Mashangilio 118

Mashangilio 118

Shangwe zao waliookoka.

1Mshukuruni Bwana, ya kuwa ni mwema! Ya kuwa upole wake ni wa kale na kale![#Sh. 107:1.]

2Waisiraeli na waseme: Upole wake ni wakale na kale![#Sh. 115:9-13.]

3Walio wa mlango wa Haroni na waseme: Upole wake ni wa kale na kale!

4Wamwogopao Bwana na waseme: Upole wake ni wa kale na kale!

5Niliposongeka nalimwita Bwana, naye Bwana akaniitikia na kunipanulia.

6Bwana akiwa upande wangu, sitaogopa; maana aliye mtu atanifanyia nini?[#Sh. 56:5; Ebr. 13:6.]

7Bwana akiwa upande wangu na kunisaidia, ndipo, nitakapowafurahia wachukivu wangu.[#Sh. 54:9.]

8Kumkimbilia Bwana kunafaa kuliko kuegemea watu.

9Kumkimbilia Bwana kunafaa kuliko kuegemea wakuu.[#Sh. 146:3.]

10Wamizimu wote walikuwa wamenizunguka, vikawa kwa nguvu ya Jina la Bwana, nikiwaponda.

11Kweli walikuwa wamenizungukana kunizinga, vikawa kwa nguvu ya Jina la Bwana, nikiwaponda.

12Walikuwa wamenizunguka kama nyuki, wakazimia upesi kama moto wa miiba; vikawa kwa nguvu ya Bwana, nikiwaponda.[#Yes. 33:12.]

13Walizidi kunikumba, nianguke, lakini Bwana akanisaidia.

14*Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, maana alinijia, akawa mwokozi wangu.[#2 Mose 15:2.]

15Shangwe za kuushangilia wokovu huu husikilika kwenye vituo vyao waongofu: Mkono wa kuume wa Bwana hufanya yenye nguvu!

16Mkono wa kuume wa Bwana umetukuka, mkono wa kuume wa Bwana hufanya yenye nguvu!

17Sitakufa, ila nitakuwapo, niyasimulie matendo ya Bwana.

18Kweli Bwana hunichapa, lakini hanitoi, nife.[#2 Kor. 6:9.]

19Nifungulieni malango ya kuingia kwake wongofu, niingie humo, nimshukuru Bwana!

20Hili ndilo lango la kuingia mwake Bwana; waongofu ndio watakaoliingia.

21Ninakushukuru, kwa kuwa uliniitikia, maana ulinijia, ukawa mwokozi wangu.[#Sh. 119:71.]

22Jiwe, walilolikataa waashi, limekuwa la pembeni.[#Yes. 28:16; Mat. 21:42.]

23Hivyo vimefanywa na Bwana; nasi tukivitazama, ni vya kustaajabu.

24Hii ni siku, Bwana aliyoitengeneza; na tushangilie na kuifurahia!*

25E Bwana, tunakuomba: Tuokoe! E Bwana, tunakuomb: Tupe kushinda!

26Na atukuzwe ajaye kwa Jina la Bwana! Tuliomo Nyumbani mwake Bwana tunawabariki ninyi.[#Mat. 21:9; 23:39.]

27Bwana ni Mungu atuangazaye. Jipambieni sikukuu na kushika makuti, mje kufika kwenye pembe za meza iliyo ya kutambikia!

28Mungu wangu ni wewe, ninakushukuru; Mungu wangu, ninakutukuza.

29Mshukuruni Bwana, ya kuwa ni mwema! ya kuwa upole wake ni wa kale na kale!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania