Nahumu 3

Nahumu 3

Makosa na mapatilizo ya Niniwe.

1Yataupata huo mji wenye damu!

Wote mzima umejaa uwongo na ukorofi! Haukuacha kupokonya.

2Na wasikie uvumi wa mijeledi

na vishindo vya magurudumu yatutumuayo

na vya farasi wapigao mbio na vya magari yarukayo!

3Wapandao farasi watakuja mbiombio

wenye panga ziwakazo moto na wenye mikuki imerimetayo kama umeme.

Ndipo, watakapouawa wengi, mizoga iwe chungu zima,

watu wakwazwe na mizoga.

4Hayo ndiyo malipo ya uzinzi mwingi wa huyo mzinzi mke

aliye mzuri wa kupendeza,

aliyenasa kwa uganga wake,

aliyeteka makabila mazima kwa uzinzi wake

na milango ya watu kwa uganga wake.

5Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi:

Utaniona, nikikujia, nizifunue nguo zako ndefu

nikizipandisha mpaka usoni kwako,

nionyeshe mataifa uchi wako,

nao walio wa kifalme niwaonyeshe yako yenye soni.

6Nitakutupia yatapishayo, nikutie soni;

nitakuweka kuwa kitisho chao watakaokutazama.

7Ndipo, kila atakayekuona atapokukimbia na kusema:

Kumbe Niniwe umebomolewa! Yuko nani atakayeombolezea?

Nitatafuta wapi watakaokutuliza moyo?

8Je? U mwema kuliko No wa Amoni

uliokaa majitoni huko Misri, uliozungukwa na maji?

Boma lake ulikuwa wingi wa maji,

nao ukuta wa nje wa boma ulikuwa wingi wa maji.

9Ulipata nguvu kule kwa Wanubi

nako kwa Wamisri wasiohesabika,

Waputi na Walubi walikuwa tayari kuusaidia.

10Nao umetekwa na kuhamishwa utumwani,

nao watoto wake wachanga wakapondwa vichwa

po pote pembeni barabarani;

waliokuwa wenye utukufu wakapigiwa kura,

nao wakuu wake wote wakafungwa minyororo.

11Wewe nawe na uleweshwe, uwe kama mtu azimiaye roho,

wewe nawe na ujitafutie ngome ya kukimbilia adui.

12Maboma yako yote inafanana na mikuyu yenye kuyu za

kwanza,

mtu akiitikisa, zitaangukia kinywani mwake anayetaka

kuzila.

13Waume wako, ulio nao mwako, utawaona kuwa kama wanawake,

nayo malango ya nchi yako yatakuwa yamefunguka,

yawe wazi mbele ya adui zako,

nao moto utayala makomeo yako.

14Jichotee maji kuwa nayo siku za kusongwa,

kayatengeneze maboma yako, yapate nguvu!

Ukiisha kuuponda mchanga, ukanyage udongo,

nayo tanuru ya kuchomea matofali itengeneze, ipate nguvu!

15Lakini patakapotimia, moto utakula,

nazo panga zitakuangamiza zikikula kama funutu,

ingawa mwe wengi kama funutu, ingawa mwe wengi kama nzige.

16Wachuuzi wako walikuwa wengi kuliko nyota za mbinguni,

wakawa kama funutu: wakigeuka kuwa nzige, huruka kwenda

zao.

17Wakuu wako wa serikali wanafanana na nzige,

nao wakuu wako wa askari wanafanana na makundi ya nyenze:

siku za baridi huja kulala kutani,

lakini jua likitoka, hujiendea kwa kuruka,

tena mahali, walipokwenda, hapajulikani.

18Wachungaji wako, mfalme wa Asuri, wamelala,

watukufu wako wamelala usingizi.

Watu wako wametawanyika milimani juu,

tena hakuna anayewakusanya.

19Donda lako haliwezekani,

pigo lililokupiga haliponi kabisa.

Wote wazisikiao habari zako watakupigia makofi,

kwani yuko nani, ambaye ubaya wako haukumpata siku zote?

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania