Marko 2

Marko 2

Mwenye kupooza.

(1-12: Mat. 9:1-8; Luk. 5:17-26.)

1Siku zilipopita, akaingia tena Kapernaumu. Watu waliposikia, ya kuwa yumo nyumbani,

2wakakusanyika wengi, wasienee mle nyumbani, wala mlangoni, akawaambia lile Neno.

3Kukaja watu waliomletea mgonjwa wa kupooza, akichukuliwa na watu wanne;

4wasipoweza kumpelekea yeye kwa ajili ya watu wengi wakafumua paa hapo, alipokuwapo. Walipokwisha kupatoboa wakakishusha kitanda, alichokilalia yule mgonjwa wa kupooza.

5Yesu alipoona, walivyomtegemea, akamwambia mwenye kupooza: Mwanangu, makosa yako yameondolewa.

6Mlikuwamo na waandishi waliokaa mlemle, wakawaza mioyoni mwao ya kwamba: Haya huyu anayasemaje? Anambeza Mungu

7Yuko nani awezaye kuondoa makosa? Siye Mungu peke yake?[#Sh. 51:6; 130:3-4; Yes. 43:25.]

8Kwa kutambua rohoni mwake, ya kuwa wanawaza hivyo mioyoni mwao, Yesu akawaambia: Mbona mnawaza hivyo mioyoni mwenu?

9Kilicho chepesi ni kipi? Kumwambia mwenye kupooza: Makosa yako yameondolewa! au kusema: Inuka, ukichukue kitanda chako, uende?

10Lakini kusudi mpate kujua, ya kuwa Mwana wa mtu ana nguvu ya kuondoa makosa nchini, akamwambia mwenye kupooza:

11Nakuambia: Inuka, jitwishe kitanda chako, uende nyumbani kwako!

12Ndipo, alipoinuka, akajitwisha papo hapo kitanda, akatoka machoni pao wote. Kwa hiyo wote wakashangaa, wakamtukuza Mungu wakisema: Yaliyo kama hayo hatujayaona kamwe.

Lawi (Mateo) anaitwa.

(13-17: Mat. 9:9-13; Luk. 5:27-32.)

13Alipotoka tena kwenda kandokando ya bahari, kundi lote la watu likamjia, akawafundisha.

14Kisha alipokuwa akitembea akamwona Lawi, mwana wa Alfeo, amekaa forodhani. Akamwambia: Nifuata! Akainuka, akamfuata.[#Yoh. 1:43.]

15Ikawa, alipokaa chakulani nyumbani mwake, ndipo, watoza kodi na wakosaji wengi walipokaa chakulani pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwani walikuwa wengi walipokaa chakulani pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwani walikuwa wengi waliomfuata.

16Waandishi wa Kifariseo walipomwona, ya kuwa anakula pamoja na wakosaji na watoza kodi, wakawaambia wanafunzi wake; Kumbe anakula pamoja na watoza kodi na wakosaji!

17Yesu alipoyasikia akawaambia: Walio wazima hawapaswi na mganga, ila walio wagonjwa. Sikujia kuwaita waongofu, ila wakosaji.

Kufunga.

(18-22: Mat. 9:14-17; Luk. 5:33-38.)

18Wanafunzi wa Yohana na Mafariseo walikuwa wakifunga. Wakaja, wakamwambia: Kwa nini wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafariseo hufunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?

19Yesu akawaambia: Walioalikwa arusini hawawezi kufunga, bwana arusi akingali pamoja nao. Siku zote, wanapokuwa na bwana arusi, hawawezi kufunga.

20Lakini siku zitakuja, watakapoondolewa bwana arusi; siku ile ndipo, watakapofunga.

21Hakuna mtu anayetia kiraka cha nguo mpya katika kanzu chakavu; kama anafanya hivyo, kile kiraka kipya kinaondoa pote paliposhonwa katika kanzu chakavu; hivyo tundu lake litakuwa kubwa zaidi.

22Wala hakuna mtu anayetia mvinyo mpya katika viriba vichakavu; kwani akiitia mle, mvinyo itavipasua viriba, nayo mvinyo itaangamia pamoja na viriba. Ila mvinyo mpya hutiwa katika viriba vipya.

Kukonyoa masuke.

(23-28: Mat. 12:1-8; Luk. 6:1-5.)

23Akawa akipita katika mashamba siku ya mapumziko; nao wanafunzi wake wakaanza kuendelea njiani wakikonyoa masuke.

24Lakini Mafariseo wakamwambia: Tazama! Mbona wanafanya siku ya mapumziko yaliyo mwiko?

25Naye akawaambia: Hamjasoma bado, Dawidi alivyofanya alipokosa chakula, wakaona njaa yeye na wenziwe?

26Hapo aliingia Nyumbani mwa Mungu kwa mtambikaji mkuu Abiatari, akaila mikate aliyowekewa Bwana, nayo kuila ni mwiko, huliwa na watambikaji tu; kisha akawapa nao wenziwe waliokuwa naye.[#3 Mose 24:9; 1 Sam. 21:6.]

27Akawaambia: Siku ya mapumziko iliwekwa kwa ajili ya mtu; lakini mtu hakuwekwa kwa ajili ya siku ya mapumziko.[#5 Mose 5:11.]

28Kwa hiyo Mwana wa mtu ni bwana hata wa siku ya mapumziko.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania