asije na kuwastusha akiwakuta, mmelala.[#Luk. 12:38.]

36Hilo, ninalowaambia ninyi, nawaambia wote: Kesheni!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania