The chat will start when you send the first message.
1Akaanza tena kufundisha kandokando ya bahari. Wakamkusanyikia kundi la watu wengi mno; kwa hiyo akaingia chomboni, akakaa ufukoni, watu wote wakiwa pwani kandokando ya bahari.
2Akawafundisha maneno mengi kwa mifano, akawaambia katika mafunzo yake:
3Sikilizeni! Tazameni, mpanzi alitoka kumiaga mbegu.
4Ikawa, alipozimiaga, nyingine zikaangukia njiani; ndege wakaja, wakazila.
5Nyingine zikaangukia penye miamba pasipo na udongo mwingi. Kuota zikaota upesi kwa kuwa na udongo kidogo,
6lakini jua lilipokuwa kali, zikanyauka, kwa kuwa hazina mizizi.
7Nyingine zikaangukia penye miiba; nayo miiba ilipoota ikazisonga, zisizae.
8Nyingine zikaangukia penye mchanga mzuri, zikazaa zikikua na nguvu, zikatoa kama punje thelathini, hata sitini, hata mia.
9Akasema: Mwenye masikio yanayosikia na asikie!
10Naye alipokuwa peke yake, wafuasi wake pamoja na wale kumi na wawili wakamwuliza maana ya mifano.
11Akawaambia: Ninyi mmepewa kulitambua fumbo la ufalme wa Mungu, lakini wale walioko nje huambiwa hayo yote kwa mifano,[#1 Kor. 5:12.]
12kusudi watazame, lakini wasione, wasikilize, lakini wasijue maana, wasije wakanigeukia, wakaondolewa makosa.[#Yes. 6:9-10.]
13Akawaambia: Msipoujua mfano huu mtaitambuaje mifano yote?
14Mwenye kumiaga analimiaga Neno.
15Lakini zilizoko njiani ndio hao: Neno linapomiagwa, wakiisha kulisikia, papo hapo Satani huja, akaliondoa Neno lililomiagwa mwao.
16Vilevile zilizomiagwa penye miamba ndio hao: wanapolisikia Neno, papo hapo hulipokea kwa furaha,
17lakini hawana mizizi mioyoni mwao, ila wanalishika kwa kitambo kidogo tu. Yanapotukia maumivu au mafukuzo kwa ajili ya Neno, mara hujikwaa.
18Nyingine ndizo zilizomiagwa penye miiba, ndio hao: wanalisikia Neno,
19lakini masumbuko ya dunia hii na udanganyifu wa mali na tamaa nyingine zikiwaingia hulisonga Neno, lisizae matunda.[#Mar. 10:23-24.]
20Nazo zile zilizomiagwa penye mchanga mzuri ndio hao: wanalisikia Neno na kulipokea, kisha huzaa matunda, kama thelathini, hata sitini, hata mia.
21Akawauliza: Iko taa inayoletwa, iwekwe chini ya kapu au mvunguni mwa kitanda? Hailetwi, iwekwe juu ya mwango?[#Mat. 5:15-16.]
22Kwani hakuna lililofichwa, isipokuwa kwamba lipate kufunuliwa halafu; wala hakuna njama, ila kwamba ipate kutokea waziwazi.[#Mat. 10:26-27; Luk. 12:2.]
23Mtu akiwa na masikio yanayosikia na asikie!
24Akawaambia: Mwangalie, jinsi mnavyosikia! Kipimo, mnachokipimia wengine, ndicho, mtakachopimiwa nanyi, tena mtaongezewa.[#Mat. 7:2.]
25Kwani aliye na mali atapewa; lakini asiye na kitu atachukuliwa hata kile, alicho nacho.[#Mat. 13:12-13.]
26*Akasema: Ufalme wa Mungu unakuwa hivyo, kama mtu anayemiaga mbegu katika nchi.
27Kisha hulala na kuamka usiku na mchana, nazo mbegu humea na kukua, yeye asivijue, vilivyo.[#Yak. 5:7.]
28Nchi huzaa yenyewe kwanza hutoa mimea, halafu suke, halafu ngano zinazojaa katika suke.
29Lakini punje zinapopevuka, mwenyewe mara hutuma wenye miundu, kwani mavuno yamefika.*[#Yoe. 3:13.]
30Akasema: Ufalme wa Mungu tuufananishe na nini? Au tuueleze kwa mfano gani?
31Umefanana na kipunje cha haradali. Kinapopandwa katika nchi ni kidogo kuliko mbegu zote zilizoko huku nchini.
32Tena kikiisha pandwa hukua, kiwe mkubwa kuliko miboga yote kwa kuchipuza matawi makubwa, hata ndege wa angani huweza kuja na kutua katika kivuli chake.[#Ez. 17:23; 31:6; Dan. 4:9,18.]
33Kwa mifano mingi inayofanana na huu akawaambia Neno, kama walivyoweza kusikia; lakini pasipo mfano hakuwaambia neno.
34Lakini wanafunzi wake akawafungulia yote, walipokuwa peke yao.
35Siku ile ilipokuwa jioni, akawaambia: Tuvuke kwenda ng'ambo!
36Wakaliacha kundi la watu, wakamchukua hivyo alivyokuwa chomboni; navyo vyombo vingine vilikuwa pamoja naye.
37Kukawa na msukosuko mkubwa wa upepo, mawimbi yakakipigapiga chombo, hata chombo kikawa kinajaa maji.
38Naye alikuwa chomboni upande wa nyuma, amelala usingizi juu ya mto. Ndipo, walipomwamsha wakimwambia: Mfunzi, huoni uchungu, tukiangamia?
39Akainuka, akaukaripia upepo, akaiambia bahari: Nyamaza, utulie! Papo haupepo ukakoma, kukawa kimya kabisa.
40Kisha akawaambia: Mbona mnaogopa hivyo? Mbona hamnitegemei?
41Wakaingiwa na woga mkubwa, wakasemezana wao kwa wao: Ni mtu gani huyu, ya kuwa hata upepo na bahari zinamtii?