The chat will start when you send the first message.
1Asubuhi kulipokucha, papo hapo watambikaji wakuu wakala njama pamoja na wazee na waandishi nao wote wa baraza ya wakuu wote, wakamfunga Yesu, wakampeleka, wakamtia mikononi mwa Pilato.
(2-19: Mat. 27:11-30; Luk. 23:2-25; Yoh. 18:29-19:16.)2Pilato alipomwuliza: Wewe ndiwe mfalme wa Wayuda? akamjibu akimwambia: Wewe unavyosema, ndivyo.
3Watambikaji wakuu walipomsuta mengi,
4Pilato akamwuliza tena: Hujibu neno? Tazama yote, wanayokusuta!
5Lakini Yesu hakujibu neno tena, ikawa, Pilato akastaajabu.[#Mar. 14:61; Yes. 53:7.]
6Kwa desturi ya sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, waliyemtaka.
7Kulikuwako mtu, jina lake Baraba, alifungwa pamoja na watu waliofunga kondo na kuua watu.
8Watu wengi walipokwenda bomani kwa kutaka, kwanza awafanyie, kama alivyozoea,
9Pilato akawajibu akisema: Mwataka, niwafungulie mfalme wa Wayuda?
10Kwani alitambua, ya kuwa watambikaji wakuu walikuwa wamemtoa kwa wivu.[#Mat. 21:36; Yoh. 11:48; 12:19.]
11Lakini watambikaji wakuu wakalichochea hilo kundi la watu, sharti awafungulie Baraba.
12Pilato akajibu tena akiwaambia: Basi, nimfanyie nini huyu, mnayemwita mfalme wa Wayuda?
13Wakapiga kelele tena kwamba: Mwambe msalabani!
14Pilato alipowauliza: Ni kiovu gani alichokifanya? wakakaza kupiga makelele kwamba: Mwambe msalabani!
15Ndipo, Pilato, kwa kuwa alitaka kuyafanya yanayopendeza watu, alipowafungulia Baraba, lakini Yesu akamtoa, apigwe viboko, kisha awambwe msalabani.
16Nao askari wakampeleka, wakamwingiza uani mwa bomani, wakakiita kikosi chote cha askari, wakusanyike.
17Wakamvika nguo nyekundu, wakasuka kilemba cha miiba, wakamvika kichwani,
18wakaanza kumwamkia: Pongezi, mfalme wa Wayuda!
19Kisha wakampiga kichwani kwa mwanzi, wakamtemea mate, wakampigia magoti na kumwangukia.
(20-41: Mat. 27:31-56; Luk. 23:26-49; Yoh. 19:16-30.)20Walipokwisha kumfyoza, wakamvua ile nguo nyekundu na kumvika nguo zake, wakampeleka nje, waje, wamwambe msalabani.
21Wakakamata mtu aliyepiga akitoka shambani; ni Simoni wa Kirene, baba yao Alekisandro na Rufu, wakamshurutisha, amchukulie msalaba wake.[#Rom. 16:13.]
22Wakampeleka mahali pa Golgota, maana yake ni kwamba: Fuvu la kichwa.
23Wakampa mvinyo iliyochanganyika na manemane, lakini hakunywa.[#Sh. 69:22.]
24Walipokwisha kumwamba msalabani, wakazigawanya nguo zake na kuzipigia kura, ndizo mtu achukue.[#Sh. 22:19.]
25Lakini ilikuwa saa tatu, walipomwamba msalabani.
26Juu yake kulikuwa na andiko la mashtaka yake la kwamba: MFALME WA WAYUDA.
27Pamoja naye wakawamba misalabani wanyang'anyi wawili, mmoja kuumeni, mmoja kushotoni kwake.
28Ndipo, lilipotimia lile neno la kwamba:
Akahesabiwa kuwa mwenzao wapotovu.
29Waliopita wakamtukana, wakavitingisha vichwa vyao wakisema: Wewe unayelivunja Jumba la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu,[#Sh. 22:8; 109:25; Mar. 14:58.]
30jiokoe mwenyewe, ushuke mtini!
31Vilevile nao watambikaji wakuu wakamfyoza pamoja na waandishi wakisema wao kwa wao: Wengine aliwaokoa, lakini mwenyewe hawezi kujiokoa.
32Huyu Kristo, mfalme wa Waisiraeli, ashuke sasa hivi msalabani, tuvione, tupate kumtegemea! Hata wale waliowambwa misalabani pamoja naye wakamtukana.[#Mat. 16:1,4.]
33Ilipokuwa saa sita, pakawa na giza katika nchi yote nzima mpaka saa tisa. Ilipokuwa saa tisa, Yesu akapaza sauti sana:
34Eli, Eli, lama sabaktani? Maana yake ni kwamba: Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?[#Sh. 22:2.]
35Wengine wao waliosimama hapo walipoyasikia wakasema: Tazama, anamwita Elia!
36Mmoja akapiga mbio, akachovya mwani sikini, akautia katika utete, akamnywesha akisema: Acheni, tuone, kama Elia anakuja kumshusha!
37Kisha Yesu akatoa sauti kubwa, nayo pumzi ikamtoka.
38Ndipo, pazia la Jumbani mwa Mungu lilipopasuka toka juu mpaka chini, likawa vipande viwili.
39Lakini bwana askari aliyesimama hapo na kumwelekea alipoona, pumzi ilivyomtoka, akasema: Kweli, mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.
40Palikuwako nao wanawake, walisimama mbali wakitazama. Kati yao walikuwapo Maria Magadalene na Maria, mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome;[#Luk. 8:2-3.]
41ndio waliomfuata na kumtumikia yeye, alipokuwa huko Galilea. Palikuwako nao wengine wengi walipanda pamoja naye kwenda Yerusalemu.
42Ilipokwisha kuwa jioni, kwa sababu ilikuwa andalio, ndio siku ya kutangulia sikukuu,
43akaja Yosefu wa Arimatia aliyekuwa mkuu mwenye macheo; naye mwenyewe alikuwa akiungoja ufalme wa Mungu. Akajipa moyo, akaingia kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu.
44Pilato akastaajabu aliposikia, ya kuwa amekwisha kufa, akamwita bwana askari, akamwuliza, kama amekwisha kufa.
45Alipotambulishwa na bwana askari akampa Yosefu mwili wake.
46Naye akanunua sanda, akamshusha msalabani, akamtia katika ile sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa mwambani, akafingirisha jiwe mlangoni pa kaburi.
47Nao akina Maria Magadalene na Maria, mama yake Yose, wakatazama, alipowekwa.