The chat will start when you send the first message.
1Wakafika ng'ambo ya bahari katika nchi ya Wagerasi.
2Alipotoka chomboni papo hapo akakutana na mtu mwenye pepo mchafu aliyetoka penye makaburi.
3Kwa kuwa hukaa pale penye makaburi, hakuwako mtu aliyeweza kumfunga kwa mnyororo wo wote.
4Kwani alikuwa amefungwa mara nyingi kwa mapingu na kwa minyororo, lakini minyororo ikararuliwa naye, nayo mapingu yakasagwa naye, mpaka yakikatika, kwa hiyo hakukuwako kabisa mtu mwenye nguvu za kumshinda.
5Siku zote mchana kutwa alikuwa penye makaburi nako milimani akipiga makelele na kujipigapiga mawe mwenyewe.
6Alipomwona Yesu, yuko mbali bado, akapiga mbio, akaja, akamwangukia,
7akapaza sana sauti akisema: Tuko na jambo gani mimi na wewe Yesu, Mwana wa Mungu Alioko huko juu? Nakuapisha kwa Mungu, usiniumize![#Mar. 1:24.]
8Kwani alikuwa amemwambia: Wee pepo mchafu, umtoke mtu huyu!
9Alipomwuliza: Jina lako nani? akamwambia: Jina langu mimi Maelfu, kwa kuwa tumo wengi.
10Akambembeleza sana, asiwafukuze, waitoke nchi ile.
11Basi, kulikuwako kule mlimani kundi kubwa la nguruwe waliokuwako malishoni.
12Wakambembeleza wakisema: Tutume kwenda kwao wale nguruwe, tupate kuwaingia!
13Alipowapa ruhusa, pepo wachafu wakamtoka, wakawaingia nguruwe; ndipo, kundi lilipotelemka mbio mwambani, wakaingia baharini, wapata kama 2000, wakatoswa baharini.
14Lakini wachungaji wao wakakimbia, wakayatangaza mjini na mashambani. Watu wakaja, watazame, lililofanyika lilivyo.
15Walipofika kwa Yesu na kumtazama yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu wa Maelfu, anavyokaa amevaa nguo, tena ana akili zake, wakashikwa na woga.
16Nao walioyaona wakawasimulia, ya mwenye pepo yalivyoendelea, hata yale ya nguruwe.
17Wakaanza kumbembeleza, atoke mipakani kwao.
18Alipojipakia chomboni, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akambembeleza, afuatane pamoja naye.
19Lakini hakumwitikia, ila akamwambia: Uende zako nyumbani mwako kwa ndugu zako ukawasimulie yote, Bwana aliyokutendea kwa kukuhurumia!
20Ndipo, alipokwenda zake, akaanza kuyatangaza katika ile Miji Kumi yote, Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.[#Mar. 7:31.]
21Yesu alipokwisha vuka tena chomboni kuja ng'ambo, kundi la watu wengi likakusanyika hapo, alipokuwa kandokando ya bahari.
(22-43: Mat. 9:18-26; Luk. 8:41-56.)22Akaja mmoja wao majumbe wa nyumba ya kuombea, jina lake Yairo; alipomwona akamwangukia miguuni pake,
23akambembeleza sana akisema: Kibinti changu yumo kufani; nakuomba, uje, umbandikie mikono, apate kupona na kuwa mzima tena.[#Mar. 7:32.]
24Akaondoka, akaenda naye; watu wengi sana wakamfuata wakimsongasonga.
25Kukawa na mwanamke mwenye ugonjwa wa kutoka damu miaka 12.
26Huyo alikuwa amepata maumivu mengi kwa waganga wengi; hivyo alizimaliza mali zake zote, lakini hawakumfaa hata kidogo, ugonjwa wake ukakaza tu kuwa mbaya.
27Alipoyasikia mambo ya Yesu akaliingia kundi la watu, akamjia nyuma, akaigusa nguo yake.
28Maana alisema: Hata nikizigusa nguo zake tu nitapona.
29Papo hapo kijitojito cha damu yake kikakauka, akajiona mwilini, ya kuwa amelipona teso lake.
30Papo hapo Yesu akatambua mwilini mwake, ya kuwa nguvu imemtoka; akaligeukia kundi la watu, akasema: Yuko nani aliyenigusa nguo zangu?[#Luk. 6:19.]
31Wanafunzi wake wakamwambia: Unaliona kundi la watu, linakusongasonga, nawe unauliza: Yuko nani aliyenigusa?
32Alipotazama huko na huko, apate kumwona aliyemgusa,
33yule mwanamke akashikwa na woga, akatetemeka, kwani alijua lililompata; kwa hiyo akaja, akamwangukia, akamwambia yote, yalivyokuwa kweli.
34Naye akamwambia: Mwanangu, kunitegemea kwako kumekuponya, nenda na kutengemana, uwe mzima, teso lako lisikurudie tena!
35Angali akisema, wakaja watu wa jumbe wa nyumba ya kuombea, wakasema: Binti yako amekwisha kufa; mfunzi unamsumbulia nini tena?
36Yesu alipoyasikia maneno haya, yakisemwa, akamwambia jumbe wa nyumba ya kuombea: Usiogope, nitegemea tu!
37kisha hakumpa mtu mwingine ruhusa kufuatana naye, ila Petero na Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo.
38Walipoingia nyumbani mwa jumbe wa nyumba ya kuombea, akaona makelele ya watu, wakilia na kuomboleza sana.
39Akaingia, akawaambia: Mnapigia nini makelele na kulia? Kitoto hakufa, ila amelala usingizi tu;[#Yoh. 11:11.]
40ndipo, walipomcheka sana. Lakini alipokwisha kuwafukuza wote akamchukua baba ya kitoto na mama yake na wale waliokuwa pamoja naye, akaingia mle, yule kitoto alimokuwa.
41Akamshika kitoto mkono, akamwambia: Talita kumi! ni kwamba: Kijana, nakuambia: Inuka![#Luk. 7:14.]
42Papo hapo kijana akafufuka, akaendaenda, kwani alikuwa wa miaka 12. Ndipo, waliposhangaa ushangao mwingi.
43Akawakataza sana, wasilitambulishe neno hili kwa mtu ye yote; kisha akasema, kijana apewe chakula.[#Mar. 1:44.]