Mashangilio 147

Mashangilio 147

Kumtukuza Mungu.

1Haleluya! kwa kuwa ni vema kumwimbia Mungu wetu, ni vizuri kumshangilia, nako kunapasa.[#Sh. 92:2.]

2Anayeujenga Yerusalemu ndiye Bwana, nao Waisiraeli waliotawanyika anawakusanya.

3Yeye anawaponya waliovunjika mioyo, ndiye anayewafunga vidonda vyao, walipoumizwa.[#Yes. 61:1.]

4Ndiye anayekiweka kiwango cha nyota, zote anaziita majina.[#Yes. 40:26.]

5Bwana wetu ni mkubwa mwenye nguvu nyingi, matambuzi yake hayahesabiki.

6Bwana ndiye anayewaegemeza watesekao, tena ndiye anayewakumba wasiomcha, waanguke chini.[#Luk. 1:52.]

7Mwitikieni Bwana na kumshukuru! Mwimbieni Mungu wetu na kupiga mazeze!

8Yeye ndiye anayeifunika mbingu kwa mawingu, naye anayezinyeshea nchi mvua ndiye yeye, ndiye anayechipuza majani huko milimani.

9Yeye ndiye anayewapa nyama vilaji vyao, nao makinda ya kunguru wamliliao.[#Iy. 38:41; Luk. 12:24.]

10Nguvu kubwa za farasi hazifurahii, wala hapendezwi na miguu ya mtu;

11Bwana hupendezwa nao wamwogopao, nao wanaoungojea upole wake.

12Yerusalemu, msifu aliye Bwana! Mshangilie Mungu wako, wewe Sioni!

13Kwani makomeo ya malango yako anayatia nguvu, anawabariki watoto, ulio nao.

14Utengemano ndio, anaoipatia mipaka yako, anakushibisha ngano zilizo nzuri kuliko nyingine.[#Sh. 81:17.]

15Hutuma amri yake kufika katika nchi, maneno yake huendelea upesi sana.

16Hunyunyiza manyunyu ya theluji, yaking'aa kama pamba, ni wingu la baridi liyamwagalo, yamwagike kama majivu.[#Sh. 148:8; Iy. 38:22-30.]

17Mawe ya mvua huyatupa, kama ni kokotokokoto, yuko nani atakayeweza kusimama kwenye baridi hiyo?

18Lakini akisema neno tu, yanayeyuka, akituma upepo wake, yanageuka kuwa maji, yajiendee.

19Yeye ndiye anayemtangazia Yakobo maneno yake, nayo maongozi yake na maamuzi yake huwatangazia Waisiraeli.

20Hivyo hakuvifanyizia wamizimu wo wote, nayo maamuzi yake hakuwajulisha. Haleluya![#5 Mose 4:7; Tume. 14:16; Rom. 3:2.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania