The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:[#4 Mose 25:17; 27:13.]
2Walipizie wana wa Isiraeli kwa Wamidiani! Kisha utachukuliwa kwenda kwao walio ukoo wako.
3Ndipo, Mose alipowaambia watu kwamba: Tengenezeni watu wa kwenu kwenda vitani, wawaendee Wamidiani kumpatia Bwana lipizo kwao Wamidiani!
4Kwao mashina ya Waisiraeli kila shina moja litoe watu elfu moja na kuwatuama kwenda vitani.
5Kwa hiyo wakatolewa katika maelfu ya Waisiraeli elfu moja katika kila shina, wakawa watu maelfu kumi na mawili waliotengenezwa kwenda vitani.
6Hayo maelfu, elfu moja la kila shina, Mose akawatuma kwenda vitani pamoja na Pinehasi, mwana wa mtambikaji Elazari; huyu alishika mkononi mwake vyombo vya Patakatifu nayo yale matarumbeta ya shangwe.[#4 Mose 10:2; 25:7.]
7Wakaenda vitani kupigana na adui, kama Bwana alivyomwagiza Mose, wakawaua wa kiume wote.[#5 Mose 20:13.]
8Nao wafalme wa Wamidiani wakawaua pamoja na watu wao waliouawa: Ewi na Rekemu na Suri na Huri na Reba; hao watano ndio waliokuwa wafalme wao Wamidiani. Naye Bileamu, mwana wa Beori, wakamwua kwa upanga.[#4 Mose 22:5; Yos. 13:21-22.]
9Kisha wana wa Isiraeli wakawateka wanawake wa Midiani na watoto wao, nao ng'ombe wao wote na mbuzi na kondoo wao wote na mali zao zote pia wakazichukua kuwa nyara zao.
10Lakini miji yao yote, walimokaa, na makambi yenye mahema yao wakayateketeza kwa moto.
11Kisha wakawachukua nyama wote na mateka yote, watu pamoja na nyama,
12wote pia wakawapeleka kwa Mose na kwa mtambikaji Elazari na kwao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli; mateka na mapato ndiyo, waliyoyapeleka pamoja na nyara makambini kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani; ndipo hapo, Yeriko ulipokuwa ng'ambo ya pili.
13Ndipo, Mose na mtambikaji Elazari na wakuu wote wa mkutano walipotoka kwenda kukutana nao huko nje ya makambi.
14Lakini Mose akawakasirikia waliowekwa kuvisimamia vikosi, wale wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia waliotoka kwa kupiga vita;
15kwa hiyo Mose akawaambia: Kumbe mmewaponya wanawake wote!
16Nao ndio walioongozwa na Bileamu, wakawakosesha wana wa Isiraeli, wamvunjie Bwana maagano kwa ajili ya Peori, nao wa mkutano wa Bwana wakapatwa na pigo kwa sababu hiyo.[#4 Mose 15:1; Ufu. 2:14.]
17Sasa waueni watoto wa kiume wote! Nao wanawake wote wanaojua waume kwa kulala nao wa kiume waueni nao!
18Lakini watoto wa kike wote wasiojua bado kulala nao wa kiume waponyeni, wakae kwenu!
19Kisha ninyi laleni nje ya makambi siku saba, ninyi nyote mlioua mtu nanyi mliogusa tu mtu aliyeuawa, mjieue siku ya tatu na siku ya saba, ninyi wenyewe pamoja na mateka yenu.[#4 Mose 19:11.]
20Nazo nguo zote navyo vyombo vyote vya ngozi navyo vyote vilivyotengenezwa kwa manyoya ya singa za mbuzi navyo vyombo vyote vya mti sharti mvieue.
21Naye mtambikaji Elazari akawaambia askari waliotoka kwa kupiga vita: Haya ndiyo maongozi ya maonyo, Bwana aliyomwagiza Mose:
22vilivyo dhahabu na fedha na shaba na vyuma na mabati na risasi,
23navyo vyote vinavyoweza kuingia motoni sharti mvipitishe motoni, vipate kutakata, kisha mvieue kwa yale maji ya kunyunyiza; lakini vyote visivyopatana na moto na mvipitishe majini.
24Kisha sharti mzifue nguo zenu siku ya saba; ndipo, mtakapokuwa wenye kutakata, baadaye mtaingia makambini.
25Bwana akamwambia Mose kwamba:
26Toa jumla yao mateka, waliyoyapata ya watu na ya nyama, wewe pamoja na mtambikaji Elazari nao wakuu wa milango ya mkutano!
27Kisha hayo mapato uyatoe mafungu mawili, moja liwe lao walioshika kazi ya mapigano na kwenda vitani, la pili liwe lao wengine wote wa mkutano.[#Yos. 22:8; 1 Sam. 30:24.]
28Kisha wao waliokwenda kupiga vita uwatoze toleo limpasalo Bwana: kwa kila mia tano mmoja, kama ni watu au ng'ombe au punda au mbuzi au kondoo.
29Hivyo ndivyo, utakavyowatoza katika nusu yao, umpe mtambikaji Elazari kuwa vipaji vya tambiko vya kumnyanyulia Bwana.
30Lakini katika nusu yao wana wa Isiraeli uchukue mmoja na kumtoa katika kila hamsini, kama ni watu au ng'ombe au punda au mbuzi au kondoo; katika nyama wote utoe hivyo, uwape Walawi wanaongoja zamu ya kuliangalia Kao la Bwana.
31Ndipo, Mose na mtambikaji Elazari walipofanya, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
32Masao ya nyara, watu wa vita walizozichukua, mapato hayo yalikuwa mbuzi na kondoo pamoja 675000,
33na ng'ombe 72000,
34na punda 61000.
35Nao wana wa kike wasiojua bado kulala na mtu wa kiume wote pamoja walikuwa 32000.
36kwa hiyo ile nusu iliyokuwa fungu lao waliokwenda vitani, hesabu ya mbuzi na kondoo ilikuwa 337500.
37Nalo toleo lililompasa Bwana la hao mbuzi na kondoo lilikuwa 675.
38Nao ng'ombe wao walkuwa 36000, nalo toleo lao lililompasa Bwana lilikuwa ng'ombe 72.
39Nao punda walikuwa 30500, nalo toleo lao lililompasa Bwana lilikuwa 61.
40Nao watu wao walikuwa 16000, nalo toleo lao lililompasa Bwana lilikuwa watu 32.
41Hayo matoleo Mose akampa mtambikaji Elazari kuwa vipaji vya tambiko vya kumnyanyulia Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
42Nayo nusu nyingine ya wana wa Isiraeli, Mose aliyoiondoa kwao waliokwenda kuvipiga hivyo vita,
43hiyo nusu iliyokuwa yao wa mkutano ilikuwa nayo mbuzi na kondoo 337500,
44nao ng'ombe walikuwa 36000,
45nao punda walikuwa 30500,
46nao watu walikuwa 16000.
47Katika nusu hii ya wana wa Isiraeli Mose akachukua mmoja aliyetolewa katika kila hamsini, kama ni watu au nyama, akawapa Walawi waliongoja zamu ya kuliangalia Kao la Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
48Kisha waliowekwa kuyasimamia maelfu ya vikosi, wale wakuu wa maelfu na wa mamia wakamkaribia Mose,
49wakamwambia Mose: Sisi watumishi wako tumetoa jumla ya watu wa vita, tuliowashika mikononi mwetu, namo miongoni mwao hakukoseka hata mmoja.
50Kwa hiyo tunamtolea Bwana vyombo vya dhahabu, kila mtu alivyoviona kuwa matoleo: vikuku na vitimbi na pete za vidoleni na mapete ya masikioni na mapambo yo yote, tujipatie upozi mbele ya Bwana.
51Mose na mtambikaji Elazari wakachukua kwao hizo dhahabu zilizotengenezwa kuwa hivyo vyombo vyote.
52Nazo dhahabu zote, walizomtolea Bwana kuwa vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa zilikuwa frasila kumi na saba, ndizo zilizotoka kwa wakuu wa maelfu na kwa wakuu wa mamia.
53Nao waliokuwa askari tu walijichukulia kila mtu nyara zake.
54Mose na mtambikaji Elazari walipokwisha kuzichukua hizo dhahabu kwao wakuu wa maelfu na wa mamia wakazipeleka Hemani wa Mkutano, ziwe za kumkumbusha Bwana, asikoe kuwatazama wana wa Iiraeli.