Mashangilio 102

Mashangilio 102

Kuomba kwa mnyonge, Sioni ujengwe tena.

(Wimbo wa juto wa 5.)

1Maombo ya mnyonge; kwa kufikisha kuzimia roho anamtolea Bwana wasiwasi wake.

2Bwana, lisikilize ombo langu! Kilio changu sharti kifike kwako wewe.

3Usiufiche uso wako, nisiuone ninaposongeka! Nitegee sikio lako, ninapokuita, uniitikie upesi!

4Kwani siku zangu hupotea kama moshi, nayo mifupa yangu huchomwa kama vijinga vya moto.

5Moyo wangu umeungua, ukanyauka kama majani, kwa hiyo mimi husahau kula chakula changu.

6Kwa hivyo, ninavyolia na kupiga kite, nyama za mwili wangu zimegandamana nayo mifupa.[#Iy. 19:20.]

7Nimefanana na korwa wa huko jangwani, nikawa kama bundi akaaye mahameni.

8Ninalala macho kwa kulia, ninafanana na ndege aliyeachwa peke yake kipaani juu.

9Siku zote adui zangu hunisimanga, hunizomea na kuapa, nipatwe na mabaya.

10Kwani ninakula uvumbi, kama ni mkate, navyo vinywaji vyangu ninavichanganya na machozi,[#Sh. 80:6.]

11kwa sababu umenitolea makali na kunichafukia, kisha ukanikamata, ukanibwaga.

12Siku zangu ni kama kivuli kilicho kirefu, nami nimenyauka kama majani.[#Sh. 90:5; Iy. 14:2.]

13Lakini wewe, Bwana, utakaa kale na kale, kwa vizazi na vizazi utakumbukwa.

14Wewe utakapoinuka, uhurumie Sioni! Kwani siku za kuuonea uchungu sasa ziko, kweli imekwisha kufika saa yake.[#Sh. 14:7.]

15Kwani watumishi wako hupendezwa, mawe yake yakitumiwa; tena jinsi yanavyokaa uvumbini, inawatia uchungu.

16Ndipo, wamizimu watakapoliogopa Jina lake Bwana, nao wafalme wote wa nchi watauogopa utukufu wako.

17Hapo, Bwana atakapokuwa ameujenga tena mji wa Sioni, ndipo, utakapokuwa umetokea nao utukufu wake.

18Atayageukia maombo yao walio wakiwa, maana yale maombo yao hakuyabeza.

19Hayo sharti yaandikiwe vizazi vitakavyozaliwa nyuma, nao wa ukoo utakaoumbwa sharti wamshangilie Bwana.

20Kwani alichungua toka Patakatifu pake palipo juu toka mbinguni aliitazama nchi hii,

21awasikilize waliofungwa, wakimpigia kite, nao walio wana wa kifo awafungulie njia,[#Sh. 79:11.]

22wapate kulitangaza mle Sioni Jina lake Bwana pamoja na kumshangilia mlemle Yerusalemu,

23makabila ya watu yatakapokusanyika yote pia pamoja na wafalme, wamtumikie Bwana.[#Sh. 87:4.]

24Njiani alizipunguza nguvu zangu, nazo siku zangu akazifupiza.

25Nikasema: Mungu wangu, usiniondoe, siku zangu simefika kati tu! Miaka ikaayo kwa vizazi na vizazi ni yako wewe.[#Sh. 55:24.]

26Huko kale uliiweka misingi ya nchi, mbingu nazo ni kazi ya mikono yako wewe.[#Sh. 20:2; Ebr. 1:10-12.]

27Hizo zitaangamia, lakini wewe utasimama. Kweli, zote zitachakaa kama nguo; utakapozigeuza kama vazi, ndipo, zitakapogeuka.[#2 Petr. 3:10.]

28Lakini wewe ndiwe yuleyule uliyekuwa kale, miaka yako haitakoma.[#Sh. 102:13.]

29Wana wa watumishi wako watakaa nao, nao wa uzao wao watakaa usoni pako wakiwa wenye nguvu.[#1 Yoh. 2:17.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania