The chat will start when you send the first message.
1Siku zile likakusanyika tena kundi la watu wengi; walipokosa vyakula, akawaita wanafunzi, akawaambia:
2Kundi hili la watu nalionea uchungu, kwa kuwa wameshinda kwangu siku tatu, wasione chakula.[#Mar. 6:34-44.]
3Kama ninawaaga, waende nyumbani kwao pasipo kula, watazimia njiani; tena wako waliotoka mbali.
4Wanafunzi wake walipomjibu: Hapa nyikani mtu atawezaje kuwashibisha watu hawa mikate?
5akawauliza: Mnayo mikate mingapi? Nao waliposema: Saba,
6akawaagiza hao watu wengi, wakae chini, kisha akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake, wawapangie; nao wakawapangia wao wa hilo kundi la watu.
7Tena walikuwa na visamaki vichache; navyo akaviombea, akasema, wawapangie hivi navyo.
8Wakala, wakashiba; kisha wakaokota makombo ya mikate yaliyosalia, yakawa makanda saba.[#5 Mose 28:5.]
9Nao walikuwa kama 4000. Kisha akawaaga, waende zao.
10Papo hapo akaingia chomboni pamoja na wanafunzi wake, akaja upande wa Dalmanuta.
11Wakamtokea Mafariseo, wakanza kubisha naye, wakamjaribu wakitaka, afanye kielekezo kitokacho mbinguni.[#Yoh. 6:30.]
12Akapiga kite rohoni mwake, akasema: Mbona wao wa ukoo huu wanataka kielekezo? Kweli nawaambiani: Wao wa ukoo huu hawatapata kielekezo.
13Kisha akawaacha, akajipakia tena chomboni, akaenda zake ng'ambo.
14Walikuwa wamesahau kuchukua mikate; namo chomboni hawakuwa na mikate ila mmoja tu.
15Akawaonya akisema: Tazameni, jiangalieni kwa ajili ya chachu ya Mafariseo na chachu ya Herode![#Mar. 3:6; Luk. 12:1; 13:32.]
16Ndipo, walipoyafikiri na kusemezana wao kwa wao: Ni kwa sababu hatunayo mikate.
17Kwa kuwatambua akawaambia: Mbona mnafikiri hivyo, ya kuwa hamnayo mikate? Hamjaerevuka bado? Wala hamjajua maana? Mngaliko wenye mioyo iliyoshupaa?[#Mar. 6:52.]
18Macho mnayo, lakini hamwoni? Nayo masikio mnayo, lakini hamsikii?[#Yer. 5:21; Ez. 12:2.]
19Wala hamwikumbuki ile mikate mitano, nilipoimegea wale 5000? Hapo mlijaza makapo mangapi mkiokota makombo? Wakamwambia: Kumi na mawili.[#Mar. 6:41-44.]
20Wala hamwikumbuki ile mikate saba, nilipoivunjia wale 4000, mlijaza makanda mangapi mkiokota makombo? Wakamwambia: Saba.[#Mar. 8:6-9.]
21Akawauliza: Hamjajua bado maana?
22Walipoingia Beti-Saida, wakamletea kipofu, wakambembeleza, amguse.[#Mar. 6:56.]
23Akaushika mkono wa kipofu, akamwongoza, watoke kijijini, akamtemea mate machoni, akambandikia mikono, akamwuliza: Kiko, unachokiona?[#Mar. 7:32-33; Yoh. 9:6.]
24Yule akainua macho, akasema: Naona watu wanaotembea, wanaonekana kuwa kama miti.
25Hapo akambandikia mikono tena machoni pake, akamwagiza kutazama tena; ndipo, macho yake yaliporudia kuwa mazima, akaona vitu vyote waziwazi, hata vilivyoko mbali.
26Kisha akamtuma, aende nyumbani mwake, akisema: Kijijini usimwingie! Wala usimwambie mtu wa humu kijijini![#Mar. 7:36.]
27Yesu na wanafunzi wake wakatoka, waingie vijiji vya upande wa Kesaria-Filipi. Walipokuwa njiani, akawauliza wanafunzi wake akiwaambia: Watu hunisema kuwa ni nani?
28Nao wakamwambia wakisema: Wanakusema kuwa u Yohana Mbatizaji, wengine: Elia, wengine: Mmoja wao wafumbuaji.[#Mar. 6:15.]
29Kisha akawauliza: Lakini ninyi mnanisema kuwa ni nani? Petero akajibu akimwambia: Wewe ndiwe Kristo.
30Ndipo, alipowatisha, wasimwambie mtu hilo neno lake.[#Mar. 9:9.]
31Akaanza kuwafundisha, ya kuwa imempasa Mwana wa mtu kuteswa mengi na kukataliwa nao wazee na watambikaji wakuu na waandishi, mpaka auawe, kisha afufuke, siku tatu zitakapopita.
32Neno hili akalisema waziwazi. Ndipo, Petero alipomchukua pembeni, akaanza kumtisha.
33Naye akageuka nyuma, akawatazama wanafunzi wake, akamtisha Petero akisema: Niondokea hapa nyuma yangu, wewe Satani! Kwani wewe huyawazi mambo ya Kimungu, ila unayawaza ya kiwatu tu.
34Akaliita kundi la watu, limjie pamoja na wanafunzi wake, akawaambia: Mtu akitaka kunifuata mimi ajikataze mapenzi yake, ajitwishe nao msalaba wake, kisha anifuate!
35Maana mtu anayetaka kuiokoa roho yake ataiangamiza. Lakini mtu atakayeiangamiza roho yake kwa ajili yangu mimi na kwa ajili ya Utume mwema ataiokoa.[#Mat. 10:39.]
36Kwani mtu vinamfaa nini kuvichuma vya ulimwengu wote, roho yake ikiponzwa navyo?
37Kwani mtu atoe nini, aikomboe roho yake?
38Kwani mtu atakayenionea soni mimi na maneno yangu kwao wa kizazi hiki kilicho chenye ugoni na ukosaji, basi, naye Mwana wa mtu atamwonea soni huyo atakapokuja mwenye utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.[#Mat. 10:33.]