Mashangilio 115

Mashangilio 115

Mungu anapaswa na kutukuzwa.

1Sisi sio, Bwana, sisi sio tupaswao na kutukuzwa, ila Jina lako sharti ulipatie utukufu kwa ajili ya upole wako na kwa ajili ya welekevu wako.[#Yoh. 1:17.]

2Mbona wamizimu wanasema: Mungu wao yuko wapi?[#Sh. 42:4.]

3Lakini Mungu wetu yuko mbinguni, yote yampendezayo huyafanya.

(4-11: Sh. 135:15-20.)

4Vinyago vyao ni fedha na dhahabu, mikono ya watu ndiyo iliyovifanya:[#5 Mose 4:28; Yes. 44:9-20.]

5vinywa vinavyo, lakini havisemi, macho vinayo, lakini havioni,

6masikio vinayo, lakini havisikii, pua vinazo, lakini havinusi,

7mikono vinayo, lakini havipapasi, miguu vinayo, lakini haviendi, wala havisemi kwa koo zao.

8Kama hivyo vilivyo, ndivyo, watakavyokuwa nao waliovifanya, nao wote pia waviegemeao.

9Wewe Isiraeli, mwegemee Bwana! Yeye ni msaada wao na ngao yao.[#Sh. 118:2.]

10Ninyi mlio wa mlango wa Haroni, mwegemeeni Bwana! Yeye ni msaada wao na ngao yao.[#Sh. 118:3.]

11Ninyi mmwogopao Bwana, mwegemmeni Bwana! Yeye ni msaada wao na ngao yao.[#Sh. 118:4.]

12Bwana hutukumbuka, atubariki. Ataubariki mlango wao wa Waisiraeli, ataubariki nao mlango wake Haroni.

13Atawabariki wao wamwogopao Bwana, walio wadogo pamoja nao walio wakubwa.

14Bwana ataendelea kuwafanyia hivyo ninyi nao wana wenu watakaokuwa.

15Ninyi ndio mliobarikiwa naye Bwana aliyezifanya mbingu hata nchi.

16Mbingu ni mbingu zake yeye Bwana, nchi aliwapa wana wa watu.

17Bwana hawamshangilii walio wafu, wala wote walioshukia huko kuliko kimya.[#Sh. 6:6; Yes. 38:18.]

18Lakini sisi na tumkuze Bwana kuanzia sasa, hata kale na kale! Haleluya!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania