The chat will start when you send the first message.
1Mshukuruni Bwana, nalo Jina lake litambikieni! Yajulisheni makabila ya watu matendo yake![#Yes. 12:4.]
2Mpigieni shangwe za kumwimbia! Mataajabu yake yote yatungieni tenzi!
3Lishangilieni Jina lake lililo takatifu! Mioyo yao wamtafutao Bwana na ifurahi!
4Mchungulieni Bwana nazo nguvu zake! Utafuteni uso wake siku zote!
5Yakumbukeni mataajabu yake, aliyoyafanya, nayo maamuzi yake yashangazayo yakisemwa na kinywa chake!
6Ninyi mlio wa uzao wake Aburahamu aliyemtumikia, nanyi wana wa Yakobo, yeye aliyemchagua!
7Yeye Bwana ni Mungu wetu, nchi zote anaziamua.
8Kale na kale analikumbuka Agano lake. aliowaagiza kulishika Neno lake, ni vizazi elfu.
9Agano ni lile, alilomwekea Aburahamu, nacho kiapo ni kile, alichomwapia Isaka.
10Mbele yake Yakobo naye akalisimamisha kuwa maongozi, Agano lakale na kale liwe kwake Isiraeli
11kwamba: Wewe ndiwe, nitakayekupa nchi ya Kanaani, iwe fungu lenu, nililowapimia.[#1 Mose 12:7.]
12Vilikuwa hapo, walipokuwa kikundi cha watu wanaohesabika, maana kule walikuwa wachache tu, tena wageni.
13Wakawaendea watu wa huko, taifa kwa taifa, walipotoka kwa mfalme mmoja, wakawajia wenziwe.
14Lakini hakuna mtu, aliyempa ruhusa kuwakorofisha, hata wafalme akawapatiliza kwa ajili yao kwamba:[#1 Mose 12:17; 20:3,7.]
15Niliowapaka mafuta msiwaguse tu, wala wafumbuaji wangu msiwafanyizie mabaya!
16Akaita njaa, ije kuziingia nchi za watu, akaivunja miti yote izaayo vilaji.[#1 Mose 41:54.]
17Hapo alikuwa amekwisha kujipatia mtu, awafungulie njia, ni Yosefu aliyekuwa ameuzwa kuwa mtumwa.[#1 Mose 37:28.]
18Huyo miguu yake waliiumiza kwa kuitia katika mapingu, kisha wakamfunga mwenyewe kwa minyororo
19mpaka siku ile, lilipotimia lile neno lake; naye alikuwa ameng'azwa kwa kuyeyushwa na maneno yake Bwana.
20Ndipo, mfalme alipotuma, akamfungua; mtawala makabila ya watu akamtoa kifungoni.[#1 Mose 41:14.]
21Akamsimamisha kuwa bwana nyumbani mwake na mtunzaji wa mali, alizokuwa nazo zote,
22awafunge wakuu wake, kama apendavyo; kisha awafundishe wazee wake, waerevuke.
23Ndipo, Waisiraeli walipokuja huko Misri, Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu.[#1 Mose 46:1.]
24Bwana akawapa wao walio ukoo wake kuzaa sana, akawatia nguvu kuliko wao waliowasonga.[#2 Mose 1:7,12.]
25Kisha akaigeuza mioyo yao wale, wawachukize walio ukoo wake, wakawaendea watumishi wake kwa udanganyifu.
26Ndipo, alipomtuma mtumishi wake, yule Mose, naye Haroni, aliyemchagua.
27Hao wakafanya kwao vielekezo, alivyokuwa aliwaambia, wakavifanya vioja vyake katika nchi ya Hamu.[#2 Mose 3—12.]
28Akatuma giza, likaiguia nchi yao, nao hawakukataa kuyatii maneno yake.
29Akayageuza maji yao kuwa damu. akawaua nyama wote wa humo mtoni.
30Nchi yao ikafurikiwa navyo vyura, wakaingia namo nyumbani mwa mfalme wao.
31Mbung'o wakaja papo hapo, aliposema, katika mipaka yao yote wakaingia nao mbu.
32Penya mvua zao aliwanyeshea mvua ya mawe pamoja na mioto iliyoichoma nchi yao.
33Akaipiga mizabibu yao, hata mikuyu yao, akaiponda miti iliyokuwako katika mipaka yao.
34Nzige wakaja papo hapo, aliposema, pamoja na funutu wasiohesabika.
35Wakala majani yote katika nchi yao. wakala navyo vilaji vyote mashambani kwao.
36Akampiga kila mzaliwa wa kwanza katika nchi yao, ndio wote waliokuwa malimbuko yenye nguvu kwao.
37Alipokwisha kuwapatia fedha na dhahabu, ndipo, alipowatoa, tena katika koo zao hakuwamo aliye mwenye kilema.[#2 Mose 12:35.]
38Wamisri wakafurahi, walipotoka, kwani waliguiwa na kituko kilichowaogopesha.
39Akatanda wingu, liwafunike, kisha liwe lenye moto, uwamulikie usiku.[#2 Mose 13:21.]
40Walipomwomba, akaleta tombo, hata mikate alitoa mbinguni, akawashibisha.[#2 Mose 16:13-17; Yoh. 6:31.]
41Akafungua mwamba, maji yakabubujika, yakajiendea nyikani kama mto.[#2 Mose 17:6.]
42Kwani alilikumbuka Neno lake lililo takatifu, alilomwambia mtumishi wake Aburahamu.
43Ndivyo, alivyowatoa walio ukoo wake, wakafurahi, kwa kuwa wateule wake wakampigia vigelegele.
44Nchi zao wamizimu ndizo, alizowapa, navyo, makabila mengine yalivyovisumbukia, wakavitwaa tu.
45Alitaka hili tu: Wayaangalie maongozi yake, nayo Maonyo yake wayashike. Haleluya!