Marko 6

Marko 6

Yesu mjini mwa Nasareti.

(1-6: Mat. 13:53-58; Luk. 4:15-30.)

1Akatoka kule, akaenda kwao, alikokulia, nao wanafunzi wake wakamfuata.

2Ilipokuwa siku ya mapumziko, akaanza kufundisha katika nyumba ya kuombea, nao wengi waliomsikia wakashangaa, wakasema: Huyu haya ameyapata wapi? Werevu huu ulio wa kweli amepewa na nani? Hizo nguvu nazo zinazotendwa na mikono yake ni nguvu gani?[#Yoh. 7:15.]

3Huyu si seremala, mwana wa Maria? Huyu si ndugu yao Yakobo na Yose na Yuda na Simoni? Nao maumbu zake hawako huku kwetu? Wakajikwaa kwake.

4Yesu akawaambia: Mfumbuaji habezwi, isipokuwa kwao, alikokulia, na kwa ndugu zake namo nyumbani mwake.

5Kwa hiyo hakuweza kufanya kule la nguvu hata moja, ila wanyonge wachache akawabandikia mikono, akawaponya.[#Mar. 6:13.]

6Akastaajabu, jinsi walivyokataa kumtegemea.

Kuwatuma mitume.

(7-13: Mat. 10:1,9-15; Luk. 9:1-6.)

7Akaenda akizunguka katika vijiji vya pembenipembeni na kufundisha watu. Akawaita wale kumi na wawili, akaanza kuwatuma wawiliwawili, akawapa nguvu za kufukuza pepo wachafu.[#Luk. 10:1.]

8Akawaagiza, washike fimbo tu, wasichukue kingine cha njiani, wala chakula wala mkoba wala senti mishipini.

9Mwende mmevaa viatu, lakini msivae nguo mbili!

10Akawaambia: Kila mtakamoingia nyumbani, kaeni mwake, mpaka mtakapotoka tena!

11Napo mahali, wasipowapokea, wasiwasikilize, basi, tokeni pale na kuyakung'uta mavumbi yaliyoishika miguu yenu, yaje yanishuhudie kwao!

12Kisha wakatoka, wakaenda na kutangaza, watu wajute.

13Wakafukuza pepo wengi, wakapaka wanyonge wengi mafuta, wakawaponya.[#Yak. 5:14-15.]

Kufa kwa Yohana.

(14-29: Mat. 14:1-2; Luk. 3:19-20; 9:7-9.)

14Mfalme Herode akayasikia, kwani Jina lake lilivuma, maana watu walisema: Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, kwa sababu hii nguvu hizo humtendesha kazi.

15Lakini wengine walisema: Ndiye Elia; wengine tena walisema: Ni mfumbuaji kama wale wafumbuaji wenzake.

16Lakini Herode alipoyasikia akasema: Ndiye Yohana, niliyemkata kichwa mimi, huyo amefufuka.

17Kwani Herode mwenyewe alikuwa ametuma kumkamata Yohana na kumfunga kifungoni kwa ajili ya Herodia, mke wa nduguye, Filipo, ambaye alikuwa amemwoa.

18Kwani Yohana alimwambia Herode: Ni mwiko kwako kuwa na mke wa nduguyo.[#3 Mose 18:16.]

19Lakini Herodia alimvizia, akataka kumwua, asiweze.

20Kwani Herode alimwogopa Yohana, kwa vile, alivyomjua kuwa mtu mwongofu na mtakatifu, akamshika na kumlinda. Naye alipomsikia mara kwa mara akahangaishwa sana moyoni, tena akapendezwa kumsikiliza.

21Siku iliyofaa ya kumpata ilikuwa sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode; ndipo, alipowaalika chakulani watawala miji yake na wakubwa wa askari na watu wenye cheo wa Galilea.

22Binti Herodia alipoingia na kucheza ngoma, akampendeza Herode na wale waliokaa pamoja naye chakulani. Ndipo, mfalme alipomwambia huyo msichana:

23Niombe kila, utakacho! nitakupa; kisha akamwapia: Cho chote, utakachoniomba, nitakupa, ijapo iwe nusu ya ufalme wangu.[#Est. 5:3,6.]

24Yule akatoka, akamwuliza mama yake: Niombe nini? Naye akasema: Kichwa chake Yohana Mbatizaji!

25Papo hapo akaingia mbio kwa mfalme, akaomba akisema: Nataka, unipe sasa hivi katika chano kichwa chake Yohana Mbatizaji.

26Mfalme akasikitika sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake na kwa ajili ya wale waliokaa chakulani hakutaka kumnyima.

27Ndipo, mfalme alipotuma askari, akamwagiza, akilete kile kichwa chake.

28Yule akaenda, akamkata kichwa chake mle kifungoni, kisha akakileta katika chano, akampa msichana, naye msichana akampa mama yake.

29Wanafunzi wake walipoyasikia wakaja, wakautwaa mwili wake, wakauweka kaburini.

Kurudi kwao mitume.

30Nao mitume wakakusanyika kwa Yesu, wakamsimulia mambo yote, waliyoyafanya nayo waliyoyafundisha.[#Luk. 9:10; 10:17.]

31Akawaambia: Njoni ninyi peke yenu, twende mahali pasipo na watu, mpumzike kidogo! Kwani watu wengi walikuwa wakija, tena wakienda, wasipate hata kula.

(32-44: Mat. 14:13-21; Luk. 9:11-17; Yoh. 6:1-13.)

32Wakaondoka, wakaenda chomboni peke yao mahali palipokuwa pasipo watu.

33Watu walipowaona, wakitoka, nao wengi walipotambua, wanapokwenda, wakatoka miji yote kwa miguu, wakapiga mbio kuwakuta palepale, wakatangulia kufika.

34Alipotoka chomboni akaona, watu ni wengi sana, akawaonea uchungu, kwani walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji, akaanza kuwafundisha mengi.[#Mat. 9:36; 4 Mose 27:17; Ez. 34:5.]

Kulisha watu 5000.

35Saa zilipofika za jioni, wanafunzi wake wakamjia, wakasema: Hapa tulipo ni nyika, nazo saa zimefika za jioni.[#Mar. 8:1-9.]

36Uwaage watu, waende zao mashambani na vijijini huko pembenipembeni, wajinunulie vyakula!

37Lakini akawajibu akiwaambia: Wapeni ninyi vyakula! Wakamwambia: Twende, tununue mikate ya shilingi 200, tuwape, wale?

38Akawauliza: Mnayo mikate mingapi? Haya! Nendeni, mtazame! Walipoijua wakasema: Mitano, tena visamaki viwili.

39Akawaagiza wote, wakae mafungumafungu uwandani penye majani.

40Wakakaa kikao kwa kikao, pengine mia, pengine hamsini.

41Akaitwaa ile mikate mitano na vile visamaki viwili, akatazama juu mbinguni, akaviombea, akawamegeamegea ile mikate, akawapa wanafunzi, wawapangie; navyo vile visamaki viwili akawagawia wote.[#Mar. 7:34.]

42Wakala wote, wakashiba.

43Kisha wakaokota makombo ya mikate wakajaza vikapu kumi na viwili pamoja na vipande vya samaki.[#5 Mose 28:5.]

44Nao waliokula ile mikate walikuwa 5000 waume tu.

Kwenda juu ya bahari.

(45-56: Mat. 14:22-36; Yoh. 6:15-21.)

45Papo hapo akawashurutisha wanafunzi wake, waingie chomboni, wamtangulie kwenda ng'ambo huko Beti-Saida, mpaka yeye kwanza aliage kundi la watu.

46Naye alipokwisha kuwaaga akaondoka kwenda mlimani kuomba.

47Jua lilipokwisha kuchwa, chombo kilikuwa katikati ya bahari, naye mwenyewe alikuwa peke yake pwani.

48Akawaona, wakihangaishwa, wasiweze kwendelea, kwani upepo uliwatokea mbele. Ilipofika zamu ya nne ya usiku, akawajia akienda juu ya bahari, akataka kuwapita.

49Nao walipomwona, anavyokwenda juu ya bahari, wakawaza kuwa ni mzimu, wakapiga makelele,

50kwani wote walimwona, wakatetemeka. Papo hapo yeye akasema nao akawaambia: Tulieni! Ni miye, msiogope!

51Alipowapandia chomboni, upepo ukakoma. Ndipo, walipostuka na kushangaa mno mioyoni mwao;[#Mar. 4:39.]

52kwani hawajaelewa maana ya ile mikate, mioyo yao nayo ilikuwa imeshupaa.

53Walipokwisha vuka wakafika nchini kwa Genesareti, wakatia nanga hapo.

54Nao walipotoka chomboni, papo hapo watu wakamtambua;

55wakaenda mbio wakiizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani waliokuwa hawawezi, wakaenda nao huko na huko, walikomsikia, ya kuwa yeye yuko.

56Kila alipoingia katika vijiji au miji au mashamba waliwaweka wagonjwa sokoni, wakambembeleza, wamguse pindo la lanzu yake tu; nao wote walioligusa wakapona.[#Mar. 5:27-28; Tume. 5:15; 19:11-12.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania