Marko 9

Marko 9

1Akawaambia: Kweli nawaambiani: Miongoni mwao wanaosimama hapa wamo wengine, ambao hawatakuonja kufa, mpaka watakapouona ufalme wa Mungu, ukiisha kuja kwa nguvu.

Yesu anageuzwa sura.

(2-13: Mat. 17:1-13; Luk. 9:28-36.)

2Baada ya siku sita Yesu akamchukua Petero na Yakobo na Yohana, akapanda pamoja nao peke yao pasipo watu wengine juu ya mlima mrefu. Huko akageuzwa sura yake machoni pao,

3nazo nguo zake zikawa nyeupe sana, zikamerimeta; nchini hakuna fundi anayeweza kuzing'aza hivyo.

4Wakatokewa na Elia pamoja na Mose, wakawa wakiongea na Yesu.

5Petero akasema akimwambia Yesu: Mfunzi mkuu, hapa ni pazuri kuwapo sisi, na tujenge vibanda vitatu, kimoja chako, na kimoja cha Mose, na kimoja cha Elia!

6Kwani hakujua, alilolisema, kwa maana waliingiwa na woga mkubwa.

7Kisha hapo pakawa na wingu, likawatia kivuli, sauti ikatoka winguni kwamba: Huyu ndiye mwanangu mpendwa, msikilizeni yeye![#Mar. 1:11; 5 Mose 8:15; Tume. 3:22; 2 Petr. 1:17.]

8Mara walipotazama huko na huko, hakuna waliyemwona, asipokuwa Yesu peke yake pamoja nao.

Kuja kwa Elia.

9Walipokuwa wakishuka mlimani, akawakataza, wasimsimulie mtu ye yote, waliyoyaona, isipokuwa hapo, Mwana wa mtu atakapokwisha kufufuka katika wafu.[#Mar. 8:30.]

10Wakalishika neno hili wakiulizana wao kwa wao: Huko kufufuka katika wafu maana yake nini?

11Wakamwuliza wakisema: Waandishi husemaje: Sharti kwanza Elia aje?

12Akawaambia: Kweli, Elia anakuja kwanza, vyote avigeuze kuwa vipya. Kisha Mwana wa mtu ameandikiwaje, ya kuwa atateswa mengi na kubezwa?[#Yes. 53:3; Mal. 4:5.]

13Lakini nawaambiani: Elia amekwisha kuja, wakamtendea yote, waliyoyataka, kama alivyoandikiwa.[#1 Fal. 19:2-10; Mat. 11:14.]

Kijana mwenye pepo.

(14-29: Mat. 17:14-21; Luk. 9:37-42.)

14Walipokuja kwa wanafunzi wakaona kundi la watu wengi lililowazunguka, hata waandishi walikuwapo wakibishana nao.

15Papo hapo kundi lote lilipomwona yeye, wakastuka, wakamwendea mbio, wakamwamkia.

16Akawauliza: Mnabishana nini nao?

17Mmoja wao wale watu wengi akamjibu: Mfunzi, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo wa ububu.

18Napo pote anapomkamata anamsukumasukuma kwa nguvu, naye hutoka pofu na kukereza meno, kisha mwili wake hunyauka. Nami nikawaambia wanafunzi wako, wamfukuze huyo pepo, lakini hawakuweza.

19Naye akawajibu akisema: Enyi wa kizazi kisichomtegemea Mungu! Nitakuwapo nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni hapa, nilipo!

20Wakampeleka kwake; naye alipomwona, mara pepo akamkumba, akaanguka chini, akafingirika na kutoka pofu.

21Akamwuliza baba yake: Hivyo vimempata tangu lini? Akasema: Tangu utoto wake;

22mara nyingi humtupa motoni na majini, maana amwue. Lakini ukiweza kitu tusaidie ukituonea uchungu!

23Yesu akamwambia: Ukiweza kumtegemea Mungu! Yote huwezekana kwake anayemtegemea Mungu.[#Mar. 11:23.]

24Papo hapo baba wa kijana akapaza sauti akisema: Namtegemea Mungu; nisaidie, nisipomtegemea![#Luk. 17:5.]

25Yesu alipoona, watu wengi wanavyomkusanyikia mbiombio, akamkaripia yule pepo mchafu akimwambia: Wee pepo uliye bubu na kiziwi, mimi nakuagiza, umtoke huyu, usimwingie tena!

26Ndipo, alipolia, akamsukumasukuma kwa nguvu, akamtoka; naye akawa kama mfu, hata wengi wakasema: Amekufa.[#Mar. 1:26.]

27Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua; ndipo, aliposimama.

28Naye alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza walipokuwa peke yao: Mbona sisi hatukuweza kumfukuza huyo?

29Akawaambia: Pepo walio hivyo hawawezi kutoka, isipokuwa kwa nguvu ya kuomba na ya kufunga.

Ufunuo wa pili wa mateso.

(30-32: Mat. 17:22-23; Luk. 9:43-45.)

30Wakatoka kule, wakatembea huko katikati ya Galilea; naye hakutaka, mtu akivitambua.[#Yoh. 7:1.]

31Kwani alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake na kuwaambia: Mwana wa mtu atatiwa mikononi mwa watu, nao watamwua; lakini akiisha kuuawa, siku zitakapopita tatu, atafufuka.[#Mar. 8:31; 10:32-34.]

32Nao hawakulitambua neno hili, lakini wakaogopa kumwuliza.[#Luk. 18:34.]

Ukubwa.

(33-50: Mat. 18,1-9; Luk. 9,46-50.)

33Wakafika Kapernaumu. Alipokuwa nyumbani akawauliza: Njiani mlibishana nini?[#Mat. 17:24.]

34Wakanyamaza; maana walikuwa wameshindana njiani wao kwa wao kwamba: Aliye mkuu ni nani?

35Akakaa, akawaita wale kumi na wawili, akawaambia: Mtu akitaka kuwa wa kwanza, sharti awafuate wenzake wote nyuma, awe mtumishi wao wote![#Mar. 10:16.]

36Kisha akatwaa kitoto, akamsimamisha katikati yao, akamkumbatia, akawaambia:

37Mtu atakayepokea kitoto mmoja aliye kama huyu kwa Jina languhunipokea mimi. Tena mtu akinipokea mimi hanipokei mimi, ila humpokea yule aliyenituma.[#Mat. 10:40; Yoh. 13:20.]

38Yohana akamwambia: Mfunzi, tuliona mtu anayefukuza pepo kwa Jina lako, lakini hafuatani nasi; tukamzuia, kwani hakufuatana nasi.[#1 Kor. 12:3.]

39Yesu akasema: Msimzuie! Kwani hakuna mwenye kufanya cha nguvu kwa ajina langua atakayeweza kipunde kidogo kunisema vibaya.

40Kwani asiyetukataa yuko upande wetu.[#Mat. 12:30.]

41Kwani atakayewanywesha ninyi kinyweo cha maji tu, kwa sababu m wa Kristo, kweli nawaambiani Mshahara wake hautampotea kamwe.[#Mat. 10:42.]

42Lakini mtu atakayekwaza mmoja tu aliye mwenzao hawa wadogo wanaonitegemea, itamwia vizuri zaidi, akitundikwa shingoni pake jiwe kubwa la kusagia, kisha atumbukizwe baharini.

43Nawe, mkono wako ukikukwaza, uukate! Kuingia penye uzima mwenye kilema kutakufaa kuliko hapo, ukiwa mwenye mikono miwili, ukajiendea kuzimuni penye moto usiozimika.[#Mat. 5:30.]

44Hapo ndipo, mdudu mwenye kuwaumiza asipokufa, tena ndipo, pasipozimika moto.[#Yes. 66:24.]

45Nawe, mguu wako ukikukwaza, uukate! Kuingia penye uzima, ukiwa kiwete, kutakufaa kuliko hapo, ukiwa mwenye miguu miwili, ukatupwa shimoni mwa moto.

46Hapo ndipo, mdudu mwenye kuwaumiza asipokufa, tena ndipo pasipozimika moto.[#Mar. 9:44.]

47Nalo jicho lako likikukwaza, basi, ling'oe, ulitupe mbali! Kuuingia ufalme wa Mungu mwenye chongo kutakufaa kuliko hapo, ukiwa mwenye macho mawili ukatupwa shimoni mwa moto.[#Mat. 5:29.]

48Hapo ndipo, mdudu mwenye kuwaumiza asipokufa, tena ndipo, pasipozimika moto.[#Mar. 9:44,46.]

49Kwani chumvi ya kumkoleza mtu ye yote ni moto.[#3 Mose 2:13.]

50Chumvi ni nzuri; lakini chumvi ikiwa imepotewa na ukolezi, mtaitia kitu gani, ipate kukolea tena? Mwe na chumvi mioyoni mwenu! Tena mwendeane kwa utengemano![#Mat. 5:13; Luk. 14:34; Kol. 4:6.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania