The chat will start when you send the first message.
1Wenye shangwe ndio wao wanaofuata njia zisizokosesha, wanaoendelea kuyafuata Maonyo yake Bwana.[#Sh. 1:1-2; 112:1.]
2Wenye shangwe ndio wao wanaoyashika mashuhuda yake, wanaomtafuta yeye kwa mioyo yote.
3Hawafanyi mapotovu hata kidogo, ila njia zake ndizo, wanazoendelea kuzishika.
4Amri zako ulizitoa wewe mwenyewe, watu wazishike kabisa na kuzifuata.
5Ninataka sana, njia zangu zishupazwe, niyashike maongozi yako.
6Kwa kuyatazama maagizo yako yote sitatwezeka.
7Na nikushukuru kwa moyo unyokao, nikijifundisha wongofu wako wa kuamua.
8Na niyashike maongozi yako na kuyafuata, nawe usiniache, niwe peke yangu.
9Kijana ataiangaliaje njia yake, iwe imetakata? Itakuwa hapo, atakapolishika Neno lako na kulifuata.
10Nimekutafuta kweli kwa moyo Wangu wote, usiniache, nikapotea na kutoka kwenye maagizo yako.
11Moyoni mwangu nimeliweka Neno lako, nisije kukukosea.
12Utukuzwe, wewe Bwana! Nifundishe maongozi yako![#Sh. 119:26,64,68.]
13Kwa midomo yangu nimeyasimulia maamuzi yote ya kinywa chako
14nikaifurahia njia ya mambo, uliyoyashuhudia wewe, kama watu wanavyofurahiwa na mali zo zote.
15Amri zako na niziwaze moyoni na kuzitazama njia zako.
16Na nijichangamshe kwa maongozi yako, nisilisahau Neno lako![#Sh. 119:24,47,61; Rom. 7:22.]
17Mtendee mema mtumishi wako, nipate uzima tena! Na nilishike Neno lako na kulifuata!
18Yafumbue macho yangu, nipate kuona, niyaone mataajabu yatokeayo kwenye Maonyo yako.
19Mimi ni mgeni katika nchi, usinifiche maagizo yako![#Sh. 39:13.]
20Roho yangu imepondeka kwa kuyatunukia hayo maamuzi yako mchana kutwa.
21Uliwakaripia wenye majivuno, wakawa wameapizwa, wakapotea kwa kuyaacha maagizo yako.[#5 Mose 27:26.]
22Ondoa kwangu matwezo na mabezo! Kwani nayashika mashuhuda yako.
23Wako nao wakuu wanaopiga mashauri ya kuniteta, lakini mtumishi wako anayoyawaza moyoni, ndiyo maongozi yako.
24Mashuhuda yako hunichangamsha, ndiyo yanayoniongoza.[#Sh. 119:35.]
25Ambayo roho yangu imegandamana nayo, ndiyo mavumbi; kwa hivi nirudishe uzimani, kama ulivyosema!
26Nilipokusimulia, njia zangu zilivyo, uliniitikia; unifundishe maongozi yako, niyajue!
27Unitambulishe njia ya amri zako, niyawaze mataajabu yako!
28Roho yangu imeyeyuka kwa ukiwa; niinue, kama ulivyosema!
29Njia ya uwongo ipitishe mbali, nisiione! Kwa huruma zako nipe kuyashika Maonyo yako!
30Njia yenye kweli ndiyo, niliyoichagua, maamuzi yako nimeyaweka machoni pangu.
31Ambayo nimegandamana nayo, ndiyo mashuhuda yako; Bwana, usiniache, nikatwezwa!
32Nitapiga mbio, nifike njiani kwa maagizo yako, kwani moyo wangu umeupatia mahali papana.
33Nifunze, Bwana, niijue njia ya maongozi yako, niishike na kuifuata mpaka mwisho!
34Nitambulishe Maonyo yako, niyashike, niyaangalie na kuyafuata kwa moyo wote.
35Niendeshe katika mkondo wa maagizo yako! Kwani yanayonipendeza ndiyo hayo.[#Sh. 119:47.]
36Uelekeze moyo wangu, uyatazame mashuhuda yako, usiyatazame tena mapato ya faida.
37Yapitishe macho yangu, yasitazame mambo ya bure, ila yazitazame njia zako zinipazo uzima!
38Mpatie mtumishi wako uliyomwambia! Naye akuogope!
39Pitisha kwangu mambo yanitiayo soni! Kwani ninayaogopa, maana maamuzi yako ndiyo yaliyo mema.
40Tazama, jinsi ninavyozitunukia amri zako! Nawe kwa wongofu wako nipe uzima!
41Magawio ya upole wako, Bwana, na yanijie! Uniokoe, kama ulivyosema!
42Hivyo ndivyo, nitakavyomjibu anitukanaye, kwani egemeo langu ni Neno lako.
43Usiliondoe kabisa kinywani mwangu hilo Neno lililo kweli! Kwani maamuzi yako ndiyo, ninayoyangojea.
44Nami nitayaangalia Maonyo yako, niyafuate siku zote pasipo kukoma kale na kale.
45Nitajiendea palipo papana kwa kuzitafuta amri zako.
46Nayo mashuhuda yako nitayasimulia hata mbele ya wafalme pasipo kuona soni.[#Mat. 10:18; Rom. 1:16.]
47Na nijichangamshe kwa maagizo yako, maana nimeyapenda.[#Sh. 119:16,70.]
48Hata mikono yangu nitaiinulia maagizo yako kwa kuyapenda, nayo maongozi yako nitayawaza moyoni.
49Likumbuke Neno lako, ulilomwambia mtumishi wako! Maana ulisema, nilingojee.
50Hili ndilo lililonituliza moyo katika mateso yangu, kwani Neno lako ndilo lililonirudisha uzimani.[#Sh. 19:8.]
51Wenye majivuno hunifyoza na kuzidi sanasana, lakini sikuondoka kwenye Maonyo yako.
52Ninapoyakumbuka maamuzi yako, Bwana, uliyoyaamua tangu kale, ndipo, ninapoutuliza moyo wangu.
53Makali yenye moto yalikuwa yamenishika kwa ajili yao wasiokucha, walioyaacha nayo Maonyo yako.
54Maongozi yako ndiyo, ninayoyaimbia namo nyumbani, nilimotua nilipokuwa mgeni.
55Jina lako, Bwana, nalikumbuka nao usiku, niyashike Maonyo yako, niyafuate.
56Hizo ndizo mali zangu, nilizozipata, kwa kuwa nimezishika amri zako.
57Bwana ni fungu langu! ndivyo, nilivyosema; kwa hiyo nayashika maneno yako na kuyafuata.
58Nikakulalamikia usoni pako kwa moyo wote, unihurumie, kama ulivyoniambia.
59Nilipozitazama njia zangu, nikairudisha miguu yangu, nikaielekeza, iyafuate mashuhuda yako.
60Sikujizuzua na mambo mengine mengine, ila nikapiga mbio. niyashike maagizo yako na kuyafuata.
61Matanzi yao wasiokucha yalikuwa yamenizunguka, lakini Maonyo yako sikuyasahau.[#Sh. 119:83.]
62Nikiamka usiku wa manane, ninakushukuru, kwa ajili ya wongofu wako wa kuamulia watu.[#Sh. 42:9.]
63Wenzangu mimi ndio wote wakuogopao wewe, wanaozishika amri zako na kuzifuata.
64Upole wako, Bwana, ndio ulioieneza nchi. Nifundishe maongozi yako, niyajue![#Sh. 33:5.]
65Mtumishi wako umemfanyizia mema, kama ulivyosema, Bwana.[#Sh. 119:17,41.]
66Nifundishe utambuzi na ujuzi ulio mwema! Kwani maagizo yako nimeyategemea.
67Nilipokuwa sijanyenyekezwa bado, nilikuwa nimepotea lakini sasa nimelishika Neno lako, nilifuate.[#Sh. 119:75; Yes. 28:19.]
68Wewe ndiwe mwema, hufanya mema; nifundishe maongozi yako, niyajue.[#Sh. 119:12.]
69Wenye majivuno wametunga uwongo wa kunisingizia, lakini mimi ninazishika amri zako kwa moyo wote.[#Sh. 119:78.]
70Mioyo yao imenenepa kama yenye unono, nami huyachangamkia Maonyo yako.[#Sh. 119:77.]
71Kule kunyenyekezwa kumenifaa kwa kunifundisha maongozi yako.[#Sh. 118:21.]
72Maonyo ya kinywa chako ni mema kwangu kuliko maelfu ya vipande vya dhahabu na vya fedha.[#Sh. 19:11.]
73Mikono yako iliniumba na kunitengeneza; nipe kuvitambua, nijifundishe maagizo yako!
74Wakuogopao hufurahi wakiniona mimi, kwani Neno lako ndilo, ninalolingojea.
75Nimeyajua maamuzi yako, Bwana, kuwa yenye wongofu, maana umeninyenyekeza kwa welekevu.[#Sh. 119:67.]
76Upole wako sharti uje, unitulize moyo, kama wewe ulivyomwambia mtumishi wako.[#Sh. 109:21.]
77Machungu yako, uliyonionea, na yaje, nipatekuwa mzima tena! Kwani Maonyo yako hunichangamsha.[#Sh. 119:143.]
78Wenye majivuno watapatwa na soni, kwani hunipotoa bure, lakini moyoni mwangu mimi ninaziwaza amri zako.[#Sh. 119:85-86.]
79Wakuogopao na waje kuwa upande wangu pamoja nao wale wayajuao mashuhuda yako.
80Moyo wangu sharti uwe pasipo kosa kwa nguvu ya maongozi yako, kusudi soni za kunipata zisinijie.
81Roho yangu imezimia kwa kuutunukia wokovu wako, lakini Neno lako ndilo, ninalolingojea.
82Nayo macho yangu yamepata kiwi kwa kulichungulia Neno lako kwa kwamba: Itakuwa lini, utakaponituliza moyo?
83Kwani nimekuwa kama kiriba kilichoanikwa katika moshi, lakini maongozi yako sikuyasahau.[#Sh. 119:93.]
84Siku za mtumishi wako zilizobaki ni ngapi tena? Utawahukumu lini wao wanikimbizao?
85Hawa wenye majivuno wamenichimbia mashimo, nao ndio wasioyafuata Maonyo yako.[#Sh. 119:69.]
86Maagizo yako yote ni ya welekevu; lakini wao hunikimbiza bure, kwa hiyo nisaidie!
87Ilikuwa imesalia kidogo, wangenitowesha huku nchini, lakini amri zako sikuziacha.
88Kwa upole wako nirudishe uzimani! Ndipo, nitakapoyashika na kuyafuata mashuhuda ya kinywa chako.[#Sh. 119:149.]
89Bwana, Neno lako ni la kale na kale, lilitiwa nguvu kule mbinguni.[#Yes. 40:8.]
90Welekevu wako hukalia vizazi na vizazi. Ulipozishikiza nchi, zikapata kusimama;
91zimesimama mpaka leo kwa hivyo, ulivyozitengeneza, kwani vinavyokutumikia ni vyote pia.
92Kama Maonyo yako yasingalinichangamsha, ningaliangamia kwa kuteseka.[#Sh. 119:50; Yer. 15:16.]
93Kale na kale sitazisahau amri zako, kwani kwa nguvu zao umenirudisha uzimani.[#Sh. 119:109.]
94Niokoe mimi niliye wako kwa kuzitafuta amri zako.[#Sh. 119:45.]
95Wasiokucha huningojea, waniangamize; lakini mimi ninayatambua mashuhuda yako.
96Kila kitu niliuona mwisho wake, siku zake zilipotimia, lakini agizo lako halina mpaka.
97Maonyo yako nimeyapenda sanasana, ndiyo yaliyomo moyoni mwangu siku zote.[#Sh. 1:2.]
98Maagizo yako hunierevusha kuliko adui zangu, Kwani kale na kale ndiyo yaliyoko kwangu.[#5 Mose 4:6.]
99Akili zangu huzipita zao wafunzi wangu wote, kwani mashuhuda yako ndiyo, niyawazayo moyoni.
100Kwa utambuzi ninawapita nao wazee, Kwani nimeziangalia amri zako.
101Miguu yangu nimeikataza kushika njia mbaya yo yote, nipate kulishika Neno lako na kulifuata.
102Kwenye maamuzi yako sikuepuka, kwani wewe mwenyewe ulinifundisha, niyajue.
103Maneno yako ni matamu peke yao katika ufizi wangu, kinywani mwangu ni matamu kweli kuliko asali.[#Sh. 19:11.]
104Katika amri zako ndipo, utambuzi wangu ulipotoka; kwa hiyo ninachukizwa na kila njia ya uwongo.
105Neno lako ni taa miguuni pangu, hunimulikia njiani pangu.[#2 Petr. 1:19.]
106Nimejiapia, tena nitayafanya, niushike wongofu wako wa kuamua, niufuate.
107Bwana, nimenyenyekezwa sanasana; nirudishe uzimani, kama ulivyosema![#Sh. 119:67,71.]
108Vipaji, kinywa changu kinavyopenda kuvitoa, na vikupendeze, Bwana! Na unifundishe maamuzi yako, niyajue![#Sh. 19:14.]
109Roho yangu nakupelekea mkononi mwangu siku zote, maana Maonyo yako sikuyasahau.[#Sh. 119:141; 1 Sam. 19:5.]
110Wamenitegea matanzi wao wasiokucha, lakini sikupotea na kuziacha hizo amri zako.
111Mashuhuda yako ndio fungu langu la kale na kale, kwani ndiyo yanayoufurahisha moyo wangu.
112Nimeuelekeza moyo wangu na kwako, uyafanye maongozi yako kale na kale mpaka mwisho.
113Walio wenye mioyo miwili nimechukizwa nao, lakini Maonyo yako nimeyapenda.[#Sh. 31:7.]
114Wewe ndiwe ficho langu na ngao yangu, nalo Neno lako ndilo, ninalolingojea.[#Sh. 3:4.]
115Ondokeni kwangu, ninyi mfanyao mabaya! Mimi ninataka kuyashika maagizo yake Mungu wangu.
116Nishikize, kama ulivyoniambia, nipate uzima tena! Usinitie soni! Maana nimekungojea.
117Unitie nguvu, nipate kuokoka! Nami na niyatazame maongozi yako siku zote!
118Unawatupa wote wapoteao na kuyaacha maongozi yako, kwani udanganyifu wao ni wa bure.
119Wote wasiokucha huku nchini unawazoa kama mitapo ya chuma, kwa hiyo nimeyapenda mashuhuda yako.
120Kwa kukuogopa sana nyama za mwili wangu zimeguiwa na kituko, nayo maamuzi yako ninayaogopa.
121Nimefanya yaliyo sawa yenye wongofu, usinitoe na kunitia mikononi mwao wanikorofishao.
122Jitoe kuwa kole ya mtumishi wako, aone mema, wenye majivuno wasinikorofishe![#Sh. 19:14.]
123Macho yangu yamepata kiwi kwa kuuchungulia wokovu wako na kwa kulichungulia Neno lako lililo lenye wongofu.
124Mfanyizie mtumishi wako kwa upole wako! Nifundishe maongozi yako, niyajue!
125Mimi ni mtumishi wako, nipe utambuzi, nipate kuyajua mashuhuda yako!
126Siku zimetimia, Bwana afanye kitu, maana Maonyo yako wameyatengua.
127Kwa hiyo nimeyapenda hayo maagizo yako kuliko dhahabu, ijapo ziwe nzuri zaidi.[#Sh. 19:11.]
128Kwani ninaziwazia amri zako zote kuwa za wongofu, lakini njia yo yote ya uwongo nimechukizwa nayo.
129Mashuhuda yako ni ya kustaajabu; hii ndiyo sababu, roho yangu ikiyashika.
130Maneno yako yakifunuliwa huangaza, huwapa utambuzi nao waliopumbaa.[#Sh. 19:8.]
131Nimekifumbua kinywa changu, nikatweta kwa kuyatunukia maagizo yako.
132Geuka, unielekee mimi na kunihurumia, kama inavyowapasa wao walipendao Jina lako!
133Mwenendo wangu uutie nguvu, ulifuate Neno lako, upotovu uwao wote usije kunitawala![#Sh. 17:5.]
134Katika makorofi ya watu na unikomboe! Nami na nizishike amri zako na kuzifuata!
135Mwangazie mtumishi wako uso wako, unifundishe maongozi yako, niyajue!
136Macho yangu yanatoka vijito vya maji kwa ajili yao wasioyashika Maonyo yako na kuyafuata.
137Wewe Bwana ndiwe mwongofu, nayo maamuzi yako kunyoka.
138Mambo yanayopasa, uyashuhudie wewe, umeyaagiza kuwa yenye wongofu na welekevu kabisa.
139Wivu wa kunija umenizimisha roho, kwani wameyasahau maneno yako wao wanisongao.[#Sh. 69:10.]
140Neno lako liko, limeng'azwa kabisa, kwa hiyo amelipenda mtumishi wako.
141Mimi ni mdogo, ninabezwa, lakini amri zako sikuzisahau.[#Sh. 119:153.]
142Wongofu wako ndio wongofu ulio wa kale na kale, nayo Maonyo yako ndiyo ya kweli.
143Masongano na mahangaiko yamenipata, lakini maagizo yako ndiyo yanayonichangamsha.[#Sh. 119:174.]
144Mashuhuda yako ni yenye wongofu kale na kale, nipe kuyatambua, nipate uzima tena!
145Nimeita kwa moyo wangu wote, niitikie, Bwana! Maongozi yako na niyashike!
146Nimekuita wewe, na uniokoe! Nami nitayashika mashuhuda yako na kuyafuata.
147Nimejidamka na mapema, nikulilie, Neno lako ndilo, ninalolingojea.[#Sh. 119:114.]
148Zamu za usiku zinapokuwa hazijapokeana, niko macho, nipate kuliwaza Neno lako moyoni mwangu.
149Isikie sauti yangu kwa upoke wako! Bwana, kwa hivyo, maamuzi yako yalivyo, nirudishe uzimani![#Sh. 119:88,154,159.]
150Wakimbiliao mapotovu wamenikaribia, ndio watu walioyaacha mbali Maonyo yako.
151Wewe, Bwana, uko karibu, nayo maagizo yako yote ndiyo ya kweli.[#Sh. 119:86.]
152Tangu kale ninayajua mashuhuda yako, nayo yalinifundisha, ya kuwa uliyawekea msingi, yawepo kale na kale.
153Utazame ukiwa wangu, uniopoe! Kwani Maonyo yako sikuyasahau.[#Sh. 119:176.]
154Nigombee kondo yangu, unikomboe! Nirudishe uzimani, kama ulivyoniambia!
155Wokovu unawakalia mbali wao wasiokucha, kwani hawakuyatafuta maongozi yako!
156Huruma zako, Bwana, ulizotupatia, huwa nyingi, kwa hivyo, maamuzi yako yalivyo, nirudishe uzimani!
157Wanaonikimbiza nao wanaonisonga ndio wengi, lakini sikuondoka na kuyaacha mashuhuda yako.
158Nikiwatazama waliorudi nyuma kwa udanganyifu najiliwana kutapika, kwa kuwa hawakulishika Neno lako na kulifuata.
159Tazama, jinsi ninavyozipenda amri zako! Bwana, kwa upole wako nirudishe uzimani!
160Neno lako lote zima ni la kweli, wongofu wako wa kuamua yo yote ni wa kale na kale.[#Yoh. 17:17.]
161Wao walionikimbiza bure ndio wakuu, lakini moyo wangu unaloliogopa sana, ni Neno lako.
162Mimi ninayafurahia, uliyoyasema, kama mtu atokaye vitani mwenye mateka mengi.
163Uwongo nimeuchukia, hunitapisha; Maonyo yako ndiyo, ninayoyapenda.
164Ninakushangilia kila siku mara saba zote kwa ajili ya wongofu wako wa kuamulia watu.
165Wayapendao Maonyo yako hupata utengemano mwingi, hawaoni lo lote litakalowakwaza.
166Bwana, wokovu wako nimeutazamia, nayo maagizo yako nimeyafanya.[#1 Mose 49:18.]
167Roho yangu imeyashika na kuyafuata mashuhuda yako, maana nimeyapenda sanasana.
168Nimezishika amri zako na kuzifuata, nayo mashuhuda yako, kwani njia zangu zote ziko machoni pako.[#Sh. 18:22.]
169Malalamiko yangu na yakufikie karibu usoni pako, Bwana! Kama ulivyosema, nipe utambuzi!
170Maombo yangu na yakujie usoni pako! Kama ulivyoniambia, uniponye!
171Shangwe na zifurike midomoni mwangu, kwa kuwa ulinifundisha maongozi yako!
172Ulimi wangu na uliitikie Neno lako! Kwani maagizo yako yote ni yenye wongofu.[#Sh. 1:2; Fano. 6:22.]
173Mkono wako na uje kunisaidia mimi! Kwani amri zako ndizo, nilizozichagua.
174Wokovu wako, Bwana, nimeutunukia, nayo Maonyo yako ndiyo yanayonichangamsha.[#Sh. 119:16.]
175Roho yangu na ipate uzima tena, ikushangilie! Nayo maamuzi yako na yanisaidie!
176Nikipotelewa na njia kama kondoo aliyepotea, mtafute mtumishi wako! Kwani sikuyasahau maagizo yako.[#Sh. 119:16; Yes. 53:6; Luk. 15:3-7.]