The chat will start when you send the first message.
1Mtukuze Bwana, roho yangu! Bwana Mungu wangu, u mkuu kabisa, yenye urembo na utukufu umeyavaa.
2Umejivika mwanga, kama ni kanzu, ukazitanda mbingu kama nguo za hema.
3Makao yake ya juu aliyawekea misingi ya majini, huyatumia mawingu kuwa gari lake, juu ya mabawa ya upepo hujiendea.
4Huwatumia malaika zake kuwa upepo, nao watumishi wake kuwa mioto iwakayo.[#Ebr. 1:7.]
5Aliishikiza nchi kwenye misingi yake, haitayumbayumba kale na kale;
6ukaivika vilindi vya maji, kama ni nguo, nako vileleni kwenye milima juu kulikuwa na maji, nayo yalikuwa yametulia kuko huko.
7Ulipoyakemea, yakakimbia, ulipoyapigia sauti za ngurumo, yakapiga mbio kujiendea.[#Sh. 74:12-13; Iy. 38:8-11.]
8Milima ikainukia kwendelea juu, mabonde yakatelemkia hapohapo, ulipoyatengenezea.
9Ukakata mipaka, maji yasiipite, yasirudi tena kuifunika nchi.
10Namo mabondeni ukatokeza chemchemi za maji, maji yapate kupita katikati ya milima.[#Sh. 74:15.]
11Nyama wote wa porini wakapata ya kunywa hukomesha kiu humo akina punda milia.
12Nao ndege wa angani hukaa kando ya maji, hupiga nyimbo zao wakikaa katika matawi ya miti.
13Milima ukainywesha maji yatokayo juu, ukaishibisha nchi mapato ya kazi zako.
14Ukachipuza majani, nyama wapate kula, nayo maboga, watu wayatumie; ndivyo, ulivyovitoa vilaji huku mchangani,[#Sh. 147:8.]
15hata mvinyo zifurahishazo mioyo ya watu, nayo mafuta ya kuzing'aza nyuso zao, nayo mikate itiayo nguvu mioyoni mwa watu.[#Amu. 9:13; Mbiu. 10:19.]
16Hata miti ya Bwana hunywa, mpaka ishibe, kama miangati ya Libanoni, aliyoipanda yeye.
17Ndimo, ndege wanamojenga viota vyao, nazo nyumba zao makorongo ziko katika mivinje.
18Kwenye milima mikubwa ndiko, minde wanakokaa, magenge ni kimbilio lao wale pelele.
19Uliumba mwezi wa kujulisha vilimo, jua hupajua pake pa kuchwea.[#Sh. 19:7; 74:16.]
20Ukaiweka nayo giza, usiku uwepo; ndipo, nyama wa porini wanapotembea wote,
21wana wa simba hunguruma wakikosa nyama wa kukamata; ndivyo, wanavyomwuliza Mungu chakula chao.
22Jua linapokucha, wale hurudi kwao mapangoni mwao, wapate kulala.
23Kisha hutokea watu kwenda kazini, watumikie huko kazini mpaka jioni.
24Uliyoyafanya, Bwana, ni makuu, tena ni mengi! Yote pia uliyafanya kwa ubingwa ulio wa kweli, hivyo nchi ikapata kijana viumbe vyako.[#1 Mose 1:31.]
25Hapo ni bahari iliyo kubwa na pana pande zote; humo ndimo, wanamofurika wadudu wasiohesabika kabisa, tena nyama wadogo nao wakubwa.
26Humo zinapita nazo merikebu zenye mizigo, tena wamo nondo, uliowaumba wa kuchezea mle.
27Hawa wote wanakuelekea wakikutazamia, uwape vilaji vyao, wanapoona njaa.[#Sh. 145:15-16.]
28Ukiwapa, hukusanya, tena hulimbika, unapokifumbua kiganja chako, hushiba mema yako.
29Ukiuficha uso wako, wataguiwa na kituko, ukiondoa pumzi zao, huzimia, kisha hurudi uvumbini.[#1 Mose 3:19.]
30Unapoituma pumzi yako, wanaumbwa, nao uso wa nchi huurudishia upya.
31Utukufu wake Bwana ni wa kale na kale, naye Bwana huzifurahia kazi, alizozifanya.
32Akiitazama nchi, inatetemeka; akiigusa milima, inatoka moshi.[#Sh. 144:5.]
33Siku zangu zote za kuwapo nitamwimbia Bwana, nitampigia Mungu wangu shangwe nikingali nipo.
34Nyimbo zangu, nilizozitunga, na zimpendeze! Mimi ninayemfurahia, ndiye Bwana.
35Wakosaji sharti wamalizwe, wasiwepo nchini tean! Mtukuze Bwana, roho yangu! Haleluya!