4 Mose 35

4 Mose 35

Miji ya Walawi.

1Kwenye mbuga za Moabu ng'ambo ya huku ya Yordani, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili, Bwana akamwambia Mose kwamba:

2Waagize wana wa Isiraeli, wawape Walawi katika mafungu yao, watakayoyachukua, miji ya kukaa, nayo malisho yanayoizunguka hiyo miji mwape Walawi![#4 Mose 18:20; Yos. 21:2.]

3Hiyo miji iwe yao ya kukaa, nayo malisho yawe ya ng'ombe wao na ya mbuzi na ya kondoo wao na ya nyama wao wengine wote.

4Hayo malisho ya miji, mtakayowapa Walawi, upana wao kutoka penye boma la mji kwenda nje sharti uwe mikono elfu kuuzunguka mji.

5Kwa hiyo na mpime huko nje ya mji upande wa maawioni kwa jua mikono 2000, nao upande wa kusini mikono 2000, nao upande wa baharini mikono 2000, nao upande wa kaskazini mikono 2000; nao mji uwe katikati; hayo na yawe malisho yao penye miji yao.

6Katika hiyo miji, mtakayowapa Walawi, sharti mwape miji sita ya kuikimbilia; hiyo mwape kwamba: mwuaji apate kuikimbilia. Pasipo kuihesabu hiyo mwape miji 42.[#2 Mose 21:13; 5 Mose 4:41; 19:2,9; Yos. 20.]

7Hivyo miji yote, mtakayowapa Walawi, itakuwa 48, ndiyo hiyo miji yenyewe pamoja na malisho yao.

8Mtakapoitoa hiyo miji katika mafungu, wana wa Isiraeli watakayoyachukua, yawe yao, kwao walio wengi na mtoe mingi, nako kwao walio wachache na mtoe michache; kila shina na litoe kwa ukuu wa fungu lake, litakalolipata kuwa lake, liwagawie Walawi miji ya kwao.[#4 Mose 26:54.]

Miji ya kuikimbili.

9Bwana akamwambia Mose kwamba:

10Sema na wana wa Isiraeli, uwaambie: Hapo, mtakapouvuka Yordani na kuingia katika nchi ya Kanaani,

11jichagulieni miji itakayowafalia ninyi kuwa miji ya kuikimbilia, mwuaji apate kuikimbilia, kama hakumpiga mwenziwe na kumwua kwa kusudi.[#5 Mose 4:41-43.]

12Miji hiyo iwe kwenu ya kuikimbilia na kumkimbia mlipizi, mwuaji asife, mpaka asimamishwe mbele ya mkutano, ahukumiwe nao.

13Nayo miji, mtakayoitoa kuwa miji ya kuikimbilia, sharti iwe sita kwenu.

14Miji mitatu na mtoe ng'ambo ya huku ya Yordani, tena na mtoe miji mitatu katika nchi ya Kanaani, iwe miji ya kuikimbilia.

15Miji hiyo sita iwe ya kuikimbilia wana wa Isiraeli, nao wageni, nao watakaokaa kwao, wapate kuikimbilia wote wasioua mtu kwa kusudi.

16Lakini kama mtu amempiga mwenzake kwa chombo cha chuma, akafa, yule ni mwuaji, naye kwa kuwa ni mwuaji, hana budi kuuawa.

17Kama amempiga kwa jiwe, alilolishika, linaloweza kuua mtu, yule akafa, basi, ni mwuaji, naye kwa kuwa ni mwuaji, hana budi kuuawa.

18kama amempiga kwa chombo cha mti, alichokishika mkononi, kinachoweza kuua mtu, akafa, basi, ni mwuaji, naye kwa kuwa ni mwuaji, hana budi kuuawa.

19Mwenye kuilipiza hiyo damu na amwue mwuaji; hapo, atakapomkuta yeye, na amwue.

20Tena mtu akimkumba mwenzake kwa kumchukia, au akimtupia kitu kwa kumvizia, yule akafa,

21au akimpiga kwa mkono wake kwa uadui, yule akafa, basi, yule aliyempiga hana budi kuuawa, kwa kuwa ni mwuaji; naye mwenye kuilipiza hiyo damu na amwue huyo mwuaji hapo, atakapomkuta.

22Lakini kama amemkumba kwa mara moja tu pasipo kuvijua, isipokuwa kwa uadui, au kama amemtupia kitu cho chote pasipo kumvizia,

23au kama ameacha pasipo kumwona, jiwe lo lote linaloweza kumwua mtu limwangukie, naye yule akafa asipokuwa wala adui wake wala mwenye kumtakia baya,

24basi, wao wa mkutano watamwamulia yule aliyeua naye mwenye kuilipiza hiyo damu, wakiyafuata hayo maamuzi.

25Nao wa mkutano watamponya huyo aliyeua mikononi mwake mwenye kuilipiza hiyo damu, kisha wao wa mkutano na wamrudishe katika mji wa kuukimbilia, alimokimbilia, naye atakaa humo, mpaka atakapokufa mtambikaji mkuu, waliyempaka mafuta matakatifu.[#3 Mose 21:10.]

26lakini kama yule mwuaji atatoka mipakani mwa mji wa kuukimbilia, alimokimbilia,

27naye mwenye kuilipiza hiyo damu akamwona nje ya mipaka ya huo mji, alimokimbilia, basi, mwenye kuilipiza hiyo damu atamwua huyo mwuaji pasipo kukora manza za damu.

28Kwani ilimpasa kukaa mle mjini, alimokimbilia, mpaka mtambikaji mkuu atakapokufa. Mtambikaji mkuu atakapokwisha kufa, huyo mwuaji naye atarudi kwao kwenye fungu lake, alilolichukua, liwe lake.

29Haya sharti yawe kwenu maongozi ya maamuzi ya vizazi vyenu po pote, mtakapokaa.

30Kila atakayemwua mwenziwe sharti wamwue huyo mwuaji kwa ushahidi wao walioviona, lakini shahidi mmoja asitoshe wa kuua mtu.[#5 Mose 17:6; 19:5.]

31Tena msichukue makombozi ya mtu mwuaji aliyekora manza za kufa, hana budi kuuawa.

32Wala msichukue makombozi ya mtu aliyekimbilia mji wa kuukimbilia, kwamba apate kurudi na kukaa kwao, mtambikaji akiwa hajafa bado.

33Wala msiipatie uchafu hiyo nchi, mtakayoiingia. Kwani damu huipatia nchi uchafu, tena haiwezekani kuipatia hiyo nchi upozi wa hiyo damu iliyomwagika kwake, isipokuwa kwa damu yake yeye aliyeimwaga hiyo damu.[#1 Mose 9:6.]

34Kwa hiyo msiichafue hiyo nchi, ninyi mtakayoikaa, mimi nami nitakakokaa; kwani mimi Bwana nitakaa katikati ya wana wa Isiraeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania