The chat will start when you send the first message.
1Mshukuruni Bwana, ya kuwa ni mwema! Ya kuwa upoke wake ni wa kale na kale![#Sh. 106:1.]
2Ndivyo, watakavyosema waliokombolewa na Bwana, aliowakomboa katika masongano.
3Ndio, aliowakusanya na kuwatoa katika nchi za ugeni, kule maawioni kwa jua nako macheoni kwake, nako kaskazini nako kwenye bahari.
4Walikuwa wamepotea nyikani katika njia za jangwani, mji uliokuwa wenye watu hawakuuona.
5Njaa ikawauma pamoja na kiu, roho zao zikataka kuzimia tu.
6Ndipo, walipomlilia Bwana kwa kusongeka hivyo, naye akawaopoa katika masumbuko yao.[#Sh. 107:13,19,28.]
7Akawaongoza katika njia iliyonyoka, wapate kufika mjini mwenye watu.
8Hao na wamshukuru Bwana, ya kuwa ni mpole! Huwafanyizia wana wa watu vioja vyake,[#Sh. 107:15,21,31.]
9hushibisha roho yenye kiu, nayo roho yenye njaa huipatia mema mengi.[#Luk. 1:53.]
10Wako wengine, walikaa gizani mwenye kufa, wakawa wamefungwa na kubanwa na vyuma.
11Kwani walikataa kuyatii maneno yake Mungu, wakalibeza shauri lake yule Alioko huko juu.
12Kwa hiyo aliinyenyekeza mioyo yao kwa kuwatesa, nao walipojikwaa, hakuwako aliyewasaidia.
13Ndipo, walipomlilia Bwana kwa kusongeka hivyo, naye akawaokoa katika masumbuko yao.[#Sh. 107:6.]
14Akawatoa gizani mwenye kufa, yale mafungo yao nayo akayavunja.
15Hao na wamshukuru Bwana, ya kuwa ni mpole! Huwafanyizia wana wa watu vioja vyake.[#Sh. 107:8.]
16Kwani milango ya shaba anaivunja, nayo makomeo ya chuma anayakata.
17Wako wengine waliopumbazwa na kuumizwa kwa ajili ya njia zao zenye mapotovu na kwa ajili ya kukora manza.
18Vilaji vyote vikazichafua roho zao, mwisho wakajifikisha huko, malango ya kifo yaliko.
19Ndipo, walipomlilia Bwana kwa kusongeka hivyo, naye akawaokoa katika masumbuko yao.[#Sh. 107:6.]
20Akalituma Neno lake, likawaponya, akawaopoa shimoni mwao.
21Hao na wamshukuru Bwana, ya kuwa ni mpole! Huwafanyizia wana wa watu vioja vyake.[#Sh. 107:8.]
22Na wamtolee vipaji vya tambiko vya kumshukuru wakiyasimulia matendo yake na kushangilia.[#Sh. 50:14.]
23Wako wengine waliosafiri baharini katika merikebu wakifuata uchuuzi kule kwenye maji mengi.[#Mat. 8:23-27.]
24Nao waliyaona matendo ya Bwana na vioja vyake kwenye vilindi.
25Kwa kusema tu alileta upepo wa kimbunga uliokweza mawimbi,
26yakawapandisha juu kwenda mbinguni, tena wakatelemka chini vilindini, roho zao zikayeyuka kwa hayo mabaya.
27Wakayumbayumba na kupepesuka kama mlevi, mizungu yao yote ikawa ya bure.
28Ndipo, walipomlilia Bwana kwa kusongeka hivyo, naye akawatoa katika masumbuko yao.[#Sh. 107:6.]
29Akakituliza kimbunga, kukawa kimya, mawimbi nayo yakanyamaza.
30Kwa kuwa yamepata kutulia, wakafurahi, kisha akawaingiza bandarini, walikotaka kwenda.
31Hao na wamshukuru Bwana, ya kuwa ni mpole! Huwafanyizia wana wa watu vioja vyake.[#Sh. 107:8.]
32Na wamtukuze kwenye mikutano ya watu walio wa ukoo wetu! Nako kwenye mashauri ya wazee na wamshangilie!
33Aligeuza mito mikubwa kuwa nyika, nazo mboji za maji kuwa nchi kavu.
34Nchi yenye wiva akaigeuza kuwa jangwa la chumvi kwa ajili ya ubaya wao waliokaa kule.[#1 Mose 19.]
35Tena nyika aliigeuza kuwa bwawa lenye maji mengi, nayo nchi kavu akaitokeza mboji za maji,
36akawapa wenye njaa ya kukaa hapohapo, wapajengee mji wa kukaa.
37Wakalima mashamba, wakapanda mizabibu, wakajipatiamo matunda, ndio malipo ya kazi zao.
38Kwa hivyo, alivyowabariki, wakawa wengi sana, nao nyama wa kufuga, aliowapa, hawakuwa wachache.
39Kisha wakapunguka tena, wakainamishwa chini kwa kulemewa na mabaya yaliyowasikitisha.
40Wakuu wao akawamwagia masimango, akawatangishatangisha maporini kusiko na njia zo zote.[#Iy. 12:21.]
41Lakini mkiwa alimkingia yale mateso, asifikiwe nayo, akaviweka vizazi vyake kuwa vingi kama kondoo.
42Wanyokao mioyo walipoviona wakavifurahia kwamba: Wapotovu wote hufumbwa vinywa![#Iy. 22:19-20.]
43Yuko nani aliye mwenye ujuzi? Na ayashike haya! Na autambue upole wake Bwana!